TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz


Oktoba 01, 2016


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, Oktoba 1, 2016
                                           
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na watu wote duniani katika kuadhimisha siku ya wazee duniani. Wakati dunia inaadhimisha siku hii, Tume inatoa wito kwa jamii yote ya Watanzania kuondoa vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi ya wazee ili kuhakikisha kuwa wanaishi katika jamii salama kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia na kauli mbiu ya taifa inayosema “Ondoa Unyanyasaji kwa Wazee”.

Uzee na kuzeeka, havikwepeki; hivyo ustaarabu wa jamii au nchi yoyote duniani si wingi wa rasilimali na mazingira mazuri bali katika uwekaji wa mifumo madhubuti ya kulinda na kutetea haki za makundi maalumu yanayohitaji ulinzi wa jamii husika. Kwa kulitambua hilo Disemba 14, 1990, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Azimio lake Na. 45/106 uliipitisha tarehe 1, Oktoba ya kila mwaka kuwa Siku ya Wazee Duniani. Vipaumbele katika Azimio hilo ni pamoja na suala la uhuru wa wazee, wazee kushiriki na kushirikishwa katika shughuli za maendeleo, kutunzwa na kuheshimiwa.

Hivyo siku hii ya tarehe 1, Oktoba dunia inawapa nafasi wazee kukutana pamoja na kubadilishana mawazo juu ya nini cha kufanya kuhusiana na mustakabali wa haki zao kwa ujumla, zikiwemo haki za kupata huduma za matibabu na mafao yao kwa wakati.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake Ibara ya 12(2) na ibara ya 14 imeeleza juu ya wazee kupewa heshima na kupata hifadhi kutoka katika jamii wanamoishi.
Aidha, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ilionesha kuwa idadi ya watanzania wote ni milioni 45; kati yao idadi ya wazee kwa Tanzania Bara ni 2,507,568 (5.6%) - wanaume 1,200,210 (5.5%) na wanawake ni 1,307,358 (5.7%). Tanzania visiwani ina jumla ya wazee 58,311 (4.5%) - wanaume 29,887 (4.7%) na wanawake 28,424 (4.2%). 

Kundi hili la wazee ni kubwa na linahitaji ulinzi na utetezi maalumu wa haki zao kwa kuwa lina wanyonge wengi kulingana na umri wao, hali duni za kiuchumi,  matatizo ya kiafya na kisaikolojia.

Tume kama taasisi ya kitaifa iliyo kitovu cha ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu nchini, imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa wazee wanapewa haki zao. Jitihada hizo ni pamoja na:-
 • Kutoa elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora, ikiwemo haki za wazee kwa viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali wa taasisi za Serikali na Asasi za Kiraia, na wadau mbalimbali wa haki za binadamu. Kazi hii imefanyika kupitia Mpango-kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu (National Human Rights Ation Plan) uliozinduliwa rasmi mwaka 2013.

 • Kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutunga Sheria ya Wazee nchini kwa kutoa maoni yatakayohakikisha kuwa haki za wazee zinalindwa na kuhifadhiwa.

 • Kushughulikia malalamiko yanayohusiana na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, hasa katika suala la mapunjo na wastaafu kutolipwa pensheni zao stahiki na kwa wakati.

Tume inatambua na kupongeza jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kujali ustawi wa wazee nchini. Jitihada hizo ni pamoja na kuundwa kwa Sera ya Wazee ya mwaka 2003, kuundwa kwa taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya Wazee, kama vile Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wanawake, Jinsia na Wazee, na jitihada za kupunguza umaskini kwa kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF).
.
Pamoja na jitihada hizi bado wazee wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo:-
 • Kutofaidika na mafao mbalimbali ya mifuko ya hifadhi ya jamii (pensheni jamii) licha ya kwamba maendeleo yaliyofikiwa na nchi yetu leo hii ni matokeo ya mchango wa wazee hao kwa kazi zao mbalimbali walizofanya.

 • Kutopata huduma muafaka za afya na matibabu bure licha ya matamko mbalimbali ya viongozi wa Serikali ya kuwapatia matibabu bure na huduma bora za afya kwa wakati muafaka; jambo lililoendelea  kuwa wimbo usio na kibwagizo kwa muda mrefu sasa. Wazee wananyanyasika hasa kwa magonjwa kwa kutopatiwa matibabu sahihi.

 • Kutokuwepo kwa sheria maalum inayoshughulikia masuala mbalimbali ya wazee;

 • Umaskini wa kipato miongoni mwa wazee wengi.

 • Kutokuwa na uwakilishi katika vyombo na ngazi mbalimbali za maamuzi ili kuwapo na utetezi wa haki zao.

 • Usalama mdogo kwa wazee kutokana na ukatili na manyanyaso wanayofanyiwa, hasa vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na walemavu na mauaji ya wazee kutokana na imani potofu.

Kwa mujibu wa taarifa za utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Help Age International (HAI) Tanzania siyo mahali salama kwa wazee kuishi; kwani kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 jumla ya wazee 2,866 waliuawa kwa imani za kishirikina katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara, ikiwa ni wastani wa mauaji ya wazee 573 kila mwaka.

Kutokana na changamoto hizo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inatoa mapendekezo yafuatayo kwa Serikali, jamii na wadau katika uimarishaji wa upatikanaji wa haki za wazee nchini:-
 1. Elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora itolewe kwa wananchi wote ili kujenga jamii inayoheshimu na kulinda haki za binadmu.

 1. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikamilishe utungaji wa Sheria ya Wazee kwani kupatikana kwa sheria hiyo kutawezesha utekelezaji wa Sera ya Wazee ya mwaka 2003.

 1. Utaratibu wa malipo ya pensheni/hifadhi ya jamii kwa wazee wote bila kujali hadhi zao, yaani bila kuangalia iwapo walikuwa wafanyakazi katika sekta rasmi au siyo rasmi, uwekwe na uharakishwe kutekelezwa.

 1. Huduma za afya ziboreshwe na kutolewa bure kwa wazee, hii ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa huduma maalum za afya, madawa ya kutosha na vyumba maalum kwa ajili ya wazee.

 1. Kwa kupitia mradi wa TASAF wa kunusuru kaya masikini Serikali itoe kipaumbele kwa wazee ili kuwanusuru wazee wote nchini. Kupitia mradi huu itakuwa rahisi kuwafikia wazee walioko vijijini kwa kuwa mradi umeweza kuwakwamua kiuchumi watu wanaoishi katika mazingira magumu.

 1. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatoa wito kwa jamiii kuwatambua wazee kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa. Aidha, inawataka wadau wa haki za binadamu kuhamasisha wananchi nchini kote kulinda, kukuza na kutetea haki na ustawi wa wazee nchini ili kuondoa unyanyasaji dhidi yao.

 1. Serikali iweke mikakati endelevu ya kukomesha na kutokomeza mauaji ya wazee yanayochangiwa na imani za kishirikina. Mauaji haya yanavunja haki za binadamu, na yanaitia doa na kuiaibisha nchi yetu.

 1. Pia Serikali kwa kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama iongeze jitihada za kuwasaka na kuwakamata wahusika wa mauaji ya wazee. Aidha, vyombo hivyo viharakishe upelelezi na uendeshaji wa kesi za mauaji ya wazee ili haki ionekane kuwa inatendeka.

 1. Mwisho, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatoa wito kwa jamii kuwathamini wazee, kwani ni kundi muhimu linalohitaji upendo, kuthaminiwa na kusaidiwa.

Wazee ni hazina ya taifa tusiwanyanyase!

Imetolewa na:

(SIGNED)

Salma Ali Hassan (Kamishna)

Kny. Mwenyekiti
                                                 
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Oktoba 1, 2016

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO