Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma, viongozi wa dini na wananchi katika kikao cha majumuisho ya ziara yake...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka kuchukua hatua
kali kwa wote waliohusika na upotevu zaidi ya sh. bilioni moja za vyama vya
ushirika.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana
jioni (Ijumaa, Januari 27, 2017) alipozungumza na watumishi wa Mkoa wa Njombe
wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani
hapa.
Alisema kati ya fedha hizo sh.
milioni 532.736 zilipotea katika SACCOS ya Kurugenzi Njombe pamoja
na sh. milioni 900 zilizopotea katika Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo
kiitwacho Wafanyabiashara Njombe SACCOS.
“Maofisa Ushirika nchini mmeendelea
kudhoofisha jitihada za Serikali katika kuimarisha ushirika. Katika eneo hili
ninahitaji Mkuu wa Mkoa ufuatilie suala hili na kuwachukulia hatua wahusiuka
wote,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wote wa
Wilaya kuwatumia warajisi wa ushirika kuimarisha ushirika Mkoani
Njombe.”Tunataka ushirika ulete tija kwa wananchi na hatutaki ushirika
ulioambatana na harakati za kugawa watu. Endeleeni kuwashughulikia wanaushirika
wasio waaminifu,”.
Aidha, Waziri Mkuu aliwasisitiza
watumishi wa umma wote nchini kuzingatia uadilifu, uaminifu, kutojihusisha na
rushwa na kutumia ipasavyo fedha za umma Serikali itachukulia hatua kali dhidi
ya watumishi wote wanaotumia nafasi zao kujinufaisha binafsi.
Alisema anataarifa za Watendaji wa
Wakuu wa Wilaya ya Makete akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Francis
Namsumbo, Mweka Hazina Bw. Edward Mdagachule, Ofisa Utumishi, Bw. Nicodemas
Tindwa na Mkaguzi wa Ndani Bw. Michael Shija kuhusika na upotevu wa sh. milioni
71 zikiwemo sh milioni 41 za UNICEF.
Waziri Mkuu alisema kuwa watumishi
hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa kwa vyombo
mbalimbali ili kuficha ubadhilifu huo. “Mkuu wa Mkoa hakikisha hatua stahiki
zinachukuliwa kuhusiana na matukio haya,”.
Pia alimuagiza Mkuu
huyo wa Mkoa kuhakikisha kuwa ……..wa Wanging’ombe Bw. Edwin Kigoda anachukuliwa
hatua stahiki kwa ubadhilifu wa sh. milioni 37.9 zilizotolewa kwa ajili ya
kuwajengea uwezo Walimu katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Mbali na watumishi
hao pia Waziri Mkuu alimtaka Bw. Ole Sendeka kumchunguza na kumchukulia hatua Ofisa
Ardhi wa Mji wa Njombe, Bw. Addo Kabange ambaye anatuhumiwa kuuza viwanja mara
mbili, kuchukua rushwa na kujipatia viwanja vingi kwa bei nafuu na kuviuza kwa
wananchi kwa bei ya juu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
alisema atawaelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG),
Msajili wa Hazina na Mrajisi wa Ushirika kuanza kufuatilia malalamiko kuhusu
umiliki wa kiwanda cha chai cha Lupembe pamoja na kufuatilia mwenendo wa
mgawanyo wa hisa za kiwanda hicho.
Alisema alipotembelea kiwanda cha
chai cha Lupembe ambapo alifarijika kukuta kiwanda hicho kimeanza kufanya kazi
baada ya kusimama kwa takriban miaka nane kutokana na mgogoro uliopo baina ya
mwekezaji wa Kiwanda hicho na Umoja wa Wakulima wa Chai Muvyulu.
Waziri Mkuu alisisitiza kwamba
Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia migogoro ya kuzuia ajira kwa wananchi,
hivyo aliahidi kushughulikia malalamiko kutoka pande hizo mbili na kutafuta
njia ya kutatua mgogoro uliopo.
Alisema baada ya kusomewa taarifa ya
kiwanda na kwa upande mwingine taarifa ya wanaushirika alibaini kuwepo kwa
mgogoro unaohitaji kutatuliwa ili kuwezesha shughuli za kiwanda kuendelea kwa
amani na usalama.
Aidha, Waziri Mkuu alielekeza shughuli za ulimaji na
uvunaji wa majani ya chai kutoka kwa wakulima na kupeleka katika kiwanda hicho
iendelee na kiwanda kisisimamishe kazi ili kulinda soko la wakulima na ajira za
watumishi wa kiwanda hicho,” alisema.
Alisema kwa kuwa kiwanda hicho
kinamilikiwa kwa ubia, alimwelekeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho kuhakikisha
kuwa wanaweka wawakilishi wawili au watatu wa wanaushirika katika Bodi ya
Kiwanda hicho.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
alizungumzia suala la kuchelewa kuanza kwa mradi wa chuma cha Liganga, ambapo
alisema ucheleweshaji huo si wa makusudi bali ni mpango wa Serikali wa
kujiridhisha na vipengele mbalimbali vya mkataba ili uwe wa manufaa kwa
Watanzania.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema baada
ya kutembelea eneo ambalo uchimbaji utakapofanyika, na kujionea maendelezo ya
wananchi yaliyopo, alipata mashaka na kiasi cha sh. bilioni 13 kilichotengwa na
wawekezaji kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo.
Alisema Serikali haina budi kufanya
tathmini ya kina na kujiridhisha. “Nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge (Deo
Ngalawa-Ludewa) na Mwenyekiti wa NDC kujiridhisha na wahusika wanaotarajiwa
kupata fidia hiyo,”.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya
watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali
kupitia Bodi ya Motisha na Mishahara inaendelea kufanya tathmini ya uzito wa
kazi ili kupanga upya viwango vya motisha na mshahara kwa watumishi wote.
Pia
aliwasisitiza waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya
likizo, masomo na uhamisho, kuandaa leave roster na mipango ya
mafunzo kwa watumishi.
COMMENTS