WATU takribani 56 wamekufa na wengine 108 wamejeruhiwa baada ya lori la mafuta kulipuka mashariki ya Msumbiji.
Taarifa za awali zilisema kwamba watu 73 wamekufa kutokana na moto huo.
Imeelezwa kuwa mlipuko huo ulitokea Alhamisi wiki hii katika kijiji cha Caphirizanje jimbo la  Tete mpakani na Malawi.
Sababu za mlipuko huo bado kujulikana.
Kuna taarifa zinazogongana kuhusiana na sababu ya tukio hilo. Wakati wengine wakisema kwamba dereva alikuwa akiuza mafuta wakati  gari lilipolipuka wengine wamesema kwamba dereva alikuwa ametekwa.
Hata hivyo imeelezwa kuwa mlipuko huo huenda umesababishwa na radi au moto  uliozuka karibu na lori hilo.
Imeelezwa kuwa serikali itawapatia majeneza watu ambao wametambulika, na wale ambao hawakutambulika watazikwa katika kaburi moja.
Taarifa zaidi zinasema kwamba takwimu zimekuwa ndogo kwa sababu idadi ilizingatia maiti waolioweza kupatikana.
Imeelezwa kuwa baadhi ya watu walioungua vibaya ni wale waliokuwa wakikimbilia  kwenye mto.
Aidha taarifa nyingine zinasema kwamba lori hilo lilipata ajali Jumatano mchana na  ilipofika Alhamisi wanakijiji walikuwa wakijaribu kuiba mafuta wakati lilipolipuka.
Serikali imesema kwamba imesikitishwa na maisha ya watu kupotea na kwamba inafanya kila juhudi kusaidia waathirika wa mlipuko huo.
Mawaziri watatu wa Msumbiji wamewasili katika eneo la tukio kusimamia kazi ya uokoaji na kuongoza mahojiano kujua ukweli wa yaliyojiri.
Pamoja na mawaziri hao watatu kufika eneo la tukio Rais wa taifa hilo  Filipe Nyusi aliitisha kikao cha Baraza la Mawaziri na kutangaza siku tatu za maombolezo.
Katika siku za karibuni Serikali ya Msumbiji iliongeza bei ya mafuta kutokana na kuanguka kwa thamani ya fedha ya nchi hiyo dhidi ya dola ya Marekani.
Msumbiji ni moja ya mataifa masikini kabisa duniani ikiwa na wananchi milioni 24 wakiishi chini ya mstari wa umasikini.
Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1975 kutoka Ureno lakini bado inakabiliwa na athari za vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa miaka 16 na kumalizika mwaka 1992.
MWISHO

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO