Majina ya wanasiasa, wafanyabiashara, viongozi wa dini pamoja na wanawake kadhaa katika Jiji la Dar es Salaam, yametajwa katika orodha mpya ya watu 65 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, inayowapa mwito wa kujitokeza katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini humo kuzungumza nao kuhusiana na suala la dawa za kulevya.

Orodha hiyo imetangazwa ikiwa ni siku sita baada ya kutangazwa kwa majina ya awali ambayo iliwahusisha wasanii mbalimbali wa maigizo na muziki.

Katika orodha mpya ya majina yaliyotangazwa leo yakihusishwa na biashara hiyo ama kwa kuuza, kutumia na wengine wakiitwa kwa ajili ya kutoa taarifa za wanaowafahamu miongoni mwa waliotajwa ni Mchungaji wa Kanisa la Uzima na Ufufuo, Josephat Gwajima na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azzan.

Pia yumo Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe pamoja na Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yussuf Manji.

Akitangaza orodha hiyo jana jijini Dar es Salaam, Makonda aliwataja pia wamiliki wa hoteli na maduka mbalimbali ambao wanasadikiwa kujihusisha na biashara hiyo wakiwemo wamiliki wa Sleep way ambaye ametajwa kuwa na eneo kubwa kwa ajili ya kuegesha boti ambazo zinasadikiwa kuhusika na usafirishaji wa dawa hizo.

Wengine waliotajwa ni wamiliki wa Trinity, Yatch Club, kasino ya Sea Cliff, kasino ya Palm Beach na mmiliki wa duka la MMI Wine.

Kuhusu wafanyabiashara, yupo mmiliki wa duka la nguo Mwinyi Machapta, Hussein Pambakali pamoja na Rose China ambaye ni mfanyabiashara kwa sasa yupo Ghana

Aidha, Makonda pia amewataka wamiliki wa kampuni tatu zinazojihusisha na usafirishaji wa mafuta, nao kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi baada ya kampuni zao kutajwa katika suala hilo, ambazo ni Kampuni ya Tanga Petroleum, GBP Tanzania Limited na NAS Haulage Limited.

“Hawa nataka wafike Central Ijumaa tuongee nao tuone kama ni kweli wanahusika. Wapo ambao nimeambiwa wako nje ya nchi, ninawataka waje na wakigomea huko nje zipo njia nyingi naimani wale watakaojificha tutawatafuta na tutawapata,” alieleza Makonda.

Mbali na majina hayo, wapo watu waliotajwa ambao sio maarufu akiwemo Hemed Horohoro ‘Mamba’, Juma Sapefu ’Bundala’, Juma ‘Jay’, Abdala Kandila wa Rainbow Bar, Remmy Muselemi Moshi Bar, Halil Muarabu Kinondoni Studio,  Hassan Chinga, Mzee Kiboko Mkazi wa Mbezi chini, How Come Mpemba wa Magomeni Mapipa.

Majina ya watu wengine walioitwa Polisi kupitia wito wa Makonda ni Hassan Chinga mkazi wa Makumbusho, Abdala Mwakaliti mkazi wa Sinza, Sahad Mwakaliti mkazi wa Sinza, Idrisa Maunga mkazi wa Msasani, Boss Chizenga mkazi wa Mbezi Beach, Abdil Kadinda mkazi wa Mbezi Beach na Deo Mchaga mkazi wa Kinondoni.

Wengine Jeni Geneva mkazi wa Mwananyamala, Hussein Mwarabu mkazi wa Wazo na Hassan Kudeba mkazi wa Magomeni.

Wilaya zinazoongoza kuwa na watuhumiwa wengi wanaojihusisha na dawa hizo ni Kinondoni, Ilala pamoja na Ubungo.

Mkuu huyo wa mkoa alizitaja njia zinazotumika katika kusafirisha dawa za kulevya kuingia nchini ni pamoja na meli zinazopakiza mizigo ambazo hutumika kuweka dawa  kwenye mapipa na kuyafunga kwa kiwango ambacho hakipitishi maji na kuingiza kwenye meli na inapokaribia bandarini, wanayatupa mapipa hayo.
Alitaja maeneo ambayo mapipa hayo hutupwa ni Bandari ya Zanzibar, Bagamoyo pamoja na Tanga.

“Wanatupa mapipa yenye dawa za kulevya yakiwa na mashine za GPRS na kuwasiliana na timu yao ambayo inakwenda na mashine za kutambua GPRS na kuyaokoa na baada ya kuyatoa wanasafirisha kwenda Mtwara na baadaye wanakwenda Afrika Kusini. Tumewalea sana watu hawa na wao kuona kuwa hamna mtu anayewaweza kuwagusa sasa niseme muda huo umekwisha nia yao kwa nchi yetu sio nzuri,” alifafanua Makonda.

Pia alisema njia nyingine inayotumika kusafirisha dawa hizo ni pamoja na usafirishaji wa magari ambapo mtu ananunua gari Japan na kwenda mzunguko mrefu, kwa kile alichoeleza kuwa wanaweka madawa na kusafirisha.

Aidha, Makonda amewapongeza wenyeviti wa serikali za mitaa na wazazi ambao wameanza kuwataja watu wanaowadhania wanajihusisha na biashara hiyo katika mitaa yao.

“Wenyeviti wangu wa mitaa yote 567 msichoke endeleeni juhudi hizi na baaada ya siku hizi kumi, tutaweza kuanza mchakato wa kutangaza awamu ya tatu ambayo itakuwa ya kupita nyumba kwa nyumba mkiendelea na moyo huu vita hii tutashinda,” aliongeza Makonda.

Aidha, alisema Watanzania wanapaswa kufahamu suala la kufuatilia dawa za kulevya hakulianza hivi karibuni, bali alianza muda mrefu hivyo ambapo hakutaka iende kimya kimya hivyo amewataka kuunga mkono juhudi hizi na sio kumrudisha nyuma.

“Nina maumivu pale ninapopita barabarani na kuwakuta mateja wengi halafu unaanza mapambano ya kuwaokoa wanaibuka watu na kutaka kukwamisha juhudi zako. Niseme tu suala la madawa ni suala gumu, lakini ni suala letu sote ni lazima tuunge mkono juhudi hizi lengo likiwa ni kuokoa kizazi chetu,” alisisitiza Makonda.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO