WANAFUNZI wa kidato cha tano na sita wa shule ya sekondari Mwanzi, wilayani Manyoni mkoani Singida ambao walilazimika kurejea nyumbani baada ya bweni lao kuteketea kwa moto, wanatarajia kurejea shuleni Jumapili wiki hii.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Jane Lubasi akizungumza kwa njia ya simu alisema kwamba maandalizi ya kuwawezesha wanafunzi hao kurejea na kuendelea na masomo yamefanyika na kwamba kwa kiasi kikubwa yamekamilika.

Alisema wanafunzi hao watakaa katika eneo la muda wakati bweni jipya linalojengwa likiendelea kumalizwa. Bweni hilo lililoungua Septemba 9 usiku wakati wanafunzi wakiwa katika maandalizi ya masomo na limesababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 50.

Thamani hiyo ilitajwa wakati Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Geofrey Mwambe akimpa taarifa Mkuu wa mkoa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ambaye alifika shuleni hapo kuangalia tukio hilo.  Mwambe alisema mali mbalimbali za wanafunzi zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 25 zimeteketea, huku hasara ya Sh milioni 24.3 ikipatikana kutokana na jengo hilo kuharibika.


Moto huo ulioanza saa 2:00 usiku wa kuamkia Septemba 10 umeteketeza kila kitu cha wanafunzi hao ambao walikuwa madarasani wakijiandaa na mitihani yao ya kawaida ya ndani. Hilo ni bweni la shule pekee wilayani Manyoni yenye kidato cha tano na sita na lilikuwa na wanafunzi 40.

Mwalimu Lubasi  alisema kwamba wananchi na serikali wameitikia wito wa kusaidia kurejesha shule hiyo katika hali ya kawaida hasa wanafunzi wake wanaokaa bweni.

“ Sina hakika na kiwango cha michango lakini huku tayari walimu wa shule mbili Mwanzi sec walimu wamechangia mifuko 33 ya sementi na Manyoni Sec pia wamechangia mifuko 22 ya sementi.Michango mingine tuliyopokea ni sare za wanafunzi, magodoro,mashuka, mablanketi, sabuni na vingine vidogovidogo kutoka halmashauri ya wilaya na wadau” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe  wakati alipofika shuleni hapo aliagiza timu maalumu iundwe kubaini chanzo cha moto huo  katika bweni hilo ambapo vitu vichache vimeweza kuokolewa. Bweni lilikuwa la vyumba vitatu ambalo vyumba viwili kuta zake zimebomoka kabisa.

“Pamoja na uchunguzi wa awali kuonesha uwezekano wa moto huo kusababishwa na hitilafu ya umeme, tusibweteke, lazima uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo cha moto huu,” alisema Mtigungwe na kuongeza kuwa kama kuna watu wamehusika, wakamatwe na kufikishwa mbele vyombo vya sheria.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO