Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Waziri wa Biashara na maendeleo wa Finland, Kai Mykkanen wakatizama moja ya mitambo ya umeme  katika Kituo cha TANESCO cha Mikocheni kabala ya kuzindua  Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Umeme jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam watumie fursa ya uwepo wa umeme wa uhakika kwa kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili waweze kujiongzea kipato. 
Ametoa wito huo leo (Jumatano, Novemba 16, 2016) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa uboreshaji miundombinu ya umeme jijini Dar es Salaam uliofanyika kwenye Ofisi za TANESCO zilizoko Mikocheni jijini humo. 
Akizungumza kabla ya kubonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema: “Umeme ni mhimili mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi yoyote ile. Tumepata umeme wa uhakika, tumieni fursa hii ya uwepo wa umeme wa uhakika kujiongezea kipato.” 
“Hivi sasa tumepata umeme wa uhakika, fanyeni kazi kwa bidii ili mfaidi matunda ya kuwepo kwa umeme huo. Serikali inategemea kwamba sasa wananchi mtaanzisha na kukuza viwanda vidogo vidogo na vikubwa, biashara zitapanuka na kilimo bora huko vijijini kitaongezeka,” amesema.  
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda na moja ya nyenzo kuu ya kuendesha uchumi wa viwanda kwa tija na ufanisi ni upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika, na ndiyo maana kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha miundombinu ya  umeme inaboreshwa ili kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme. 
“Wataalam wamenieleza kuwa mradi huu ulihusisha ujenzi wa kituo kikubwa cha kupozea umeme cha MVA 100, ujenzi wa njia za usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 132 katika maeneo mbalimbali ya Jiji kupitia chini ya ardhi, ujenzi wa njia za usambazaji umeme wa msongo wa kilovoti 33, pamoja na ujenzi wa ujenzi kituo cha udhibiti mifumo ya usambazaji umeme (Distribution SCADA System) katika msongo wa kilovoti 33 na 11.” 
“Kukamilika kwa mradi huu kunaondoa adha zilizokuwepo awali kutokana na kukatika umeme mara kwa mara. Jiji la Dar es Salaam ni kitovu cha shughuli za biashara katika kuleta maendeleo ya Taifa ambapo upatikanaji wa umeme wa uhakika ni wa lazima,” ameongeza. 
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amesema Wakala wa Jiolojia Tanzania kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia wa Finland wanaunda mpango wa pamoja wa kuibua madini ya kisasa ambayo yanatafutwa zaidi duniani kukidhi mahitaji ya kiteknolojia.  
“Hivi sasa madini kama graphite na lithium yanahitajika zaidi kwenye teknolojia za kisasa kama za utengenezaji wa simu, tuachane na madini yaliyozoeleka kama vile dhahabu na Tanzanite,” alisisitiza. 
Alitumia fursa kuuagiza uongozi wa TANESCO uhakikishe kuwa hakuna mgao wa umeme nchi nzima kwani Watanzania wamechoshwa na tabia ya kukatiwa umeme mara kwa mara. “Ili tujenge nchi ya viwanda, tunahitaji umeme wa uhakika, umeme unaotabirika na zaidi ya yote umeme wa bei nafuu,” alisema huku akishangiliwa. 
Naye Waziri wa Biashara za Nje na Maendeleo wa Finland, Bw. Kai Mykkanen alisema Serikali yake imedhamini ujenzi wa mradi huo kwa vile inaamini kuwa umeme wa uhakika ni suluhisho la kuondoa umaskini kwa hiyo kukamilika kwa mradi huo kutaondoa adha ya kukatika umeme kila mara. 
Aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika eneo la nishati ya umeme na nishati mbadala. 
Katika hatua nyingine,  Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Eng. Felchesmi Mramba alisema ujenzi wa mradi huo umegahirimu sh. bilioni 74.6 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni 63.56 zimetolewa na Serikali ya Finland na sh. bilioni 11.03 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.  
Alisema kukamilika kwa mradi huo kumewezesha sehemu kubwa ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na njia za mzunguko (ring circuit) zinaoingizaa umeme. “Teknolojia hii iliyotumika itawezesha vituo vya kupozea umeme kuwa na njia mbadala ya kupata umeme endapo njia mojawapo inayopeleka umeme itapata hitilafu,” alisema. 
Naye Meneja wa Kituo cha Kudhibiti Mifumo ya Usambazaji, Eng. Alex Kalanje alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kompyta, (distribution SCADA SYSTEM) kituo hicho cha udhibiti wa mifumo ya usambazaji umeme katika jiji la Dar es Salaam kitawasaidia watoa huduma wao waweze kufuatilia kwa haraka zaidi pale matatizo yanapotokea. 
“Baada ya kukamilika kwa kituo hiki, lengo letu ni kujenga kituo kama hiki kwenye mjai ya Arusha, Mbeya, Dodoma na Mwanza,” alisema.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATANO, NOVEMBA 16, 2016.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO