waziri Mkuu, spika wa bunge na kiongozi wa upinzani bungeni wakishuhudia safari ya mwisho ya mbunge wa Dimani na mwamuzi wa kimataifa hafidh Ally

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo asubuhi ameongoza wabunge kumuaga Mbunge wa Jimbo la Dimani kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM) Hafidh Ally Tahir aliyefariki usiku wa kuamkia leo mjini hapa.
Tahir alifariki majira ya saa 9 usiku katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa shinikizo la damu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dk James Kiologwe alisema Tahir alifika hospitalini hapo akiwa na gari yake huku akilalamika sehemu za kifuani kubana na kufariki akipatiwa matibabu.

Mwili wa Tahiri ambaye pia alikuwa Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania  ulisafirishwa asubuhi saa 11.45,kwa ndege kwenda Zanzibar .
Huzuni kubwa ilitanda miongoni mwa Wabunge kwa kutambua kwamba alikuwa  mmoja wa watu waliosaidia michezo katika Bunge hilo na Tanzania kwa ujumla.
Uwanjani hapo mbali na Majaliwa pia alikuwepo Spika wa Bunge Job Ndugai na kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe.
Akizungumza jana katika uwanja huo,Kocha wa timu ya Bunge Sports Club, Venance Mwamoto alisema marehemu alikuwa ni mtu muhimu kutokana na kuwa kiunganishi katika timu ya bunge na michezo kwa ujumla.
Alisema amejuana na Tahir wakati akiichezea timu ya Majimaji kutokana na kuchezesha michezo mingi ya Ligi daraja la kwanza wakati huo.
‘’Nimehuzunika sana kumpoteza mtu wa michezo alikuwa mwamuzi  ambaye alikuwa akisimamia haki na pia tulisoma nae wote mafunzo ya juu ya ukocha Zanzibar kabla ya mimi kwenda Ujerumani hapa katika timu ya bunge mimi kocha mkuu yeye ni msaidizi wangu’’alisema
Naye Mwenyekiti wa timu ya Bunge Sport Club,Wiliam Ngeleja alisema hadi saa tatu usiku wa jana walikuwa na marehemu wakipanga mipango ya kushiriki katika mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki wakijadili ushiriki wa timu hiyo.
Alisema wakati wakiwa katika vikao hivyo hakuonesha dalili za kudhoofika kiafya na walikuwa wakicheka  pamoja na kujadiliana jinsi ya kuhakikisha timu hiyo inachukua ubingwa katika mashindano hayo.
Tahir  alizaliwa Oktoba 30 mwaka 1953 huko Dimani Zanzibar na Elimu ya Msingi amesoma  shule ya Kombeni mwaka 1957-1966  na Sekondari akisoma katika shule hiyo hiyo.
Mara baada ya kumaliza masomo yake Yugoslavia kwa masomo ya juu na baadae Misri.
Hafidh  amefanya kazi kwa muda mrefu katika redio ya Zanzibar (ZBC).
Pia katika uhai wake amechezesha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika(AFCON) mara 9 pamoja na mashindano ya Dunia kwa Vijana under 17.
Vilevile ni mwamuzi ambaye alikuwa akichezesha michezo mikubwa  Tanzania na barani Afrika mfano wa mechi hizo ni Zamaleck na Al Ahly za Misri.
Source: Sifa Lubasi, DodomaPost a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO