Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakishiriki matembezi kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani yaliyoandaliwa na Taasisi ya Pink Ribbon Red Ribbon yaliyohitimishwa katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road jijini humo

WATANZANIA takribani 50,000 kila mwaka wanagundulika na ugonjwa wa saratani za aina mbalimbali nchini huku saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ikiongoza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa imeelezwa. 
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani jijini Dar es Salaam leo iliyoandaliwa na Taasisi ya Pink Ribbon Red Ribbon, Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukiza katika wizara hiyo, Prof. Ayoub Magimba alisema kutokana na ongezeko hilo serikali imechukua hatua kadhaa kupambana na kasi ya ongezeko la saratani nchini,
“Kwa Tanzania wagonjwa wa saratani wanatarajia kuongezeka kwa asilimia 50 kufikia 2035,  serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wengine tuko pamoja katika kudhibiti janga hili la magonjwa ya saratani,” alisisitiza
 
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakishiriki matembezi kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani yaliyoandaliwa na Taasisi ya Pink Ribbon Red Ribbon yaliyohitimishwa katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road jijini humo

Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa yasiyoambukiza wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Ayoub  Magimba (wa pili kulia), akishikana mikono na Mkrugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Pink Ribbon Red Ribbon, Celina Schocken katika hafla ya kuwatangaza washindi wa shindano la ubunifu wa mchoro wa majengo ya makazi ya wagonjwa wa saratani

Mkurugenzi huyo alisema katika Taasisi ya Ocen Road taarifa zinasema katika kipindi cha 2006 hadi 2016 saratani zinazoongoza ni shingo ya kizazi (32.8%), matiti (12.8%), ngozi(11.9%), mfumo wa njia ya chakula (10.9%), kichwa na shingo (7.5%) ikifuatiwa na saratani nyingine ya tezi dume ikiwa ya mwisho kwa asilimia 2.1.
“Kwa mara nyingine tena, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Taasisi ya George W Bush (The George W Bush Institute), HKS, Chuo Kikuu cha Southern Methodist (SMU) na T-MARC Tanzania ambao wamejitoa kuokoa maisha ya kinamama na wasichana wa Tanzania,” aliongeza.
Katika hafla hiyo ambayo Taasisi ya Pink Ribbon Red Ribbon ilikuwa ikitangaza washindi wa shindano la ubunifu wa michoro ya majengo kwa ajili ya wagonjwa wa saratani katika taasisi ya saratani ya Ocean Road.
Mkurugenzi  Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Pink Ribbon Red Ribbon, Celina Schocken alisema ni matarajio yao majengo ya makazi hayo yatakuwa mkombozi mkubwa kwa wanawake na wasichana wanaokwenda kupata matibabu ya saratani katika hospitali hizo.
“Kwa vituo viwili nchini kutibu saratani huwafanya maelfu ya wanawake ama kusafiri umbali mrefu na kulala katika nyumba za wageni kwa gharama kubwa au kama wengi wanavyoamua kubaki nyumbani na kusubiri siku ya kufa,” alisema.   

 
Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa yasiyoambukiza wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Ayoub  Magimba (wa tatu kushoto), akimpongeza mmoja wa washindi wa shindano la ubunifu wa mchoro wa majengo ya makazi ya wagonjwa wa saratani, Henok Yared kutoka Taasisi ya Ubunifu Majengo ya Ethiopia.
 Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Julius Mwaiselage alisema kwamba katika maadhimisho hayo ni muhimu wananchi  kupata elimu, taarifa juu ya ugonjwa huo, dalili zake na namna sahihi ya kukabiliana nao.
“Sisi kwa upande wetu tunalo jukumu la kuelimisha umma juu ya uwepo wa ugonjwa wa saratani na kuchukua maamuzi sahihi ya kupata tiba katika taasisi husika,” aliongeza
Alifafanua kwamba hatua kubwa iliyochukuliwa na Rais John Pombe Magufuli ya kutoa kiasi cha shilingi za kitanzania 5 billioni kwenye taasisi ni jambo la kupongezwa kwa moyo wa dhati wa Rais kusaidia wagonjwa wa kansa nchini.
Katika shindano hilo, wanafunzi wa Taasisi ya Ubunifu Majengo ya Ethiopia, Akrem Abdulrahima, Emaelaf Tebikew na Henok Yared walishinda mchoro wa jingo litakalojengwa katika Hospitali ya Bugando, huku washindi wa pili na watatu wakitoka Moscow, Marratech, Dar es Salaam na Santa Domingo.
Mwisho

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO