MFUMO wa utoaji haki unaoshirikisha vyombo vya dola umedaiwa kuwa na mapungufu mengi kiasi cha kufanya watuhumiwa wengi wa ukatili wa kijinsia kutodhibitiwa ipasavyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Lisilokuwa la Kiserikali linalofanya kazi na jamii kwa mabadiliko Chanya (AFNET), Sarah Mwaga wakati akieleza kuhusu maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yaliyoanza jana.
Alisema mapungufu hayo ni pamoja na kukosekana kwa vituo vya polisi na madawati ya jindia kwenye maeneo mengi hasa ya vijijini kunakotokea matukio mengi  ya ukatili.
“Watekelezaji wengine wa sheria vijijini wakiwemo maofisa watendaji wa vijiji na kata kujichukulia madaraka na kuamua kesi ambazo kisheria zinatakiwa kwenda mahakamani kama kesi za ubakaji na makosa mengine ya jinai” alisema.
Pia alisema kuna urasimu katika mfumo mzima wa utekelezaji wa sheria na ugumu katika kuthibitisha makosa kunakofanya watuhumiwa kuachiwa huru hata kama wana makosa.
Aidha kukosekana kwa huduma rafiki kwa watu wanyonge na rushwa kwa baadhi ya maofisa.
Aidha alisema kwamba jamii inatakiwa kuangalia kwa umakini biashara ya watu kwani katika mazingira ya sasa biashara hii inafumbiw amacho kutokana na ugumu wa ufuatiliaji na pia sheria zinazoweza kubana wanaohusika na biashara hiyo.
Biashara ya watu mara nyingi inawakutanisha wasichana wadogo na wavulana na aina mpya ya utumwa, utumishi katika sekta ya ngono.
Akitolea mfano wa manispaa ya Dodoma, Mwanga alisema kuna aina mpya ya ukahaba ambapo baadhi ya wasichana wamekuwa wakipeleka picha kwenye mahoteli makubwa ili watafutiwe wateja wa kuwaliwaza.
Bila kutaja hoteli au nyumba za wageni zinaozhusika na biashara hiyo ambayo inaanza kushamiri alisema tabia hiyo imekuwa ikifanya wasichana wengi kujiuza kwa staili ya aina yake na kwa kuwa ni kinyume cha sheria madhira wanayokutana nayo hawana pa kuyapeleka.
“Baadhi ya hoteli wasichana wamekuwa wakipeleka picha na namba za simu kwa mameneja wa hoteli ili akitokea mteja aweze kuitwa” alisema
Alisema kwa kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni funguka, pinga ukatili wa kijinsia, elimu salama kwa wote ni vyema mifumo ya haki ikaangaliwa upya na pia jamii ikajikita kuonesha madhara ya matendo mbalimbali ya biashara ya biandamu ambayo mara nyingi inayishia katika ukatili wa kijinsia.
“Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha wadau mbalimbali na wanajamii kutonyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia na badala yake wafunguke na kuvisemea kwa lengo la ama kuzuia visitokee, ama kudai haki itendeke pale vinapotokea” alisema.
Pia Mwaga alisema mazingira ya utoaji elimu kwa watoto si salama na ni hatarishi kuanzia nyumbani, njiani mitaani na hata shuleni.
“Tunapata kesi nyingi za watoto wa kike na kiume kubakwa na kulawitiwa na wazazi wao, ndugu wa karibu na hata viongozi wao wa kimila tena wengine katika umri mdogo sana” alisema
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Ernest Kimola alisema ukatili wa aina yoyote ni kinyume na haki za binadamu na ni makosa ya jinai.
Mwenyekiti wa kamati ya maadhimisho hayo, Profesa Adam Mwakalobo wa Chuo kikuu cha Dodoma (Udom) alisema watahakikisha wananchi wa Dodoma wanapata elimu ya kutosha kuhusiana na vitendo vya ukatili.
Source: Sifa Lubasi, Dodoma


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO