Mkuu wa Chuo cha Ufundi VETA,  injinia Lucius mwishoni akizungumza na baadhi ya walimu na wanafunzi  wa VETA kuhusu mfumo wa masomo kwa njia ya simu za mkononi wa VSOMO mwishoni mwa wiki. 

VIJANA  zaidi ya elfu 28 wamejiunga na masomo ya ufundi stadi yanayotolewa na VETA kwa njia ya simu za mkononi kwa mfumo ujulikanao kama VSOMO.

Mfumo huo unawezeshwa na kampuni ya simu ya Airtel.

Idadi ya wanafunzi hao ni wale ambao wameanza kusoma toka mfumo huo uzinduliwe Mei mwaka huu.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa hafla fupi ya kueleza mafanikio ya mfumo wa VSOMO iliyofanyika katika Ukumbi wa VETA kipawa, Mkuu wa Chuo cha Ufundi VETA, Lucius Luteganya alisema mfumo huo umeonesha mafanikio makubwa na sasa wanatarajia kuongeza kozi kufikia 10 ili kutanua zaidi fursa hiyo ya VSOMO.

 “Airtel na VETA baada ya kuanzisha wa VSOMO yaani masomo kwa njia ya simu za mkononi na kuipeleka taarifa katika vituo vya VETA vilivyopo katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Dar es salaam, Arusha na Mbeya, leo hii zaidi ya vijana  28 elfu  wameshajiunga na mtandao wa VSOMO ili kuanza kusoma, hii inaonyesha kuwa mfumo huu wa kusoma kwa njia ya simu umekubalika na pia kunauhitaji mkubwa wa vijana kutaka kusoma VETA”

Aidha Lutejanya alisema kuwa kozi zilizopo sasa ni za umeme wa nyumbani, kuchomelea, ufundi wa pikipiki, masuala ya urembo, kutengeneza aluminum, pamoja na ufundi simu.
 “Kwa vijana wote ambao tayari wameshapakua aplikesheni ya VSOMO katika simu zenu sasa hivi wanaweza kuchagua kozi na kuanza kusoma papo hapo popote walipo mara tu baada ya kulipia,” aliongeza.

Alisema baada ya kuona kuna ongezeko la vijana kujisajili na huduma hii ya VSOMO tayari wamewasiliana na baadhi ya vijana kwa kushirikiana na mdhamini wa mradi huu Airtel ili kubaini kozi wanazotaka.

Kutokana na mawasiliano hayo katika miezi miwili ijayo watapandisha kozi zingine 10 kwenye mfumo wa VSOMO ili vijana wote waliojiandikisha waweze kuchagua kozi wanazotaka..

Mradi wa VSOMO uko chini ya mradi wa kijamii wa Airtel FURSA ukiwa na lengo la kuwasaidia vijana kuweza kujisomea kozi za ufundi  stadi ili kujipatia ajira za uhakika.  Mradi wa VSOMO ulibuniwa kwa ushirikiano kati Airtel na Mamlaka ya elimu na mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)  hivyo kufanya simu ya mkononi kuwa Darasa.


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO