Mkurugenzi wa Halmashuri ya Mji Njombe Bi.Illuminatha Mwenda akionesha upendo kwa kumbeba mtoto Caren anayelelewa katika kituo cha kulelea watoto cha Imiliwaha Mission mara baada ya kutembelea kituo chao na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo Mafuta,sukari na sabuni za kufulia. 

HALMASHAURI ya  Mjini Njombe imetoa msaada wenye thamani ya shilingi milioni 1.3 kwa vituo viwili vya watoto yatima, Uwemba Mission na Imiliwaha Mission.
Akiambatana na wataalamu kutoka idara ya maendeleo ya jamii wakati wa kukabidhi mahitaji ya sabuni, mafuta, sukari, nepi za watoto na mafuta ya kupikia,  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Illuminatha Mwenda alisema halmashauri yake kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii inatambua uwepo wa watoto wenye mahitaji kama  hayo na ndio maana imechukua jukumu la kusaidia vituo hivyo.
 “Watoto mnaowalea hapa ni wadogo sana, na tukiangalia hali ya hewa ya Mkoa wetu wa Njombe una baraka ya kupata mvua nyingi sana kwa kipindi kizima cha Mwaka. Takribani miezi mitatu tu kwenye mwaka mzima ndio inaweza kuwa sio ya mvua. Naamini kwamba Kwa kipindi chote mvua zinapokua zinanyesha mahitaji ya nepi kwa watoto ni ya muhimu na yanahitajika kwa wingi sana.Si hayo tuu lakini pia zitawasaidi kwenye kuwabadili watoto, kuwafanya wakavu muda wote na kuwaweka katika hali ya usafi,” alisema Mkurugenzi Mwenda.
Aidha, mlezi wa kituo cha kulelea watoto cha Imiliwaha alisema kuwa anaishukuru halmashauri kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii kwa Misaada ya mara kwa mara ambayo wamekua wakikipatia kituo hicho na kusema kuwa watoto hao wanapotembelewa husaidia kujenga upendo miongoni mwa watoto vilevile kujiona wao sio kundi lililosahaulika katika jamii.
“Mkurugenzi tunakushukuru sana kwa kweli mnapotutembelea na sisi mnatupa moyo wa kuendelea kuwasaidia hawa watoto. Changamoto ni nyingi kwenye malezi ya hawa watoto kwani tunapokea watoto wa kila aina, wengine wanaugua magonjwa tofauti. Lakini sisi hatutakata tamaa ya kuendelea kuwasaidia kwani tunatambua fika hata tukikwama wapo watu waliopo nyuma yetu.
Mwenyezi Mungu awabariki sana na awarejeshee pale amlipotoa,” alisema mlezi huyo.
Halmashauri ya Mji Njombe imejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa katika kila robo ya mwaka makundi yenye mahitaji maalumu yanafikiwa kwa namna yoyote bila kujali hali zao za kimaisha.
Sopurce:Hyasinta Kissima.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO