Kaimu Mkurugenzi   Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba, akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya TPDC kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2016 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Wengine wanaofuatilia ni Watendaji kutoka Wizarani na TPDC.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba ameileza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa, hivi sasa zaidi ya asilimia 50 ya umeme uliopo katika Gridi ya Taifa unatokana na gesi asilia.

Mhandisi Musomba aliyasema hayo hivi karibuni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya TPDC kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba, 2016 na kuongeza kuwa, mipango ya Serikali ni kulifanya Shirika hilo kuchangia zaidi mapato Serikalini yanayotokana na rasilimali hiyo.

Aidha, alieleza kuwa, kwa kuwa Tanzania imeingia kwenye uchumi wa Gesi asilia, shirika linajipanga kuwekeza kwenye shughuli za utafutaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi ili Taifa linufaike na rasilimali hiyo.

Akifafanua shughuli ya usambazaji gesi asilia kwa kuzalisha umeme, alisema kuwa, TPDC inaendelea kuhakikisha kwamba mitambo ya kuzalisha umeme inaunganishwa na miundombinu ya usambazaji gesi asilia ili iweze kutumia gesi asilia kuzalisha umeme.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, TPDC kwa kushirikiana na TANESCO iliendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu ya Kudumu ya usambazaji gesi asilia kwenye mitambo ya Kinyerezi I, Ubungo II,Tegeta na IPTL,”alisema Musomba.

Akizungumzia matumizi ya gesi asilia viwandani, Mhandisi Musomba alisema kuwa, katika kipindi cha mwaka  wa fedha 2016/17, Shirika linaendelea na shughuli za kutafuta wateja zaidi na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi kwa wateja na kuwataja baadhi ambao wamefanya majadiliano kuwa ni pamoja na viwanda vya Dangote Cement Tanzania Limited, Goodwill Ceramic Tanzania Limited, Bakhresa Food Factory , Knauf Gypsum na Lodhia Steel vilivyopo Mkuranga Pwani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Doto Biteko, aliitaka TPDC kusaidia kuokoa uharibifu wa mazingira kwa kuwezesha mradi wa usambazaji gesi majumbani ili wananchi waachane na matumizi ya mkaa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilikutana na Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake kuanzia tarehe 23- 26 Januari, 2017 kwa lengo la kupokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi na shughuli za Wizara na Taasisi zake.


Mbali na Kamati hiyo, Wizara  pia ilikutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ambapo ilipokea taarifa fupi ya Wanafunzi wa Kozi ya Mazingira ya Chuo Cha Madini Dodoma.
source:Nuru Mwasampeta na Asteria Muhozya, Dodoma.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO