TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa washiriki wa  Kongamano la Pili la Biashara kati ya Tanzania na Comoro kutumia taarifa na masuala yatakayojadiliwa katika Kongamano hilo kujenga mtandao wa ushirikiano utakaorahisisha uendeshaji wa shughuli zao kwa ufanisi.

Akizungumza katika Kongamano hilo la siku moja ambalo linafanyika katika hoteli ya kitalii ya Sea Cliff iliyoko Kaskazini Mashariki ya Kisiwa cha Unguja leo, Dk. Shein amewataka pia wafanyabiashara na wawekezaji wa Zanzibar kutumia fursa zilizoko Tanzania Bara na Comoro ili kuimarisha biashara na uwekezaji.

Dk. Shein amesema Kongamano hilo ambalo linajumuisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Comoro lina nafasi ya pekee kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi mbili hizo kwa kuwa linachangia kuibua fursa na maeneo mapya ya uhusiano na ushirikiano.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein aliahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inaweka mazingira mazuri yatakayowezesha makubaliano kati ya Jumuiya za wafanyabiashara wa Zanzibar na Comoro yaliyofikiwa mwezi Juni mwaka jana yanatekelezwa kwa mujibu wa malengo ya jumuiya hizo.

Dk. Shein alibainisha kuwa mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Comoro yamedumu kwa karne nyingi na kwamba hatua zinazochukuliwa na jumuiya za wafanyabiashara wa nchi hizo hivi sasa ni kurejesha historia hiyo kubwa ya biashara kati ya nchi zetu.

Kwa hivyo alisema kuwa kongamano hilo ambalo limetayarishwa kwa pamoja na jumuiya za wafanyabiashara za Tanzania Bara, Zanzibar na Comoro ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo.

Dk. Shein aliongeza kuwa uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Comoro ni wa kihistoria ambao umejengwa kwa misingi ya udugu na urafiki uliodumu kwa karne nyingi.
“Kama ulivyo uhusiano wa watu wa Zanzibar na watu Tanzania Bara ndivyo ulivyo uhusiano kati ya watu wa Zanzibar na Comoro hivyo sisi ni watu wamoja wenye historia moja na utamaduni unaofanana” Dk. Shein aliwaeleza washiriki wa Kongamano hilo.
Aliwaambia washiriki wa Kongamano hilo kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimekuwa zikiimarisha huduma za usafiri wa majini na anga hatua ambayo itazidi kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Comoro.
Kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo, Dk. Shein aliwaeleza washiriki hao kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinatambua na zinathamini sana mchango wa sekta binafsi katika kujenga nchi.

Alibainisha kuwa kwa upande wa Zanzibar, Serikali imepitisha sheria ya ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma lengo lake likiwa ni kuleta uwiano wa sekta hizo katika kuleta maendeleo.

Akizungumza kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Augustine Mahiga alieleza kuwa ukaribu wa kijiografia pamoja na udugu wa watu wa Tanzania na Comoro unaupa nguvu uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo.

Alifafanua kuwa katika kuangalia uhusiano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Comoro, Zanzibar ndio kioo cha jitihada za Tanzania kukuza uhusiano huo.

“Mahusiano ya kibiashara na uchumi lazima yanajengwa katika msingi imara wa uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia na kwetu sisi historia ya uhusiano wetu na Comoro iwe dira ya uhusiano huo” Balozi Mahiga alilieleza Kongamano hilo.
Kwa upande wake Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar Balozi Amina Salum Ali alisema kuwa lengo la Kongamano hilo ni kutengeneza mazingira mazuri yatakayowezesha wafanyabiashara wa Tanzania na Comoro kukuza biashara na uwekezaji katika nchi hizo.
Alifafanua kuwa katika Kongamano hilo Comoro imewakilishwa na ujumbe mzito wa watu 25 wakijumuisha Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mheshimiwa Mohamed Bacar Dossar pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali hiyo na viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa nchi hiyo.
Balozi Amna alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadhamini wa Kongamano hilo kwa kufanikisha maandalizi yake kwa mafanikio makubwa

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO