Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe akiwa na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Malinyi akiwemo mkuu wa wilaya , Majula Kasika , wakiwa pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Lumbanga, ya jamii ya wafugaji wa kisikuma , baada ya kuweka jiwe la msingi katika kitongoji cha Salatongo, kijiji cha Misegese, Kata ya Malinyi 
HALMASHAURI ya wilaya ya Malinyi, mkoa wa Morogoro,imetoa kiasi cha Sh milioni tisa kwa ajili ya kupaua jengo la vyumba viwili vya madarasa Shule ya Msingi Lumbanga ya watoto wa jamii ya wafugaji wa Kisukuma ili kuwaondoa kwenye  mabanda yaliyojengwa na  mabua ya ufuta na kuezekwa  nyasi. 

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Marcelin Ndimbwa, kabla ya mkuu wa wilaya hiyo, Majula Kasika, kumkaribisha mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe.

Dk Kebwe , alikuwa mgeni rasmi katika uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya mwalimu ya shule ya Msingi Lumbanga, katika kijiji cha Misegese, wilayani humo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo , baada ya wananchi ambao ni jamii ya wafugaji wa kisukuma kujitokeza kujenga jengo hilo hadi kufikisha hatua ya linta , halmashauri ya wilaya imetenga Sh milioni tisa kwa ajili ya kupaua jengo hilo.


Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, ( kati kati) akipinga makofi baada ya kuweka   jiwe la msingi la ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya mwalimu ya shule ya Msingi Lumbanga, kitongoji cha Salatongo, kijiji cha Misegese, Kata ya Malinyi ,wilayani humo. Wakwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Marcelin Ndimbwa,  na ( kulia) ni mkuu wa wilaya hiyo, Majula Kasika.

Mwalimu mwanzilishi wa  shule ya Msingi Lumbanga, iliyopo katika kitongoji cha Salatongo, kijiji cha Misegese, Kata ya Malinyi, wilaya ya Malinyi, mkoa wa Morogoro, Masunga Kanuda , akipita karibu na banda la darasa la shule hiyo lililojengwa kwa mabua ya ufuta na kuezekwa nyasi,

Baadhi ya wanafunzi wa  shule ya Msingi Lumbanga, iliyopo katika kitongoji cha Salatongo, kijiji cha Misegese, Kata ya Malinyi, wilaya ya Malinyi, mkoa wa Morogoro wakiwa karibu na jengo jipya la  madarasa ya  shule hiyo  lenye  vyumba viwili na ofisi moja ya mwalimu 

Awali, Katibu w Kamati ya Ujenzi wa shule hiyo, Joseph Pascal, katika risala yake kwa mkuu wa mkoa alisema,shule ya Lumbanga tarajiwa iliyopo katika kitongoji cha Salatongo, kijiji cha Misegese, Kata ya Malinyi, ilianzishwa Machi 24, 2012 na wanafunzi 16 wa chekechea. 

Alisema hadi sasa shule hiyo ina wanafunzi 250 kati ya hao wavulana 150 na wasichana 100 ambao ni kuanzia darasa la awali hadi la nne, na walimu watatu wa kujitolea wanaolipwa posho kutokana na michango ya wazazi na walezi wa watoto hao wa jamii ya wafugaji.

Katibu wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo alisema , kuanzishwa kwa shule hiyo imesaidia kuokoa watoto wengi  ambao walikuwa wanachunga ng’ombe na maisha ya kuhamahama .

Alisema kuwa , hadi sasa wengi wa watoto hao baada ya kuandikishwa shule  wanajua kusoma na kuandika.

Pascal, alisema ujenzi wa shule hiyo unatokana na mwitikio wa wazazi uliokuwa umetolewa na mkuu wa mkoa alipotembelea Kitongoji hicho na kukuta watoto wakisoma katika  mabanda mawili yaliyojengwa kwa  mabua ya ufuta na kuezekwa nyasi  na  wakiketi kwenye  mbao za magogo.

Alisema ,kitongoji hicho kina kaya 405 , ambapo kaya 250 zimechangia jumla ya Sh 7,650,000 , wakati kaya 150 bado hazijatoa michango yao  na  hatua ya  ufuatiliaji  kupitia kamati ya ujenzi wa shule hiyo inaendelea kufanyika.

 Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo pia alisema Ofisi ya mkuu wa wilaya ilichangia Sh 2,580,000 fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya safari ya uzimaji Mwenge wa Uhuru mwaka jana , wakati Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dk Haji Mponda akichangia Sh 500,000.

Naye  mkuu wa mkoa Dk Kebwe, aliitaka Kamati ya ujenzi kuongeza kasi ya ukusanyaji wa michango ili ziweze kupatikana fedha kwa ajili ya kumalizia hatua ya ujenzi kufikia ngazi ya linta ili halmashauri iweze kupaua jengo hilo.

Pia aliutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuharakisha ukamilisha jengo hilo  hadi kufikia Machi mwaka huu  ili wanafunzi wanaosomea katika mabanda hayo waweze kuhamia.

Lengo  waondokane  na adha wanayoipata hasa wakati wa mvua kulowa maji kipindi cha mvua zitakapoanza kunyesha na wanafunzi 12 waliofaulu darasa la nne  wahamishiwe shule mama ya Miembeni.

Dk Kebwe , aliuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuwapatia fursa ya kuwasomesha walimu waanzilishi hao vyuo vya ualimu ili wakuze taaluma na kuwa na sifa rasmi za  kufundisha shule za msingi na kipaumbele kupangiwa kwenye shule hiyo.

Kwa upande wake , mkuu wa wilaya hiyo, Kasika, alisema , wilaya imefanya utambuzi wa maeneo ya wafugaji  na kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha watoto wa jamii ya wafugaji wanapata fursa ya kupata elimu ya awali, msingi na sekondari.

“ Shule za aina hii za wafugaji zipo nyingi katika wilaya ya Malinyi na kwamba wilaya inajitahidi kuboresha ili kutoa fursa kwa watoto wa jamii hii watape elimu “ alisema Mkuu wa wilaya.

Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hyo wa darasa la nne , Msua Yohana na mwenzake Hinda Mwita, kwa nyakati tofauti walimpongeza mkuu wa mkoa kwa kuwahimiza wazazi wao kujenga shule hiyo ambayo itawapa wao fursa ya kusoma bila kupata mateso kama ilivyo sasa kwenye mabanda hayo.

Walisema , kutokana na kuvunja wakati wa masika , wanalazimika kukatisha masomo hadi jua litakapowaka na pia kuumia mgongo kwa kujipinda chini na kuchafuka kwa sare zao za shule , na kwamba kukamilika kwa jengo hilo ni ukombozi kwao.

source:John Nditi HabariLeo


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO