Ilikuwa Alhamisi, Oktoba 21, 1999
ILIKUWA Alhamisi, Oktoba 21, 1999, pale Uwanja wa Uhuru. Ilikuwa siku ya mwisho kabla mwili wa Mwalimu Nyerere kusafirishwa Butiama kwa maziko. Inakadiriwa watu takriban milioni 3 walihudhuria kuaga mwili wa Mwl. Nyerere kuanzia siku ya Jumanne (Okt. 19, 1999). Kuna mwandishi wa BBC alishangazwa na umati wa watu uliokuwapo, akatamka (bila kujua? Kwa mshangao; "This is the shock of the century for Tanzanians. Nyerere was so much loved by everyone,"
Tafsiri isiyo rasmi; “….huu ni mshituko wa karne kwa Watanzania. Nyerere alipendwa mno na kila mtu.”
Rais wa Kenya, Daniel arap Moi, alitamka: "He was one of the greatest sons of Africa. The passing of Mwalimu Nyerere represents the passing of an era in Africa... he was rightly called the conscience of Africa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani; Madeline Albright alitamka; “….there was no question that Mr Nyerere was one of the great leaders of our time. He had bequeathed Tanzania a proud tradition of unity and tradition.”
Wakati Rais Benjamin Mkapa anasoma hotuba yake; nilijisemea moyoni; huyu (Benjamin Mkapa) alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Rais Nyerere, leo anamuaga Mwl. Akiwa Rais wa nchi- kisa Mwl. Nyerere aling’atuka madarakani na kujenga msingi wa viongozi kukaa Ikulu miaka isiyozidi 10. Nikahitimisha (moyoni) Mkapa atakuwa anajivunia Mwl. Nyerere.
Nakumbuka pia namna Rais Sam Nujoma alivyokuwa akipiga hatua kukaribia ‘kidirisha’ cha jeneza chenye sura ya Mwl. Nyerere, ndani ya jeneza lililohifadhiwa katika kivuli cha kibanda maalumu. Sam Nujoma ndiye ambaye barabara ya Mwenge hadi Ubungo kupitia Mlimani City Dar imeitwa jina lake.
Huyu alipiga hatua zilizokuwa zikipishana kwa takriban sekunde mbili hivi. Niliwaza, kwa namna anavyotembea kwa kujivuta, anakumbuka namna Nyerere alivyosaidia kuikomboa Namibia, anakumbuka alivyotoroshwa na kufichwa Mbeya kuwakwepa wakandamizaji Namibia na kusaidiwa kupanga mikakati ya kurejea kwenye mapambano kule Windhoek.
Nujoma alitazama sura ya Mwl. Julius ndani ya jeneza, akaangusha chozi. Kati ya viongozi wa kimataifa zaidi ya 70 miongoni mwao marais wa Afrika 16, Rais Thambo Mbeki wa Afrika Kusini na Robert Mugabe wa Zimbabwe, ilifika zamu yao kusogelea jeneza kumuaga Mwl. Nyerere.
Mikono ya Robert Gabriel Mugabe, ilipiga ishara ya msalaba huku macho yake yakiangusha chozi, akiwa amesimama kumuaga Komredi wa kweli kwake.
Ilifika zamu ya Madeleine Albright, aliyefika msibani Tanzania akitokea Nigeria kikazi. Lakini wakati Albright akijongea kwenye jeneza, nilimwona Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Jakaya Kikwete, akitoa kitambaa cheupe mfukoni, akijifuta machozi huku wimbo wa … Tanzania … Tanzania…nakupenda kwa moyo wote ukipigwa.
Madeline naye alisogelea jeneza lenye mwili wa Mwl. Nyerere sikujua kama aliangusha chozi kwa sababu alivaa miwani yenye ‘vioo’ vyeusi tii kama rangi ya suti yake ya blauzi (koti) na sketi. Nilimwona tu akishika miwani yake kuashiria kuiweka sawa.
Watu walitokwa machozi. Ni machozi yaliyotiririka kutoka machoni mwa waislamu, wakristo, masikini na ombaomba, pamoja na wafanyabiashara wakubwa.
Kwa sababu machozi haya yalikuwa ni kimiminika chenye rangi inayofanana, yaliashiria jambo moja tu, kwamba; binadamu wote ni sawa, ujumbe ambao ulikuwa wa kipaumbele enzi za uhai wa Mwl. Nyerere. Buriani Julius.

By Dil's

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO