WASIFU WA MAREHEMU BALOZI SIR CLEMENT GEORGE KAHAMA Balozi Clement George Kahama, aliyejulikana zaidi kama Sir George alizaliwa tarehe ...
WASIFU WA MAREHEMU BALOZI SIR CLEMENT GEORGE
KAHAMA
Balozi
Clement George Kahama, aliyejulikana zaidi kama Sir George alizaliwa tarehe 30
Novemba, 1929 katika Wilaya ya Karagwe na kufariki dunia tarehe 12 Marchi, 2017
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ugonjwa
wa Figo Renal Failure) kwa takribani miaka miwili.
Katika
uhai wake, Marehemu alifanya kazi katika Serikali kwa vipindi mbalimbali zaidi
ya miaka 50 ikiwemo awamu tatu za uongozi wa taifa hili baada ya uhuru wa
Tanganyika tarehe 9 Desemba, 1961. Marehemu Sir George alikuwa miongoni mwa
waafrika wachache waliopata fursa ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria yaani Legislative Council mwaka 1957 na miaka
miwili baadaye kuteuliwa kuwa Waziri katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya
Mpito ya kikoloni kuelekea uhuru kwa nafasi ya Waziri wa Ushirika na Ustawi wa Maendeleo ya
Jamii akiwa na Wenzake wazalendo Chief Abdalah Fundikira, Amir Jamal, na Solomon
Eliufoo na Mwalimu akawa Waziri Kiongozi
( Chief Minister).
Baada ya Uhuru Mwaka 1961, Mhe Balozi George
Kahama aliteuliwa kuwa Waziri wa kwanza wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
katika Baraza la Mawaziri la Watu tisa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
akiwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru. Kutoka Uhuru mwaka 1961 hadi mwaka 2005 Sir
George Kahama aliuteuliwa na Baba wa taifa na baadaye Mhe. Benjamin Mkapa, Rais
Mstaafu wa awamu ya tatu, kushika nyazifa za Wizara mbalimbali serikalini zikiwemo
Wizara ya Mawasiliano, Uchukuzi na Ujenzi, Wizara ya Biashara na Viwanda,
Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ushirika na Masoko, Waziri Ofisi ya
Rais anayeshughulikia Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma na wakati huohuo akiwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA).
Katika
muda wote wa utumishi wa Umma, Sir George aliaminiwa sana na Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere baadaye Mhe Benjamin Mkapa kwa nyakati tofauti waliweza kumtuma
katika nchi mbalimbali kuwawakilisha kama
mwakilishi maalum wa Rais (Special Envoy) katika nchi mbalimbali ikiwemo
Zaire ambayo sasa inajulikana kama DRC, Burundi na Rwanda, Holy See (Vatican) na nchi nyingine.
Kazi
nyingine alizowahi kufanya Mhe Sir George Kahama ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu
wa kwanza wa Shirika la Maendeleo la taifa (NDC), taasisi iliyopewa jukumu la
kusimamia uanzishwaji wa Viwanda nchini, Mkurugenzi Mkuu na mwanzilishi wa Kituo cha Kuvutia wawekezaji (IPC) ambacho baadaye kimekuja
kujulikana kama Tanzania Investment
Centre-TIC. Kabla ya Uhuru Sir George alikuwa kiongozi wa Chama cha ushirika
cha Bukoba, chama ambacho kilitoa msaada
mkubwa wa hali na mali katika kusaidia harakati za ukombozi na kuimarisha TANU
kama ilivyokuwa kwa vyama vingine vya Ushirika katika maeneo mbalimbali nchini.
Itakumbukwa kuwa Wazalendo watano
waliounda Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mpito mwaka 1959 akiwemo Mzee Paul
Bomani, Chief Abdullah Fundikira (Tabora), Solmon Eliufoo (Kilimanjaro), Amir
Jamal ( Morogoro) na Kahama Mwenyewe (Kagera) walikuwa viongozi katika vyama
vya ushirika katika maeneo waliyotoka.
Aidha,
katika Uhai wake, Sir George Kahama aliwahi kutumikia taifa katika nyanja za
kidiplomasia kama Balozi wa Tanzania Ujerumani mwaka 1965-1966, Balozi wa
Tanzania China (1984- 1989) na Balozi wa Tanzania Zimbabwe (1989-1991).
Katika
uhai wake, Sir George Kahama aliwahi kutunikiwa nishani mbalimbali za kitaifa
na Kimataifa ikiwemo Knight Commander of the Order of St. Gregory the Great
iliyotolewa na Pope John XXIII mwaka 1962. Hii ndiyo nishani iliyozaa jina la Sir George. Nishani
zingine ni kama “The Order of Kilimanjaro iliyotolewa na Rais Mstaafu Ali
Hassan Mwinyi 1990, ambayo ni nishani ya juu kabisa wanayotunukiwa watumishi wa
umma. Mwaka 1975-1976 alikuwa Mjumbe wa Kundi la Watu Mashuhuri duniani walioteuliwa
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufanya utafiti kuhusu athari za Uendeshaji
wa Makampuni Makubwa ya Kimataifa katika uchumi wa nchi zanazoendelea.
Mabadiliko
mbalimbali yaliyofanyika ndani ya Chama cha Mapinduzi na Serikali ikiwemo Serikali
kuhamia Dodoma kwa kasi kubwa na chama
kuimarika zaidi kumetokea siku chache kabla ya kufariki kwake na kutimiza
ndoto yake zaidi ya miaka 40 aliyojishughulisha
na mradi wa Ustawishaji ya Makao Makuu.
Mwaka
1976, Sir George aliteuliwa na Serikali ya Nigeria kama Mjumbe wa Kamati ya
watu watatu waliopewa kazi ya kufanya tathmini ya mchakato wa uhamishaji wa Mji
Mkuu wa Nigeria kutoka Lagos kwenda Abuja.
Sir
George aliwahi kuandika maandiko na vitabu mbalimbali katika Nyanja za Kidiplomasia, Ushirika, Uchumi, Maendeleo ya Ujenzi, ikiwemo kitabu cha “The
Challenge for Tanzania’s Economy” kilichochapishwa na kampuni ya James Currey
Heinemann ya Uingeleza na “Tanzania into the 21st Century”,pia
alichangia kuandika kitabu cha “The First Tanganyika Industrial Development
Blue Print” pamoja na Arthur D. Little
Inc. wa Marekani.
Mbali
na utumishi Serikalini, Sir George Kahama alikuwa Baba mzuri wa familia
aliyependa umoja wa familia na alikuwa baba tuliyemtegemea kwa ushauri na dira
katika maisha yetu.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana Lihimidiwe
Utaratibu wa Maombolezo na Mazishi ya Balozi Sir Clement
George Kahama aliyefariki Dunia tarehe 12 Machi, 2017
Mwili wa
marehemu utawasili nyumbani kwake eneo la Mikocheni B kituo cha Mabasi
kijulikanacho kama Business, mnamo saa 11 jioni tarehe 15 Machi, 2017
(Jumatano) na kukesha hadi asubuhi tarehe 16 Machi, 2017.
Mwili wa
Marehemu utaondolewa nyumbani kwake kuelekea Julius Nyerere International
Convention Centre kuanzia saa mbili
kamili kwa ajili ya viongozi mbalimbali na wananchi kutoa heshima zao za mwisho
kabla ya kuelekea Kanisa la Mtakatifu Petro ( St. Peters) Oysterbay Dar es
salaam saa tano na nusu 5.30 asubuhi kwa ibada.
Ibada ya
mazishi itafanyika katika Makaburi ya Kinondoni
kuanzia saa tisa na nusu 9.30
alasili.
COMMENTS