RAIS, Dk John Magufuli akiongoza kwa mara ya kwanza Sherehe za Miaka
53 ya Mapinduzi tangu aingie madarakani mwishoni mwa mwaka juzi,
ameapa kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa nguvu zake
zote, huku akiapa yeyote akayejaribu kuleta chokochoko za kutaka
kuuvunja, atavunjika yeye kabla ya Muungano.

Akizungumza katika hotuba fupi ya dakika 17 jana kwenye Uwanja wa
Jamhuri mjini hapa ambako sherehe za Muungano zimefanyika kwa mara ya
kwanza tangu Uhuru na pia kwa mara ya kwanza tangu Serikali ihamishie
rasmi makao makuu ya nchi Dodoma kuanzia mwishoni mwa mwaka jana,
alisema kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, DK Ali Mohamed Shein,
watafanya kila linalowezekana kuhakikisha muungano inazidi kuimarika,
badala ya kuvunjikia mikononi mwao.

“Nataka niwahakikishie, mimi na Dk Shein tutaulinda kwa nguvu zote
Muungano huu, na kamwe asijitokeze mtu yeyote, atakayekaidi au
kujaribu kuvunja Muungano, atavunjika yeye…," alisema.

Alisema kufikisha umri wa miaka 53 ya kuzaliwa kwa taifa la Tanzania
si jambo dogo, kwani mataifa mengi yamejaribu kufanya hivyo, lakini
bila ya kufanikiwa, huku akisisitiza kwa kusema,”Hii ni siku ya
kipekee, ya kihistoria kwa tanzania. Leo ni `Birthday’ (siku ya
kuzaliwa) ya Tanzania.”
Aliongeza kuwa, si  jambo dogo kusherehekea Miaka 53 ya Muungano,
kwani kazi ya kuulinda Muungano  ni ngumu, kwa sababu hata kulinda
ndoa ni ngumu.

“Hii inathibitisha kuwa suala la kulinda muungano si jambo rahisi hata
kidogo, hivyo basi hatuna budi kuwapongeza waliofanikisha nchi yetu
kufikisha miaka 53, tunawapongeza sana.

“Tunafahamu wapo wengi waliotoa mchango wao, lakini kwa leo nitawataja
wote. Wa kwanza kwa niaba yenu, napenda niwashukuru waasisi wa
Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa
Zanzibar,  Hayati Abeid Amani Karume kwa kuufanikisha na kuuwezesha
Muungano huu. Hawa ndio waliosaini hati ya Muungano, bahati nzuri, leo
hii tunao hapa Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume,” alisema.

Aliwapongeza pia viongozi wote wan chi katika awamu zote, Ali Hassan
Mwinyi aliyeiongoza Serikali ya Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa wa Awamu
ya Tatu na Jakata Kikwete aliyeiongoza Awamu ya Nne, lakini pia
waasisi mbalimbali. Alirudia kuahidi yeye na Dk Shein, watafuata nyayo
za kuulinda na kuutetea Muungano huo.

Aidha, alisema wakati Watanzania wakisherehekea kutimiza miaka 53 ya
kuzaliwa kwa taifa la Tanzania, ni vyema watu kutafakari walikotoka,
walipo na wanakokwenda.

“Niwaombe pia baada ya kuzaliwa kwa taifa la Tanzania mwaka 1964 na
leo tunatimiza miaka 53, ni ushahidi Watanzania wengi tunaoishi, ambao
ni asilimia kubwa wamezaliwa baada ya Muungano, kwa hiyo tuna wajibu
mkubwa, bila kujali makabila wetu, bila kujali vyama vyetu na bila
kujali maeneo yetu, kuulinda na kuudumisha Muungano huu ili taifa la
Tanzania liendelee kudumu,” alisema.

Alisema anafahamu kukiwa na mshikamano, itawezekana kuulinda Muungano,
hivyo kushauri Watanzania wazidi kushikamana ili kuwe na miaka mingine
mingi zaidi ya kusherehekea Muungano.

Changamoto; za Muungano

Alisema licha ya mafanikio, bado zipo changamoto za Muungano, lakini
akaahidi kuwa zinashughuliwa kwa kuwa kuna Kamati ya Pamoja
inayoshughulikia masuala ya Muungano ambayo Mwenyekiti wake ni Makamu
wa Rais, Samia Hassan Suluhu na wajumbe ni pamoja na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd,
mawaziri na makatibu wakuu wa Serikali zote mbili.

Alisema kamati hiyo inafanya kazi nzuri, lakini pia haipaswi kuachwa
ifanye kazi peke yake, hivyo kila Mtanzania awe mshiriki wa kulinda
Muungano.

Alisema dhamira hiyo inashabihiana na kaulimbiu ya sherehe za  mwaka
huu, inayosema “Miaka 53 ya Muungano; “Tuulinde, Kuuimarisha. Tupige
Vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii,” hivyo kusema imekuja
kwa wakati mwafaka.

Kuhamia Dodoma

Alisema kufanyika kwa sherehe hizo mkoani Dodoma kwa mara ya kwanza
katika historia ya Tanzania, ni ishara kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) imedhamiria kwa dhati
kuhakikisha makao makuu ya Serikali yanahamia Dodoma.

“Na niwahakikishie wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla, Serikali
sasa imefika Dodoma na hatutarudi nyuma tena. Kama tulivyoahidi,
kufikia mwaka 2020 serikali yote itakuwa imehamia hapa,” alisema na
kushangiliwa mno.

Rais Magufuli ambaye mwaka jana alifuta sherehe za miaka 52 ya
Muungano na kupeleka fedha kiasi cha Sh bilioni 2 katika shughuli ya
upanuzi wa barabara ya Uwanja wa Ndege jijini Mwanza, alisema katika
kuthibitisha utayari wa kuhamia Dodoma, tayari hatua kadhaa
zimefanyika.

Alizitaja kuwa ni pamoja na mawaziri wote, manaibu waziri, makatibu
wakuu, manaibu na wakurugenzi mbalimbali wameshahamia Dodoma. Alisema
zaidi ya watumishi wa umma 3,000 wameshahamia Dodoma.

Lakini pia alisema awamu ya pili na ya tatu ya kuhamia Diodoma
imepangwa kuhamia katika mwaka ujao wa fedha, ambapo serikali imepanga
kutumia zaidi ya Sh bilioni 200 kwa ujenzi wa ofisi na nyumba za
viongozi wa Serikali.

Aidha, amesema juhudi za kujenga miundombinu ya usafiri na
usafirishaji, ikiwemo ya upanuzi uwanja wa ndege, lakini pia ujenzi wa
reli ya kisasa itakapita Dodoma, ujenzi wa barabara unaendelea sehemu
mbalimbali, upatikanaji umeme, huduma za afya, elimu lakini pia
maandalizi ya ujenzi wa uwanja mkubwa na wa kisasa wa michezo
utakaojengwa na Serikali ya Morocco.

“Yote haya yanalenga kukidhi mahitaji ya kuwa makao makuu ya nchi,”
alisema na kuwataka wakazi wa Dodoma na mikoa jirani Singida, Arusha,
Manyara, iringa na Morogoro, kujipanga kutumia fursa za Dodoma kuwa
makao makuu ya nchi.

Pamoja na dhamira nzuri ya Serikali ya kutaka kuulinda Muungano,
alisema hiyo itakuwa kazi bure kama nchi haitakuwa na amani na kusema
kama waasisi wasingeweza kulinda amani, leo hii Watanzania wasingekuwa
na chereko za miaka 53 ya Muungano, hivyo kusisitiza kila mmoja
ashiriki kuilinda amaniya nchi iliyopo.

Faida za Muungano
Alisema licha ya awali kuwapo kwa mwingiliano baina ya watu wa
Tanganyika na Zanzibar, miaka 53 ya Muungano, nchi imekuwa na faida
nyingi zaidi, mojawapo ikiwa kuwa taifa lenye nguvu, hivyo kuwezesha
kulinda uhuru, amani na umoja. Alisema nchi imekuwa yenye amani na
mipaka iko salama.

Aidha, alisema Muungano umewezesha mafanikio makubwa katika nyanja za
kiuchumi, kisiasa na kijamii.

“Serikali zetu mbili zimefanya jitihada za kiuchumi na pia kukabiliana
na matatizo ya kimasikini na ukosefu wa ajira. Mambo mbalimbali
yameimarika, demokrasia pia imeimarika.
Tanzania ya sasa si ile ya mwaka 1964. Lakini pia tunaheshimika kimataifa.

"Jamani, tusione vyaelea, vimeundwa na kuna watu wamefanya kazi usiku
na mchana kuhakikisha Muungano huu unadumu,” alisema na kuongeza kuwa,
nchi imekuwa yenye heshima kubwa kimataifa imekuwa ikisaidia katika
shughuli za ukombozi na kutafuta amani katika nchi mbalimbali kikanda
na duniani kwa ujumla.


Source:eric mkutai habarileo

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO