Vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini watafaidika na mafunzo yatakayotolewa na kampuni ya Empower kutoka Korea yatakayohusu utengenezaji vifaa Umeme Jua ambavyo vinatumika kuwasha taa na kuchaji simu huku gharama yake ikiwa ni nafuu.
Hayo yamebainika jijini Dar es Salaam
wakati wa kikao baina ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
Balozi wa Korea nchini, Song
Geum-Young na watendaji wa
kampuni ya Empower, inayotengeza vifaa hivyo.
Watendaji wa kampuni hiyo walifika na baadhi ya vifaa hivyo vya Umeme
Jua ili kuionesha Wizara namna vinavyofanya kazi.
Dkt. Hong Kyu Choi, kutoka kampuni ya
Empower alisema kuwa wamepanga kutoa mafunzo hayo sehemu mbalimbali nchini ili
vijana hao waweze kujiajiri na pia kuwezesha wananchi hasa wa vijijini kupata
huduma ya umeme.
Alisema kuwa mafunzo hayo pia yatatolewa
kwa walimu wa Sayansi nchini ili nao waweze kuwafundisha wanafunzi kuhusu
teknolojia na hivyo kuwa endelevu.
“ Vijana wa Tanzania wana uelewa mkubwa
sana hivyo wanachohitaji ni kupata fursa ya kupata mafunzo kama haya na nyenzo
ili waweze kujiajiri na pia kuweza kufundisha watu wengine, hii itawasaidia wao
kujiajiri pia,” alisema Dkt. Choi.
Kwa upande wake, Profesa Muhongo alisema
kuwa vifaa hivyo ni muhimu sana hasa katika sehemu ambazo hazijafikiwa na
nishati ya umeme na kwamba suala la kutoa mafunzo hayo kwa vijana ni muhimu
kwani itawawezesha kupata uelewa wa teknolojia inayotumika kutengeneza vifaa
hivyo pamoja na kujiajiri.
“Napata simu nyingi sana Watu wakilia,
Umeme, Umeme, hii teknolojia ni nzuri na itawasaidia wananchi wetu kupata
mwanga na pia kuchaji simu zao, hivyo nawakaribisha kuanza kutoa mafunzo hayo
mwezi Machi mwakani,” alisema Profesa Muhongo.
Hii ni mara ya Pili kwa Profesa Muhongo
kukutana na Watendaji wa kampuni hiyo ambapo mara ya kwanza alikutana nao
mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo Balozi wa Korea hapa nchini alifika
kuitambulisha kwa Waziri wa Nishati na Madini na pia kueleza shughuli za
kampuni hiyo katika sehemu mbalimbali duniani.
Katika Kikao hicho cha mwezi Novemba,
Mtendaji wa Empower, Dkt. Choi alisema
kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikitengeneza vifaa hivyo vya Umeme Jua kwa kutumia
teknolojia ya kisasa tangu mwaka 2011 na kwamba lengo lake ni kusambaza huduma
hiyo vijijini ili kuwasaidia vijana na wananchi kupata huduma ya umeme na kwa gharama nafuu.
Alitaja baadhi ya kazi ambazo
wameshazitekeleza kuwa ni pamoja na kubuni na kutengeneza Mfumo wa Umeme Jua
katika Kituo cha ‘City Christian Center (CCC)’ kilichopo Dar es Salaam pamoja
na kutengeza Paneli za Umeme Jua za gharama nafuu katika sehemu mbalimbali Barani Afrika.
Aliongeza kuwa gharama ya Paneli hizo ni nusu ya bei ya kuunganisha umeme
unaosambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao unagharimu shilingi
27,000 .
Source:Teresia Mhagama,
Post a Comment
Post a Comment