Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi Halmashauri ya Mji Njombe inakadiriwa kuwa ni wastani wa asilimia 14.8% kwa ngazi ya Mkoa. Hii ikimaanisha kuwa kwa kila watu 100, watu 15 wanaishi na VVU.
Akiwasilisha taarifa ya kiwango cha maambukizi katika Halmashauri ya Mji Njombe Kwa wadau wa mapambano ya Ukimwi Mkoa wa Njombe, Mratibu wa UKIMWI Katika Halmashauri, Daniel Mwasongwe amesema kuwa kiwango cha maambukizi ni kibaya.
“Leo hii tumekutana na ninyi wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya Ukimwi lengo ikiwa ni kupunguza maambukizi mapya na kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Tunaamini katika mdahalo huu wa wadau tutatoka na maazimio mazuri ambayo hayataishia mezani bali tutayapeleka kwenye utendaji ili kuhakikisha maambukizi mapya hayatakuepo tena, na Halmashauri yetu inaendelea kuwa salama.”
Akifafanua sababu zinazopelekea kiwango hicho kuendelea Mratibu huyo amesema kuwa sababu kuu zilizopelekea kiwango hicho kuendelea Ni pamoja Na sababu za Kibaiolojia, mabadiliko ya kitabia, vichocheo vya Kijamii na masuala ya kiuchumi likihusisha pia suala la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Kwa upande wake msimamizi wa huduma za wagonjwa nyumbani katika Halmashauri ya Mji Njombe amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya uhaba wa vituo vichache vya kutolea huduma za dawa jambo ambalo limeleta kero kubwa, kwa watumia dawa kutokana na kutembea umbali mrefu na kuingia gharama kubwa za usafiri kufuata vituo vya kutolea dawa na kusababisha kasi ya maambukizi kuendelea na hivyo wameiomba serikali na wadau kuongeza vituo vya huduma ili kuwezesha upatikanaji wa dawa maeneo ya karibu.
 Ameendelea kusema ipo kasumba ya upande wa watu waliopima na kugundulika kuwa na maambukizi kutokuwa wafuasi wakubwa wa dawa na wameitaka jamii kuongeza jitihada za uhamasishaji, utoaji elimu kwa watumia dawa waendelee kuwa wafuasi wazuri wadawa.
“Wamepima na wameshaingia kwenye huduma ukweli asilimia kubwa sio wafuasi wazuri wa dawa, nguvu zote za serikali na hata mdahalo wa wadau wa leo tunawatazama wale ambao wameshaingia kwenye huduma. Tunataraji kuwa hawa ambao wameshaingia kwenye huduma wakimeza dawa kwa miongozo mizuri hawatasababisha maambukizi kuhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine hivyo ni jukumu letu kupitia mdahalo huu kuongeza jitihada za kuhimiza watu wanaochukua dawa.” Alisema Rustica
Akiwasilisha salamu za Pongezi kwa serikali Mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi na Maambukizi Taifa (NACOPHA) Justine Mwinuka Amesema wanaishukuru serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwani imewapa usahihi na uhalali wa huduma ya ARV ambao kwao wafuasi wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Aidha ameendelea kusema kuwa miongoni mwa maazimio ya kitaifa na ambayo halmashauri imeanza kutekeleza ni pamoja na uundwaji wa baraza la WAVIU ngazi ya halmashauri lijulikanalo kama KONGA kwa ajili ya utetezi, shuhuda na uratibisha.
“Tunashukuru Baraza la Taifa na wenzetu wa TB kwa kuunda mahusiano kutoka ngazi ya Taifa hadi ngazi ya jamii na ndio maana ndani ya Halmashauri kuna KONGA. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila   palipo na mkusanyiko wa kiutendaji wa serikali na sisi sauti ya WAVIU na TB tunakuwepo ndani yake kwa ajili ya kuisaidia serikali kupanga mipango yake kupitia shuhuda tulizo nazo sisi tuliosaidiwa lakini pia kuwashawishi wadau mbalimbali ambao wamekua kwenye mapambano haya.”Alisema Mwinuka.
Mwinuka alisema kuwa kumekuwa na unyanyapaa mkubwa na ukosefu wa ushirikiano katika ngazi za vijiji, mitaa na kata na hii husababishwa na pale mabaraza haya yanapotaka kutoa elimu na shauhuda  kwa umma na amewataka  wadau kuendelea kuutoa elimu kwa jamii  ili kuondoa unyanyapaa uliopo ngazi ya jamii. Wengi wamekuwa na mila potofu kufanya ngono isiyo salama lakini hii yote inasababishwa na inasababishwa na uduni wa elimu. Hivyo ni vyema jamii ikaendelea kupatiwa elimu zaidi ya unyanyapaa.
Miongoni mwa Maazimio ambayo wadau hao waliafikiana kuyatekeleza ni pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na vikao vya wadau mara kwa mara katika kubadilishana uzoefu juu ya changamoto wanazokabiliana nao, uimarishaji wa Kamati za UKIMWI za vijiji ili kuhakikisha zinafanya kazi na kufikia malengo ya kufikisha huduma kwa jamii, na kuhakikisha kuwa elimu ya mabadiliko ya tabia kwa jamii inaendelea kutolewa katika jamii zetu tunazoziudumia.
Licha ya kuwa Halmashauri ya Mji Njombe kuendelea kuongoza jitihada mbalimbali zimekua zikifanyika ikiwa ni pamoja na kuwaleta wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya UKIMWI kujadili changamoto ili kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanapungua na mwishowe kuisha.Wadau waliokutana katika mdahalo huo ni pamoja na TUNAJALI,JHPIEGO,PSI,SHISO,HIGLANDHOPE,JSI,NJODINGO,KONGA,COCODA,IMO,BAYLOR,URC,MDH,TAASISI ZA KIDINI NA VYOMBO VYA HABARI.
Imetolewa na,
Hyasinta Kissima
Afisa Habari-Njombe TC.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO