WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo aliongoza mamia ya waombolezaji
kumuaga baba wa waziri mkuu mstaafu mizengo Pinda,Xavery Mizengo Pinda
huku Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete akumuelezea marehemu
kuwa alikuwa ni mtu mkarimu na Mcha Mungu.
Shughuli za kuaga mwili wa marehemu zilifanyika nyumbani kwa Waziri
Mkuu mstaafu Pinda kwenye Kijiji cha Zuzu na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwemo mawaziri, Manaibu Mawaziri, wabunge, viongozi wa
chama na serikali, viongozi wa dini na wananchi.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali itaratibu shughuli zote na
itaakilishwa kwenye mazishi na Naibu Waziri wa Maji ambaye pia ni
Mbunge wa Mlele, Isack Kamwelwe.
“Niliwahi kufika hospitalini kumuangalia kwa kweli hali yake haikuwa
nzuri, tumuombee apumzike kwa amani” alisema
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alisema wakati akiwa Rais alifanya ziara
mkoa wa Rukwa na alipita kijiji cha Kibaoni kumsalimia mzee huyo.
“Alikuwa ni mtu mwema sana na mwenye upendo mkubwa alikuwa akitambua
ugumu wa kazi za uongozi wa taifa alituombea sana alisema uongozi ni
kuvumilia na kupokezana kijiti” alisema
Alisema Pinda alimpa taarifa za kifo cha baba yake mzazi na kufika ili
kumuaga marehemu.Kwa upande wake Waziri Mkuu Pinda akizungumza alisema
kuondokewa na baba si jambo rahisi lakini anamshukuru Mungu kwa kila
jambo.
“Siku za mwisho za uhai wake zilikuwa nzuri lakini mimi nilijua
haiwezekani tena” alisema
Akiongoza ibada nyumbani hapo Padri Chesco Msaga wa kanisa katoliki
alisema kila mwanadamu anatakiwa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.
Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Alex Malasusa alisema marehemu alitumia uhai wake vizuri na
aliyoayaacha yaendelee kuokoa walio wengi.
Diwani wa kata ya Zuzu, Abdallah Awadhi alisema wananchi wametoa
ng’ombe moja, mbuzi wanne, kilo 200 za mchele na Sh 269,000.
Kwa mujibu wa wasifu wa marehemu uliotolewa kabla ya kuagwa kwa mwili
wa marehemu, alizaliwa mwaka 1926 akiwa mtoto pekee wa Mizengo Pinda
na alikuwa hajapata bahati ya kumuona baba yake kwani alifariki wakati
mama yake akiwa mjamzito.
Alilelewa na binamu yake na kubatizwa mwaka 1937, alipata kipaimara
mwaka 1940 na Desemba 11, 1944 alifuga ndoa na kubahatika kupata
watoto tisa.
Mzaliwa wake wa kwanza Mizengo Pinda alizaliwa Mwaka 1948.
Marehemu ameacha wajukuu 54  vitukuu 40 na sehemu kubwa ya maisha yake
alitumikia kama mwalimu wa dini (katekista) kazi aliyoianza mwaka 1951
na kustaafu mwaka 1972 na kuwa mzee wa kanisa huku akiendesha shughuli
za kilimo.
Mwanzoni mwa mwaka 2013 alianza kusumbuliwa na nyonga kutokana na
kuanguka usiku na alipatiwa matibabu katika hospitali ya taifa ya
Muhimbili na kuwekewa chuma kwenye mfupa wa nyonga.
Baadae alifika Dodoma kwa mtoto wake ambapo aliishi miaka mitatu na
Novemba 21, mwaka huu hali yake ilibadilika na kulazimika kupelekwa
hospitali ya mkoa wa Dodoma  ambapo alifariki Novemba 27.
Mwili wa marehemu umesafirishwa kwa ndege ambapo mazishi yatafanyika
kesho kijiji cha Kibaoni Wilaya ya Mlele.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO