OFISA Habari wa Halmashauri ya Mji wa Masasi,  Clarence Chilumba amefariki dunia leo wakati akipelekwa kwa matatibu zaidi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kujeruhiwa kwenye ajali ya pikipiki.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Masasi ilisema Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Gimbana Emmanuel anasikitika kutangaza kifo cha ofisa habari huyo kilichotokea wakati akiwa njiani kupelekwa Muhimbili.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Chilumba ambaye pia alikuwa akiandikia HabariLeo na Uhuru kutokea mkoani Mtwara, alipata ajali ya pikipiki Agosti 31, mwaka huu jioni mjini Masasi wakati akitokea kazini kuelekea nyumbani kwake.

Taarifa hiyo ilisema baada ya kupata ajali aliwahishwa katika hospitali ya Mkomaindo ambapo alipatiwa huduma ya kwanza, baadaye kupelekwa Ndanda, hata hivyo hali yake ilizidi kuwa mbaya, ndipo Septemba mosi alipata rufaa kwenda Muhimbili.

Saa 8:00 usiku wa kuamkia leo akiwa njiani Somanga kuelekea Muhimbili alifariki dunia na kwamba taarifa za mazishi zitatolewa baada ya kuwasiliana na ndugu wa marehemu.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mtwara, Hassan Simba amethibitisha kufariki kwa Chilumba aliyekuwa mwanachama wa klabu hiyo.

Simba alisema Chilumba alifikwa na mauti njiani akiwa anapelekwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili(MOI) kwa matibabu zaidi baada ya kupata ajali ya pikipiki mjini Masasi.

Akizungumza na gazeti hili, Simba alisema baada ya mwajiri wake na familia kuzungumza wamekubaliana marehemu Chilumba atazikwa kesho saa 8:00 mchana kijijini kwao Malolo, kata ya Nangumbu, wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.

“Hivi sasa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Masasi, kesho asubuhi tutaondoka kwenda kijijini kwa marehemu Malolo, kwa ajili ya shughuli za maziko zitakazofanyika saa 8:00 mchana,” alisema.

Simba akielezea zaidi alisema Chilumba alipata ajali Agosti 31 wakati akiwa katika shughuli za kiofisi ambapo alitoka kufuatilia kwa mkandarasi uwekaji wa mabango ya kuhimiza kulipa kodi kwa hiari, akiwa amepakizwa kwenye pikipiki kama abiria.

Kwa mujibu wa Simba wakati wakiingia barabara kubwa ya Masasi-Newala waligongana na pikipiki nyingine ambayo nayo ilikuwa na watu wawili. Baada ya ajali hiyo dereva wa pikipiki aliyokuwa amepanda Chilumba alivunjika mguu na kulazwa hospitali ya Ndanda na jana aliruhusiwa na majeruhi wa pikipiki iliyowagonga pia walijeruhiwa na wanaendelea vizuri.

Simba alisema Chilumba alivunjika mguu wa kulia lakini pia alijeruhiwa  kichwani kwani alidondoka chali na huenda damu ilikuwa ikivujia ndani kwani hali ilibadilika na kuwa mbaya ndipo ikaamuliwa akimbizwe Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Ameacha mke na watoto.
REST IN PEACE KAKA 

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO