KUNA baadhi ya sinema ukizitazama ni lazima urejee tena na safari hii nimerejea tena kuangalia Stiletto.
Hii sinema ina utamu wake kwa kuwa ina mambo ambayo huwezi kuamini kwamba huwatokea binadamu.
Mambo hayo ambayo huwa ni sumu kali katika maisha yameoneshwa na kufuatiliwa sana katika sinema hii ambapo staa wake mkubwa ni Tom Berenger na mdada Raina (Stana Katic).
Ndani ya  filamu hii unaanza kwa kuona mauaji katika mkutano wa watu wawili katika sauna.
Mmoja wa hawa anapigwa kisu (stiletto kwa maana halisi)  anapona na kukimbizwa hospitalini na kuamka baadaye akisema kwamba aliyefanya mauaji hayo ni mpenzi wake.
Mpaka unapomaliza sinema hii unakuwa unahema kama wewe si mtu wa kupenda masikhara ya kuona damu au kuona ubamizaji usiokuwa wa kawaida na tabia za uwehu.
 Nini stori yake: Ukianza unaweza kabisa usijue hii ni stori ya aina gani lakini unapomuona Tom Berenger unajua moja kwa moja kwamba hii ni sinema ya gangstar.
Unajua hivi kwa kuwa muziki na aina ya mazungumzo yanagusia ujahili wa aina fulani wa magenge makubwa ya chini kwa chini, magenge ambayo yanashindana katika biashara huku yakiwa na ubabe wa juu kiasi cha kutishia hata mwenendo wa serikali.
Wakati Tom Berenger akicheza kama Virgil Vadalos  akizungumza na tajiri moja la Kigiriki kiongozi wa kundi la mafia anaingia na kumchinja huyu mwingine na kisu na anapojitokeza tunamuona kwamba ni msichana.
Vadalos akizubaa naye anajikuta  akichomwa kisu cha tumbo na mdada huyo huyo ambaye ama hakika alikuwa mpenzi wake.
Mdada Raina aliua na kuondoka lakini Vadalos anaponea tundu la sindano na hapa ndipo picha linapoanza.
Nasema ndipo picha linapoanza kwa kuwa wakati wa upelelezi wanajaribu kujua nani anafanya mauaji ya watu wa magenge,Vadalos anataka mshikaji wake wa zamani Raina atafutwe kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa anahusika na mauaji hayo.


Filamu hii iliyoongozwa na Nick Vallelonga ni moja ya filamu ambayo utapenda kuiangalia kwa kuwa uwongo wake na utamu kolea unakaribia na ukweli kwa wale wanaojua ukweli wa sinema.
Stiletto hii ya mwaka 2008  ambayo ni picha ya kimarekani pamoja na akina Stana na Tom Berenger wapo pia Michael Biehn, William Forsythe, na Tom Sizemore.
Filamu hii ambayo ilionwa kwa mara ya kwanza katika tamasha la sinema la kimataifa la  Newport Beach Aprili 28, 2008 na kuachiwa katika DVD Machi 3,2009 imetengenezwa katika mazingira ambayo raha yake ni kuona kuchachawa kwa Raina, aina yake ya mauaji na jinsi wanaume walivyo viumbe dhaifu.
Virgil  pamoja na kuagiza watu wake pamoja na askari mmoja mpenda rushwa wamsake mdada huyo ambaye aliwaarifu kuwa ni mpenzi wake wa zamani,  alikuwa anashangazwa na kasi ya mauaji ya Raina na sababu zake.
Hakuwa anaua katika kundi lake tu bali aliwachanganya .
Hapakuwepo na maelezo wala akili kwamba kwa nini Raina anaua hovyo kwenye makundi yanayopingana. Pamoja na mambo kuonekana ya hovyo Virgil anajikuta akihamanika kutokana na kupotea kwa dola za Marekani milioni 2.
Wasaidizi wakubwa wawili wa Virgil Lee (Biehn) na  Alex (Forsythe) wanajikuta wanatiliana shaka kuhusu kupotea kwa fedha hizo.
Mauaji ya Raina, baadaye unayagundua kwamba yalikuwa ni kuwashughulikia watu waliomfanyia ndivyo sivyo katika maisha yake.
Anawasaka watu hawa, anaonesha urafiki wa kurudiana na kisha anawaua katika furaha zao. Watu hawa walikuwa wakitoka katika makundi mbalimbali na hivyo kusababisha taharuki kubwa ndani ya makundi hayo wakishindwa kuelewa nani anawapa  wakati mgumu.


Kiukweli wakati anaua mmoja baada ya mwingine mchakato wake wa kwenda kumalizia kazi yaani ya kumuua Virgil ulikuwa unazidi kujisogeza.
Filamu hii unatakiwa kuiangalia vizuri sana kwani  njia nzima utafanyiwa kujua kwamba Raina anafanya vile kwa watu ambao wamemdisi lakini baadaye unaweza kuoanisha mawazo yako na kisasi.
Katika vurugu za kulipiza kisasi cha kuuawa kwa dada yake anagundua  kitu kibaya na ambacho kinamfanya ajiulize kwa nini alikuwa na imani kubwa na shughuli zake alizokuwa akizifanya na kuzitekeleza.
Raina (Stana Katic) kiukweli  alikuwa anampenda sana Virgil Vadalos (Berenger) hadi pale alipogundua kwamba yeye ndiye aliyehusika na kupotea kwa dada yake.
Kuanzia hapo akaamua basi, na kuapa kwamba atawaondoa Virgil na kundi lake  lote.
Akiwa hana kingine zaidi ya kisu na hasira, ndipo Raina anapoingia katika bafu na kufanya mambo yale, kisha taratibu akaingia katika ngazi za juu  za magenge hayo huku akipanda kwa kasi katika namna anavyoua akitumia kisu.
Virgil alijua kwamba si rahisi sana kumkomesha muuaji ambaye anafanya vitu vyake kwa akili akiwa amejiamini sana ndipo alipompa kazi polisi mmoja mpuuzi anayependa vijisenti na kumpa kazi ya kumsaka Raina kwa udi na uvumba.
Polisi huyu Beck ( nafasi iliyochezwa na Paul Sloan) anatakiwa kumsimamisha Raina ambaye alionekana kuwa tishio kubwa na katika saka nikusake ndani ya Los Angeles, Raina na Beck  wanagundua kitu kingine kwamba huwezi kukwepa rushwa inayofanya akili za watu zisiwe sawasawa.


Filamu hii kama utaipata mimi niliiona katika You Tube baada ya muda mrefu ni mbaya kwa maana ina mtetemo wa mauaji usiopendeza, dawa za kulevya na maeneo yasiyotamkika lakini shua ni aksheni kwa kwenda mbele ni advencha na kubwa zaidi inasisimua na inakuacha  ukishindwa kuamua mpaka mwisho wa safari.
Wiki hii kuna mtu anataka nimpe taarifa ya sinema gani ina ukweli wa kutosha kuhusu uvamizi wa Entebe uliofanywa na Waisrael. Nikuhakikishe ndugu yangu naingia katika genge langu la kuchakura na nitakuja kukupa kitu.
Ukitaka zaidi unaweza kunisaka katika ujumbe mfupi 0713176669 au ndani ya msimbebeda @gmail.com

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO