JESHI la Polisi Mkoani Dodoma limekiri kumhoji Mbunge wa
Mtera,Livingstone Lusinde kwa dakika 45 kuhusiana na tukio la mauaji
ya kikatili ya watafiti watatu wa kituo cha Utafiti cha Selian Arusha
(SARI) baada ya kubainika alikuwa na mawasiliano kwa njia ya simu na
baadhi ya wananchi wa eneo hilo siku ya tukio.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma Lazaro Mambosasa alisema hayo jana
mjini hapa wakati wa mkutano na waandishi wa habari ambapo mmoja ya
waandishi hao alitaka ufafanuzi kama ni kweli Mbunge huyo alihojiwa na
jeshi a Polisi kuhusiana na mauaji hayo.
Alisema walimhoji Lusinde kwa dakika 45 baada ya kutajwa na baadhi ya
wakazi hao kuwa alikuwa na mawasiliano ya simu na baadhi ya watu wa
eneo hilo.
“Ni Kweli Mbunge Lusinde alihojiwa kuhusiana na mauaji ya Iringa
Mvumi, tuna taaluma ya upelelezi wa kesi za jinai katika hili tulipata
taarifa kama kulikuwa na  mawasiliano kati ya Mbunge na wananchi”
alisema
Kamanda Mambosasa alisema licha ya kumhoji Mbunge huyo lakini
hawakupata viunganishi vya kumuunganishana na tuhuma hizo.
“Kama angehusika moja kwa moja angepelekwa mahakamani,” alisema
kamanda Mambosasa.
Hivi karibuni baada ya kuchapishwa taarifa za kuhojiwa na Jeshi la
Polisi, mbunge huyo alikuja juu na kudai kuwa taarifa hizo zilikuwa za
kizushi huku akitishia kulishtaki gazeti hili.
Wakati akitoa ufafanuzi wa taarifa  awali ambayo gazeti hili iliripoti
juu ya kuhojiwa kwake na jeshi la polisi, Lusinde alisema akiwa kama
kiongozi wa
Jimbo hilo analaani tukio baya la kumwaga damu za watu wasio na hatia
Pia aliwataka wananchi waliokimbia  kurudi kwenye makazi yao na kutoa
ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili wote waliohusika katika tukio hilo
waweze kukamatwa.
“Sijawahi kuhojiwa kuhusu uchochezi na taarifa hizo si za kweli
zimeniletea usumbufu mkubwa” alisema. Nimesikitishwa na taarifa kuwa
nilihojiwa na polisijuu ya tukio la kuuawa kwa watafiti, jambo ambalo
si kweli tangu niwe kiongozi sijawahi kuchochea wananchi kwa jambo
lolote” alisema.
Alisema amekuwa Mbunge katika jimbo la Mtera kwa kipindi cha pili sasa
 hakuwahi kushuhudia watu wakifanya matukio ya kinyama kama
lililotokea Iringa Mvumi.
“Siku ya tukio sikuwa kijijini Iringa Mvumi nilikuwa kwenye ziara ya
Waziri Mkuu na tangu uchaguzi umepita sijawahi kufanya mkutano wowote
kwenye kile kijiji” alisema.
Alisema amekuwa akifanya kazi kama timu na madiwani na wenyeviti wa vijiji.
“Kichwa cha habari kuwa Lusinde ahojiwa kuhusiana na mauaji ya
watafiti hakikuwa na ukweli wowote, habari ile imenipa usumbufu mkubwa
na kupewa pole nyingi na hata kupigiwa simu” alisema
Alisema alikwenda kituo cha Polisi kwa ajili ya kuwasalimia viongozi
na wananchi ambao wako mahabusu kuhusiana na tukio lile akiwemo Diwani
Robert Chipole, Mwenyekiti wa Kijiji Albert Chimanga na alipata fursa
ya kuwaona na kuwasalimia viongozi hao na mwananchi mmoja aitwaye Noco
Kwanga.
Akizungumza jana Kamanda Mambosasa alisema katika tukio hilo tayari
watu 13 wamefikishwa mahakamani.
Alisema kabla ya mauaji hayo watuhumiwa walieneza taarifa za uongo
kuwatuhumu watafiti hao kuwa ni wanyonya damu (mumiani) au au kwa
lugha yao waliwaita ‘Wanyobanyoba’ na kuwaua pasipo kuwahoji japo
walikuwa na vitambulisho, barua ya utambulisho kutoka halmashauri ya
Chamwino na gari la serikali. Alisema tukio hilo lilihusisha watu
wengi ambapo wengine walitoroka kwenda mafichoni, msako mkali
unaendelea na kuwakamata wote waliohusika ili kufikishwa mahakamani
kuungana na wenzao.
Kamanda Mambosasa alisema kati ya watu 30 waliokuwa wakishukiliwa
tayari 13 wamepelekwa mahakamani na 17 wameachiwa.
“Bado tunaendelea kuwatafuta kila aliyeshiriki siku ya tukio
atakamatwa ili nao wajutie kitendo walichofanya” alisema
Alisema wengi waliokimbia ni wahusika wa tukio hilo na jeshi la polisi
litawasaka na kuwakamata.
Waliouawa katika tukio hilo ni Nicas Magazine (53), dereva, Faraja
Mafuru (27) na Theresia Nguma (42) ambao ni watafiti.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO