TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bw. Evarist Ndikilo atoe wiki mbili kwa wakuu wa taasisi za umma na za binafsi wajieleze ni lini wataendeleza viwanja vya ofisi walivyopewa mjini Kibaha. 
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Septemba 21, 2016) wakati akizindua Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2015 - 2020) na Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, Kibaha, mkoani Pwani. 
Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo kwamba kuna taasisi za umma na za binafsi ambazo zimepewa viwanja vya kujenga Ofisi kwa zaidi ya miaka mitatu lakini zimeshindwa kuviendeleza hadi sasa wakati kuna watu bado wana shida ya kupatiwa viwanja. 
“Kibaha ni kimbilio la mkoa wa Dar es Salaam, kule kumejaa na hapa kuna nafasi kwa hiyo hawa ambao hawajaendeleza waandikie barua leo hii hii na uwape wiki mbili waeleze ni lini watakuwa tayari kuanza kazi hiyo.” 
Waziri Mkuu amezitaja taasisi hizo kuwa ni HAZINA Ndogo yenye viwanja viwili ambapo kiwanja kimoja chenye namba 232 kimeendelezwa lakini kiwanja kingine chenye namba 221 bado hakijaendelezwa. Taasisi nyingine na viwanja vyao kwenye mabano ni Chuo Kikuu Huria (kitalu na. 228), Njuweni Institute (kitalu na. 229), TANESCO (kitalu na. 218), TRA (kitalu na. 233) na SF Group (kitalu na. 225). Vingine ni vya Benki ya CRDB na TAKUKURU ambavyo hakutaja namba za vitalu vyake.      
“Najua kuna watu wa Serikali watasema hawana bajeti, lakini Bunge la bajeti linaanza Aprili mwakani. Kwa hiyo, wajipange kwenye bajeti ijayo, ili ifikapo Julai mosi, 2018 hawajafanya kitu, tuwachukulie hatua. Tuchukue viwanja vyetu tuwape wengine, na hawa wanaosuasua, tuwaache ili watakapokuwa tayari waombe upya na tutawapa wakati mwingine,” amesema. 
Amemtaka Bw. Ndikilo awawekee deadline ya kujieleza katika barua hizo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
JUMATANO, SEPTEMBA 21, 2016.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO