HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI...
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja
kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu
na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako
sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali
kwa mwaka 2016/2017 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018. Aidha,
ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko
wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
2.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge
lako Tukufu limeondokewa na Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani - CCM na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha,
aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum - CHADEMA. Pia, Taifa lilimpoteza Mheshimiwa
Samwel John Sitta aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Aidha, nchi yetu imekumbwa na majanga na maafa
yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Ninaomba Mwenyezi Mungu
awajalie nafuu ya haraka wale wote waliopata majeraha, na kuwapumzisha kwa
amani wale waliopoteza maisha, Amina!
Ninatoa pole kwa familia za wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki. Pia
ninatoa pole kwa Mheshimiwa Aida Khenani aliyepata ajali ya kugongwa na
pikipiki wakati akitoka Bungeni. Tunamuombea apone haraka na aweze kurejea
Bungeni ili kuendelea na majukumu yake.
PONGEZI NA SHUKRANI
3.
Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa hii
kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Makamu wa Rais na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa kutimiza mwaka mmoja wa
uongozi wao. Sisi tunaowasaidia tunajivunia uongozi wao mahiri, uzalendo
uliotukuka na dhamira njema waliyonayo kwa Watanzania.
4. Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limepokea na kuwaapisha Wabunge wapya
watano, ambao ni Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb.), Mheshimiwa Anne
Killango Malecela (Mb.), Mheshimiwa Juma Ali Juma (Mb.), Mheshimiwa Prof.
Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) na Mheshimiwa Salma Rashidi Kikwete
(Mb.). Ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wapya kwa heshima waliyoipata ya
kujumuika nasi kwenye Bunge hili. Kama ilivyo ada, tutatoa ushirikiano
unaotarajiwa kwa Waheshimiwa Wabunge hawa ili watekeleze majukumu yao kwa
ufanisi na tija. Kipekee, ninampongeza Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan
Mwaluko Kabudi (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Pia ninatumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge wote walioteuliwa kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Makatibu
Wakuu wapya walioteuliwa na Mheshimiwa Rais yaani Profesa Kitila Alexander
Mkumbo, Dk. Leonard Akwilapo, Maimuna Tarishi na Dk. Ave Maria Semakafu.
Nawapongeza sana wote walioteuliwa kushika nyadhifa hizo.
5.
Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa hii
kuwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali
zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ninawashukuru kipekee sana Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa
Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile,
Mbunge wa Kigamboni na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa wakati
wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri
Mkuu. Pia, niwapongeze Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za
Bunge kwa kuongoza kwa umahiri mkubwa Kamati zao wakati wa kupitia makadirio ya
sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti
ya Serikali kwa mafungu yote.
6.
Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na
Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu
Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika na Taasisi zote za
Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu.
Aidha, ninawashukuru Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya
Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka
2017/2018.
7.
Mheshimiwa Spika, kipekee, ninamshukuru Mheshimiwa Jenista
Joakim Mhagama (Mb.), Mbunge wa
Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb.), Mbunge wa
Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na
Vijana) kwa ushirikiano wao mkubwa
katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, ninamshukuru
Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya wakati akiitumikia nafasi hiyo. Ninamtakia kazi
njema kwenye jukumu lake jipya la
kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani. Vilevile, ninawashukuru wafanyakazi
wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi
H. Mwinyimvua; Bwana Eric F. Shitindi na aliyekuwa Katibu Mkuu Bwana Uledi A.
Mussa kwa ushauri wao wa kitaalam kwangu na kwa Waheshimiwa Mawaziri.
8.
Mheshimiwa
Spika, ninazishukuru pia nchi
marafiki, Taasisi na Mifuko ya Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Madhehebu
ya Dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuunga mkono jitihada za Serikali
katika kujenga uchumi wa nchi yetu.
Misaada na mikopo iliyopatikana kwa wakati imechangia kutekeleza miradi
ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
9.
Mheshimiwa
Spika, ninapenda kutumia fursa hii
kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono
na kuielewa vizuri dhamana ya Kitaifa niliyonayo ya kusimamia utendaji wa
Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Mwisho ninaishukuru familia yangu
hususan mwenza wangu mpendwa, Mary na watoto wetu kwa upendo, dua na kuendelea
kunitia moyo ili nitekeleze kwa ufanisi zaidi majukumu yangu ya Kitaifa. Asanteni
sana!
MWELEKEO WA BAJETI
10.
Mheshimiwa
Spika, ni
mwaka mmoja sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Katika kipindi hicho, yapo mambo mengi
yaliyofanyika kwa mafanikio makubwa ambayo yataanishwa kwa kina katika bajeti
za Sekta pindi Mawaziri husika watakapoziwasilisha. Baadhi ya mafanikio hayo ni
utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Elimu Bila Malipo; kuongezeka kwa uzalishaji
na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini; kuimarika uwajibikaji na nidhamu
katika Utumishi wa Umma; kuongeza ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi
ya fedha za Umma; kuboresha huduma za kiuchumi na za kijamii; na kutekeleza Awamu
ya Kwanza ya Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma. Nitumie fursa hii kuwashukuru
Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Serikali, Watumishi wa Umma na Watanzania wote
kwa ujumla kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa majukumu
yake, kwani bila ushirikiano wao, tusingeweza kupata mafanikio hayo.
11.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti ya Ofisi ya Waziri
Mkuu imeendelea kuandaliwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi ya mwaka 2015; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; ahadi za
Mheshimiwa Rais alizotoa wakati wa Kampeni, pamoja na maelekezo yake wakati
anazindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba,
2015. Bajeti hii itaendelea kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka
uliopita na kushughulikia utatuzi wa vikwazo vya kukuza uchumi kwa haraka na
baadhi ya changamoto zilizojitokeza. Aidha, Serikali itajikita zaidi katika
maeneo yatakayochangia kuimarisha uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za
jamii. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla, kuendelea
kushirikiana na Serikali katika kufikia azma hiyo ili dhamira yetu
ya kuboresha maisha ya Watanzania iweze kutimia. Ni vyema tukakumbuka kwamba
tuna mwaka mmoja tu wa utekelezaji wa yale tuliyopanga kufanya ndani ya kipindi
cha miaka mitano. Tutatumia bajeti ya mwaka ujao wa fedha kukabili changamoto
zilizojitokeza. Ahadi ya Serikali ni kuendelea kuwatumikia wananchi kwa
uadilifu na bila ubaguzi wowote, huku tukitanguliza mbele maslahi ya Taifa.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
12. Mheshimiwa
Spika, tarehe 23 Julai 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia Mkutano Mkuu Maalum
wa Chama Cha Mapinduzi, alitangaza uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za
Serikali Kuu Dodoma. Kufuatia uamuzi huo, mipango ya kuhamia Dodoma kwa awamu
ilianza baada ya mahitaji halisi yatakayoiwezesha Serikali kuhamia Dodoma
kubainishwa, ikiwa ni pamoja na ofisi na nyumba za makazi kwa viongozi na watumishi
wa umma. Awamu ya kwanza ilipangwa kuhama ifikapo mwisho wa mwezi Februari,
2017.
13.
Mheshimiwa Spika, ninafurahi
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari watumishi 2,069 wakiwemo Mawaziri,
Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, baadhi ya Wakuu wa Idara
na Vitengo na watumishi wengine wamekwishahamia Dodoma kama ilivyopangwa.
Vilevile, Wizara zote zimepata majengo ya Ofisi yatakayotumika katika kipindi
cha mpito.
14.
Mheshimiwa Spika,
ili Mji wa Dodoma uweze kuendelezwa kwa mpangilio mzuri, Serikali inaupitia upya
Mpango Kabambe wa Mji wa Dodoma. Mapitio hayo yatasaidia sana kuepuka makosa
yaliyofanyika katika miji mingi hususan ujenzi holela unaochangia katika
uchafuzi wa mazingira na kuharibu mandhari ya miji. Ni wazi kwamba, ujenzi wa
Mji wa Dodoma hautafanywa na Serikali pekee, bali tutaendelea kuhamasisha Sekta
binafsi na wadau wengine kuwekeza Dodoma. Ninalipongeza sana Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) kwa kujenga nyumba 300 za makazi hapa Dodoma ambazo watumishi
wanaweza kununua au kupangishwa. Ninatoa wito kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kuongeza kasi ya
upimaji wa viwanja, kuboresha miundombinu na kudhibiti ujenzi holela kwa kushirikiana
kwa karibu na Manispaa ya Dodoma na Taasisi nyingine za Serikali.
SIASA
15.
Mheshimiwa Spika,
mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, hali ya kisiasa nchini
imeendelea kuwa shwari na ya kuridhisha. Aidha, Chaguzi Ndogo zilifanyika
tarehe 22 Januari, 2017 katika Jimbo la Dimani - Zanzibar na Udiwani katika
kata 20 Tanzania Bara kwa kushirikisha wagombea kutoka vyama 15 vya siasa. Ninavipongeza
vyama vyote vilivyoshiriki katika chaguzi hizo, na kipekee nakipongeza Chama
cha Mapinduzi kwa ushindi wa Jimbo la Dimani na viti 19 vya udiwani katika chaguzi
hizo.
16. Mheshimiwa
Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mashauri 53
ya kupinga ushindi wa Ubunge na mashauri 194 ya kupinga ushindi wa Udiwani
yalifunguliwa. Mashauri hayo yamekwishasikilizwa na hukumu kutolewa, isipokuwa
shauri moja la kupinga matokeo ya Ubunge katika Jimbo la Mbagala. Nizipongeze Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi kubwa waliyofanya
ya kuhakikisha kesi hizo zinaendeshwa kwa kasi na kwa weledi na hivyo kuwezesha
wananchi kuendelea kupata uwakilishi.
17. Mheshimiwa
Spika, ili kuendelea kuboresha demokrasia hapa nchini,
hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na uvumilivu wa
kisiasa. Ninatoa rai kwa wadau wa siasa kote nchini kujenga utamaduni wa
masikilizano na kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa
za kuunganisha watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya
siasa za mazoea. Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu misingi ya siasa zinazolenga
kuleta ustawi wa wananchi na zinazotanguliza maslahi ya nchi na wananchi.
MUUNGANO
18. Mheshimiwa
Spika, Serikali inaendelea kudumisha muungano wetu ambao
ni tunu na mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia nzima. Wananchi wanaendelea
kunufaika na matunda ya Muungano wetu ambao ni imara na dhabiti. Serikali zote
mbili zinafanya mashauriano kupitia Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya Muungano
chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, viongozi na watendaji wa sekta nyingine zisizo
za Muungano wamekuwa wakikutana mara kwa mara ili kubadilishana uzoefu na
kubaini maeneo ya ushirikiano kwa ustawi wa wananchi wa pande zote mbili. Jumla
ya vikao 13 vya sekta ambazo siyo za Muungano vilifanyika kati ya Julai 2016 na
Machi 2017.
19.
Mheshimiwa Spika,
ninapenda kutumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendesha kwa ufanisi mkubwa
kikao kilichofanyika tarehe 13 Januari, 2017 ambapo taarifa kuhusu hoja
zilizopatiwa ufumbuzi, maagizo na maelekezo ya kufuatilia utekelezaji wa changamoto
zilizobaki ilitolewa. Serikali itaendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wetu kwa
manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
HALI YA UCHUMI
20.
Mheshimiwa Spika,
mwenendo wa viashiria vya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2016/2017
vinaonesha kuwa uchumi wetu unakua na kuimarika. Kwa mujibu wa takwimu
zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifikia
asilimia 7.0 mwaka 2016. Sekta
zilizochangia kwa kiwango kikubwa kwenye ukuaji huo ni uchimbaji madini na
mawe; usafirishaji na uhifadhi wa mizigo;
habari na mawasiliano; pamoja na shughuli za fedha na bima. Mfumuko wa Bei
uliendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja na kasi ya upandaji bei
ilipungua kutoka wastani wa asimilia
5.6 mwaka 2015 hadi asilimia 5.2 mwaka 2016. Kwa upande mwingine, tathmini ya hali ya Taasisi za
Fedha inaonesha kuwa Benki zetu ziko salama na zina mitaji na ukwasi wa
kutosha. Aidha, taarifa za Mashirika mbalimbali ya Kimataifa zinaonesha kwamba
katika mwaka 2016 uchumi wa Taifa letu ulikua vizuri na hivyo kutufanya kuwa miongoni
mwa nchi sita (6) za Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi
wake unakua kwa kasi kubwa zaidi.
21.
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka juhudi kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya
Serikali. Kutokana na juhudi hizo, makusanyo ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) yaliongezeka kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 850 kwa mwezi katika mwaka 2015/2016 hadi Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwezi katika
mwaka 2016/2017. Pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, juhudi kubwa
zimefanyika kudhibiti matumizi ya rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kuziba
mianya ya rushwa, ubadhirifu, wizi na upotevu wa fedha za umma. Mwenendo huo
umeiwezesha Serikali kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa kwa fedha za ndani na
pia utoaji huduma kwa wananchi. Serikali itaendelea kupanua wigo wa vyanzo vya
mapato ya ndani na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kila anayestahili
kulipa kodi aweze kuilipa.
22.
Mheshimiwa Spika,
kuimarika kwa viashiria vya uchumi wa nchi yetu katika kipindi cha mwaka mmoja
tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni dalili njema katika kujenga
uchumi imara na tulivu utakaotusaidia kuelekea katika Uchumi wa Viwanda na
kufikia nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Serikali itaongeza juhudi
katika kuchochea ukuaji wa sekta za kipaumbele zenye fursa kubwa ya kukuza
uchumi kwa haraka na kuondoa umaskini kama vile Kilimo na Viwanda. Pia, itahakikisha
kwamba sekta wezeshi kama vile Nishati, Habari na Mawasiliano, Fedha na ujenzi
wa miundombinu muhimu ya barabara, bandari, reli, vivuko na viwanja vya ndege zinaimarishwa.
Vilevile, Serikali itaendelea kuhimiza utekelezaji thabiti wa miradi ya
maendeleo na kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
23. Mheshimiwa
Spika,
Serikali imeendelea kuwezesha Wananchi kupitia Mipango na Programu mbalimbali
kwa kuelekeza nguvu zaidi kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Serikali imeweka mazingira bora kwa vikundi vya kiuchumi na vijana kujiunga na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, SACCOS na VICOBA. Aidha, Serikali imeanzisha
majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika mikoa yote na kufanya
mapitio ya Mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa mwaka 2007. Mapitio
hayo yana lengo la kuboresha uendeshaji na usimamizi wa Mfuko huo ili kuwezesha
wanawake wengi zaidi kukopesheka.
24.
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba asilimia 56 ya
nguvu kazi ya Taifa ni vijana. Hivyo, Serikali inatekeleza Programu ya Kukuza
Ujuzi na Stadi za Kazi ili kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi
wa viwanda pamoja na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi. Katika mwaka
2016/2017, Serikali inatoa mafunzo kwa vijana 9,120 katika fani mbalimbali zikiwemo
stadi za kushona nguo, kutengeneza bidhaa za ngozi, mafunzo ya kurasimisha
ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi na mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za
kujiajiri katika fani mbalimbali. Jumla ya vijana 1,469 wamehitimu mafunzo hayo
na kupata ajira. Vijana 7,651 waliobaki wanaendelea kupata mafunzo kupitia
viwanda vya TOOKU GARMENTS, MAZAVA FABRICS, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam
(DIT), VETA na Don Bosco. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itatoa mafunzo ya
kukuza ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana 15,350 katika fani
mbalimbali.
25.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana, imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 kwa
vikundi vya vijana 297 katika Halmashauri mbalimbali nchini. Aidha, Mamlaka za
Serikali za Mitaa kupitia mapato yake ya ndani zimetoa Shilingi bilioni 4.6
ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya vijana 2,356. Hatua hizi
zimekwenda sanjari na utengaji wa maeneo maalum yenye jumla ya ekari 85,603 kwa
ajili ya shughuli za vijana za kilimo, biashara ndogo ndogo, burudani na
michezo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kusimamia Halmashauri zote
nchini kutenga asilimia tano (5) ya mapato yao kwa ajili ya vijana na asilimia tano
(5) kwa wanawake.
Ajira na Mahusiano Mahali pa Kazi
26. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa juhudi za kukuza ajira nchini kama inavyoelekezwa
kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Hadi kufikia Machi 2017, jumla
ya ajira 418,501 zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 239,017 sawa na
asilimia 57 zimezalishwa katika sekta binafsi wakati ajira 179,484 sawa na
asilimia 43 zimezalishwa kutokana na shughuli za sekta ya umma ikiwemo miradi
ya maendeleo.
27.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 58 ya migogoro ya kikazi
inatokana na kutozingatiwa kwa taratibu za kuachisha kazi. Sekta zinazoongoza
kwa migogoro ya kazi ni usafirishaji, ujenzi, ulinzi binafsi, elimu, huduma za
hoteli na viwanda. Katika kupunguza migogoro mahali pa kazi, Serikali imefanya
kaguzi na kusimamia uundwaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi. Aidha, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi imeendelea kutimiza
wajibu wake wa kusuluhisha migogoro ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi
Februari 2017, Tume imesajili jumla ya migogoro 8,832 kati ya hiyo migogoro
3,319 sawa na asilimia 37.6 ya migogoro yote iliyosajiliwa imesuluhishwa. Kati
ya migogoro hiyo iliyosuluhishwa, migogoro 1,957 ilifikia suluhu (mediation) na
migogoro 1,362 haikufikia suluhu. Aidha, migogoro 5,513 inaendelea kusuluhishwa
katika hatua mbalimbali.
Ninatoa
wito kwa waajiri na waajiriwa wote nchini, kuzingatia Sheria za Kazi na
kuimarisha uhusiano mzuri kwenye maeneo ya kazi, ili muda mwingi zaidi utumike
kwenye uzalishaji mali badala ya kutatua migogoro. Vilevile, ni muhimu
sana kuimarisha kaguzi za kazi na kuendelea kusaini mikataba ya kuunda na
kusajili mabaraza ya wafanyakazi ili kuimarisha zaidi mahusiano mahali pa kazi.
MAENDELEO YA KISEKTA
Sekta za Uzalishaji
Viwanda
28.
Mheshimiwa
Spika, ili kujenga uchumi wa
viwanda, Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda
vidogo, vya kati na vikubwa. Viwanda vinavyopewa kipaumbele ni vile
vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu
wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa nchini na nje ya nchi. Katika
kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda,
Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na mashirika ya
umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya
NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza na kujenga
viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini. Natoa pongezi kwa
Bodi na Menejimenti ya Mifuko hiyo, kwa kuunga mkono jitihada za Serikali
katika ujenzi wa viwanda nchini. Aidha, ninaendelea kuyasisitiza mashirika ya
umma kuhakikisha kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa Mpango wa Pili
wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa viwanda.
Maliasili na Utalii
29. Mheshimiwa
Spika, sekta ya utalii ni moja kati ya sekta muhimu sana katika
uchumi wa nchi yetu. Kote ulimwenguni, mafanikio ya sekta ya utalii kwa kiasi
kikubwa hutegemea miundombinu thabiti ya utalii, huduma bora na ulinzi na
usalama. Ili kuendelea kunufaika na sekta hiyo, Serikali inaboresha miundombinu
ya utalii, kupanua wigo wa vivutio vipya vya utalii na kuimarisha huduma ya
usafiri wa anga. Vilevile, Serikali inafanya juhudi kubwa za kudhibiti ujangili
na biashara haramu ya wanyamapori ambapo watuhumiwa 897 walitiwa mbaroni na kati yao watuhumiwa 282 wamefikishwa Mahakamani.
30. Mheshimiwa
Spika, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi watalii 1,284,279 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 12 na
kuliingizia Taifa Dola za Marekani bilioni 2. Juhudi zilizoanza za kuliimarisha
shirika letu la ndege zinalenga pia kutoa mchango mkubwa kwenye sekta ya utalii
kwa kusafirisha watalii wa ndani na kutoka nje ya nchi. Shabaha yetu ni
kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea nchi yetu na pia mapato
yatokanayo na sekta hiyo. Nitumie fursa hii kuisihi sekta binafsi kuwekeza
zaidi kwenye miundombinu muhimu ya sekta hii zikiwemo hoteli, kuboresha huduma
na kubuni mbinu mpya za kuvutia watalii.
Kilimo
31.
Mheshimiwa Spika,
uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2015/2016 ikijumuisha mazao
ya nafaka na yasiyo ya nafaka ulifikia tani
16,172,841 ikilinganishwa na mahitaji ya kitaifa ya tani 13,159,326. Hivyo, katika kipindi hicho nchi ilikuwa na ziada
ya tani 3,013,515 za chakula. Katika
msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017, hali ya upatikanaji wa mvua katika Mikoa
inayopata mvua za vuli haikuwa ya kuridhisha na hivyo kusababisha ukame na
upungufu wa mavuno katika baadhi ya maeneo. Tathmini ya awali imebainisha
kwamba Halmashauri 55 zimeathirika na ukame.
32.
Mheshimiwa
Spika,
ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi
kununua mazao ya chakula kutoka katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika
maeneo yenye uhaba. Aidha, wafanyabiashara
waliokuwa wamehifadhi nafaka katika maghala, walitakiwa kuzisambaza
katika masoko ya ndani. Vilevile, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
walielekezwa kuwahamasisha na kuwaelekeza wakulima kupanda mbegu bora za mazao
ya kilimo yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa muda mfupi kwa kipindi hiki
cha mvua za masika. Ili kutoa msukumo katika kazi hiyo, kiasi cha tani 1,969 za mbegu bora za mazao
yanayostahimili ukame zilinunuliwa na Serikali na kusambazwa katika Halmashauri
zilizobainika kuathirika na ukame. Pia, wakulima wanaendelea kuhamasishwa
kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha katika msimu huu wa masika kwa kupanda mazao
hayo yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.
33.
Mheshimiwa Spika,
kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika uchumi wetu, Serikali imeweka
dhamira ya kuongeza uzalishaji, tija na kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara.
Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilifanikisha kupatikana kwa tani 277,935 za mbolea na tani 23,333 za mbegu bora. Aidha, hadi Februari
2017, Serikali ilitoa tani 30,773 za
mbolea ya ruzuku ya kukuzia na kupandia kupitia vituo vya mauzo ya mbolea vya
Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).
34. Mheshimiwa
Spika,
moja ya ahadi ya Serikali kwa wakulima wetu ni kupunguza kodi, tozo na ada
mbalimbali zinazochangia kupunguza faida kwa mkulima. Katika mwaka 2016/2017, Serikali
ilifuta baadhi ya tozo za mazao ambazo ni kero kwa wakulima katika mazao ya
pamba, chai na kahawa. Tozo zilizofutwa kwenye zao la pamba ni mchango wa Mwenge wa Shilingi 450,000 unaotolewa na kila
kiwanda cha kuchambua Pamba na ada ya vikao vya Halmashauri za Wilaya ambayo ni
shilingi 250,000. Kwa zao la chai, kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na
katika zao la kahawa, ada ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250
nayo pia imefutwa.
35. Mheshimiwa Spika,
Serikali pia imeboresha Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani kwa kuanzisha
utaratibu wa wazi wa ununuzi wa mazao kupitia minada. Mathalani, katika msimu
wa 2016/2017 kwenye zao la korosho, utaratibu huo umechangia kwa kiasi kikubwa
kuongezeka kwa bei ya korosho kwa kilo kutoka shilingi 1,200 hadi shilingi 3,800,
bei ambayo haijawahi kufikiwa katika historia ya zao la korosho nchini. Aidha,
Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani na utaratibu wa minada umeongeza ushindani
na kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hususan nchi ya Vietnam na
nchi nyingine kuja wenyewe kununua korosho badala ya kutegemea soko la India
pekee. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na uchambuzi wa kina wa
kodi, tozo na ada zilizobaki katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo
la kuziondoa au kuzipunguza ili kumwezesha mkulima, mvuvi na mfagaji anufaike
zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya Halmashauri zetu. Kwa sasa,
tunashughulikia zao la tumbaku kwa kupitia tozo zake na pia kubaini ubadhirifu
unaoendelea kwenye ushirika huo.
Mifugo
36.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza uzalishaji wa mitamba na uhimilishaji wa mifugo ili kuhamasisha ufugaji
wa kisasa na wenye tija. Mitamba 546 imezalishwa kutoka mashamba ya Serikali na
mitamba 88 kutoka NARCO na kusambazwa kwa wafugaji wadogo. Aidha, Kituo cha
Taifa cha Uhimilishaji – NAIC Usa River, Arusha kimeimarishwa na kuongeza
uzalishaji wa mbegu bora za ng’ombe hadi kufikia dozi 10,494 ikilinganishwa na dozi
8,000 zilizozalishwa na kusambazwa katika mwaka 2015/2016. Pia, ng’ombe
waliohimilishwa wameongezeka kutoka 221,390
mwaka 2015/2016 hadi ng’ombe 457,557
mwaka 2016/2017.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuimarisha kituo chetu cha
kuzalisha mitamba cha Kitulo wilayani Makete ili kukiongezea uwezo wake. Aidha,
Serikali inatoa nafasi kwa mashamba binafsi kuzalisha mitamba zaidi kama
mashamba ya ASAS kule Iringa ili wafugaji wadogo wanufaike. Serikali pia itaendelea na zoezi la kutenga,
kupima na kumilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji na kujenga miundombinu ya
mifugo kwa kuongeza idadi ya malambo na mabwawa katika mikoa. Hatua hizo
zitasaidia kupunguza uzururaji wa mifugo na migogoro baina ya wafugaji na
wakulima na hifadhi za misitu.
Madini
38. Mheshimiwa Spika, Sekta ya
madini ni muhimu kwa uchumi wetu. Serikali imetenga maeneo zaidi kwa ajili ya
wachimbaji wadogo, kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kutoa ruzuku pamoja na kuimarisha
shughuli za ugani. Katika kipindi cha mwezi
Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali imetenga maeneo 11 yenye
ukubwa wa hekta 38,567 kwa ajili ya
wachimbaji madini wadogo. Maeneo hayo ni Msasa na Matabe mkoani Geita,
Biharamulo na Kyerwa mkoani Kagera, Itigi mkoani Singida, D-Reef, Ibindi na
Kapanda Mkoani Katavi, Ngapa mkoani Ruvuma, Kitowelo na Namungo mkoani Lindi
pamoja na Nzega mkoani Tabora.
39.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
yatokanayo na rasilimali za madini na kuimarisha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini kwa
migodi mikubwa, ya kati na midogo. Aidha, Serikali itaendeleza
wachimbaji wadogo na wa kati wa madini pamoja na kuhamasisha shughuli za
uongezaji thamani wa madini hayo.
Huduma za Kiuchumi
Ardhi
40.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
2016/2017, Serikali iliahidi
kuanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi. Ninapenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi ya ujenzi wa mfumo huo awamu ya kwanza
ilizinduliwa rasmi Agosti, 2016 na Mkandarasi tayari ameanza kazi. Sambamba na
zoezi hilo, Serikali inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Taarifa za
Ardhi. Kukamilika kwa mradi huo kutaboresha utendaji kazi, kuharakisha huduma
za utoaji hati miliki, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha utunzaji wa
kumbukumbu za ardhi ambapo nyaraka zote za ardhi zitakuwa katika mfumo
unganishi wa kielektroniki.
41.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia iliidhinisha
ramani za upimaji zenye jumla ya viwanja 78,771 na mashamba 239. Aidha, Serikali imekamilisha upigaji wa picha za anga za
Jiji la Dar es Salaam na inaendelea kutatua migogoro ya
matumizi ya ardhi baina ya wakulima,
wafugaji na hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini.
42. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kujenga
Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi na kuboresha usimamizi wa
sekta ya ardhi kwa kufanya mapitio ya Sera na Sheria za Ardhi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sera, sheria,
kanuni na miongozo ya ardhi ili kudhibiti viashiria vya migogoro ya matumizi ya
ardhi nchini. Ninatoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashughulikia
migogoro ya ardhi mapema na kuweka mazingira wezeshi ya upimaji wa ardhi katika
Halmashauri zao.
Umeme
43.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imechukua
hatua thabiti za kuongeza uzalishaji, kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na
kuongeza kasi ya usambazaji umeme. Katika mwaka 2016, umeme uliozalishwa na kuingizwa
katika Gridi ya Taifa uliongezeka na kufikia Gigawatt hours (GWh) 7,092 ikilinganishwa
na Gigawatt hours (GWh) 6,227 zilizozalishwa
mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia
13.9. Vilevile, Serikali imepanua na
kuboresha njia za usafirishaji umeme kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme wa
msongo wa kilovolti 400 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme kutoka Iringa –
Dodoma – Singida – Shinyanga.
44.
Mheshimiwa
Spika, Serikali iliendelea
kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017, Wakala
ulikamilisha ujenzi wa vituo
sita (6) vya kuongeza nguvu ya umeme kutoka msongo wa kilovolti 11 hadi kilovolti
33 katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru; ujenzi wa
njia za kusambaza umeme zenye urefu wa kilometa
17,740 za msongo wa kilovolti 33;
ujenzi wa vituo vidogo vya kupoza na kusambaza umeme 4,100; na ujenzi wa njia ndogo ya usambazaji umeme wenye urefu wa kilometa 10,970.
45.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2017/2018, Serikali itaongeza uzalishaji,
kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme
nchini. Aidha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Ujenzi wa
Bomba la Mafuta kutoka Kabaale (Uganda) hadi Tanga (Tanzania). Serikali pia,
itawezesha uwekaji wa mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwenye viwanda na
matumizi ya majumbani pamoja na uendelezaji wa mradi wa kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas - LNG) mkoani
Lindi.
Barabara
46. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali imejenga
na kukarabati jumla ya kilometa 430
za barabara kuu sawa na asilimia
62
ya lengo la kilometa 692. Aidha, ujenzi wa
barabara za juu kwenye makutano ya TAZARA unaendelea
vizuri pamoja na maandalizi ya kuitisha zabuni za ujenzi wa Daraja Jipya la
Selander na ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze kwa kiwango cha Expressway. Vilevile, ujenzi wa barabara
za juu (Interchange) kwenye makutano
ya Barabara ya Ubungo ulizinduliwa rasmi tarehe 20 Machi, 2017. Hizi ni hatua
muhimu za kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya msongamano wa magari katika
Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015.
Vivuko na Usafiri Majini
47.
Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha
2016/2017, Serikali ilipanga kujenga kivuko kipya cha Pangani (MV Pangani) na
kukarabati kile cha Magogoni – Kigamboni. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu
kwamba hadi kufikia Februari, 2017 ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo ulikuwa
umekamilika. Aidha, ununuzi wa boti ndogo za abiria kwa ajili ya vivuko vya
Kilambo – Namoto (Mtwara), Mkongo – Utete (Pwani), Pangani – Bweni (Tanga) na
Msemo – Msangamkuu (Mtwara) utakamilika katika mwaka huu wa fedha. Kwa upande
wa huduma za usafiri kwenye maziwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa meli moja
katika Ziwa Victoria, meli mbili katika Ziwa Nyasa zitakazofanya safari kati ya
Kyela na Mbambabay pamoja na ukarabati wa meli za MV Victoria na Butiama (Ziwa
Victoria) na MV Liemba (Ziwa Tanganyika).
Bandari
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inatekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Bandari nchini kwa kufanya upanuzi na
kuimarisha miundombinu ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Mifumo ya Ulinzi katika bandari hizo imeimarishwa na mashine za kisasa za
kukagua mizigo zimefungwa. Kutokana na jitihada hizo, tumeanza kuona mwelekeo
mzuri wa kuimarika ufanisi wa kiutendaji hususan katika Bandari ya Dar es
Salaam. Tutaendelea kufanya maboresho zaidi ili Bandari ya Dar es Salaam iwe
chaguo namba moja katika usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi yetu.
Reli
49.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya uboreshaji wa
miundombinu ya Reli ya Kati ili kuongeza uwezo wa reli hiyo kutoa huduma za
uchukuzi nchini na nchi jirani zinazotumia bandari zetu. Awamu ya kwanza ya
ujenzi wa reli mpya ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa kiwango cha standard gauge imeanza kutekelezwa kwa
kusaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha reli ya Dar es Salaam - Morogoro (kilometa 205). Taratibu za kuwapata
makandarasi wa ujenzi wa reli kutoka Morogoro – Makutupora (kilometa 336), Makutupora- Tabora (kilometa 294), Tabora- Isaka (kilometa 133) na Isaka- Mwanza (kilometa
254) zinaendelea.
Usafiri wa anga
50. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali imetekeleza kwa dhati azma ya kuimarisha Kampuni ya
Ndege Tanzania (ATCL). Katika kipindi hicho, ndege mbili (2) aina ya Dash 8 –
Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zilinunuliwa na kuanza kutoa
huduma mwezi Oktoba, 2016. Aidha, mwishoni mwa mwaka 2016, Serikali iliingia
mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine nne (4). Kati ya hizo, ndege moja ya aina
ya Dash 8 - Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 inatarajiwa kuwasili mwezi
Julai, 2017. Ndege nyingine mbili (2) aina ya CS300 zenye uwezo wa kubeba
abiria 127 kila moja zinatarajiwa kuwasili mwezi Juni, 2018 na ndege kubwa moja
ya masafa marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262
inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2018.
51. Mheshimiwa Spika, kukamilika
kwa ununuzi wa ndege hizi kutaisaidia ATCL kuongeza safari za ndani na nje ya
nchi na hivyo kuchangia katika jitihada za kuongeza watalii wanaokuja nchini
kutembelea vivutio vyetu na kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini. Aidha, ATCL
imeanzisha safari za kuja Dodoma na hivyo kuongeza uhakika wa usafiri wakati
huu ambapo Serikali inahamia Dodoma. Wigo wa upanuzi kwa viwanja vyote nchini
unaendelea na sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege.
Mawasiliano
52. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi
zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kutekeleza
Mradi wa Anuani za Makazi na Postikadi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji
wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na
huduma za kibenki. Aidha, Sekta ya Mawasiliano inatekeleza Programu ya
Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school),
Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na
ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika Mikoa 26 na Taasisi za Serikali.
53.
Mheshimiwa Spika, Serikali
pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mawasiliano Vijijini kwa
kushirikiana na Kampuni ya Viettel ya Vietnam.
Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu
2015-2017. Viettel wamekwishafikisha
miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417, Ofisi za
Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya
131 na Ofisi za Posta 68.
54. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha
kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government
Data Centre). Lengo ni kuongeza na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa
unaoenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika
kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Pamoja na ujenzi wa vituo hivyo, matumizi
ya TEHAMA yameongezeka na hivyo kuziwezesha taasisi za Serikali kutoa mchango
mkubwa kwenye uboreshaji na utoaji wa huduma, kuongeza mapato na kuokoa gharama
mbalimbali.
Sekta ya Huduma za Jamii
Elimu
55. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa walimu wa
shule za msingi kwa kuwapa mafunzo hasa katika ufundishaji wa stadi za Kusoma,
Kuandika na Kuhesabu (KKK). Jumla ya walimu 22,995 wa shule za msingi na walimu
519 wanaofundisha elimu maalum kwa wanafunzi wasioona na wenye ulemavu wa kusikia
wamepewa mafunzo hayo. Lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayemaliza darasa
la saba anajua kusoma na kuandika.
56.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2016/2017, Serikali iliendelea na mpango wa kutoa Elimumsingi bila
malipo. Tangu utekelezaji wa mpango huo uanze, Serikali imekuwa ikipeleka
wastani wa Shilingi bilioni 18.77 kila
mwezi, ambapo shule za msingi 16,088 na shule za sekondari 3,602 zimenufaika na
mpango huo. Mpango huo umeleta manufaa kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini
na cha kati na umeongeza uandikishaji wa wanafunzi kwenye shule za Msingi na
Sekondari. Kufuatia ongezeko hilo, tulijikuta tukilazimika kupambana na upungufu
wa madawati, jambo ambalo liliifanya Serikali ianzishe kampeni maalum ya kumtoa
sakafuni mtoto wa Kitanzania. Hivi sasa madawati sio tatizo tena kwenye shule
nyingi nchini. Nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa Watanzania wote
walioshirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya upungufu wa madawati. Natoa pongezi kwa taasisi binafsi, watu
binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao yote.
57. Mheshimiwa Spika, uchumi wa viwanda
kwa kiasi kikubwa unahitaji rasilimaliwatu yenye weledi hasa katika masomo ya
hisabati na sayansi. Kama zilivyo nchi nyingine Barani Afrika, Tanzania
inakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kutopenda kusoma masomo ya hisabati na
sayansi na hivyo kuchangia katika ufaulu duni kwenye masomo hayo. Ni dhahiri
kuwa watoto wetu wasipoweka bidii katika masomo ya hisabati na sayansi viwanda
vyetu vitalazimika kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi jambo litakalowafanya
Watanzania kuwa watazamaji.
58. Mheshimiwa Spika,
ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imefanya juhudi za kuhamasisha
wanafunzi kupenda masomo ya sayansi katika ngazi zote za shule. Aidha, Serikali
inaendelea na Mpango wa Ujenzi wa Maabara katika shule za sekondari na vyuo
vikuu pamoja na ununuzi wa vifaa. Katika mwaka 2016/2017, Serikali imenunua
vifaa vya maabara kwa ajili ya shule 1,625
za sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara na usambazaji wa vifaa umeanza mwezi
Machi, 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa mwezi Aprili, 2017 kwa nchi nzima. Aidha, Serikali
inatoa mafunzo kwa walimu 5,920 wanaosoma
Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA.
59. Mheshimiwa
Spika, Serikali inakusudia kuimarisha ufundishaji wa
masomo ya TEHAMA kwa shule za Sekondari. Serikali inaendelea na mpango wake wa
kujenga maabara za kompyuta ili wanafunzi wawe na uelewa wa TEHAMA. Utekelezaji
wake utafanyika hatua kwa hatua.
60.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imetoa vibali vya ajira kwa walimu wa Hisabati na Sayansi 4,129.
Natoa wito kwa wazazi wenzangu kuhamasisha watoto wetu kupenda masomo ya Hisabati
na Sayansi. Naagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na
TAMISEMI na wadau wengine waandae Mkakati Maalum wa kuhamasisha na kuwavutia
wanafunzi kusoma masomo ya Hisabati na Sayansi. Mkakati huo pia uwezeshe
upatikanaji wa walimu watakaofundisha masomo ya Hisabati na Sayansi katika
shule za msingi na sekondari kwa kipindi kifupi bila kuathiri ubora wa
ufundishaji.
61.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu Kishiriki cha
Mkwawa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam. Ujenzi wa majengo 20 ya mabweni
ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 umekamilika. Vilevile, Serikali inaimarisha
miundombinu katika vyuo vya ufundi vya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam,
Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya na Chuo cha Ufundi Arusha kwa lengo la
kuimarisha mafunzo ya Ufundi na Sayansi nchini. Katika mwaka 2017/2018,
Serikali itaimarisha Vyuo vya Elimu ya Juu ili kuwezesha upatikanaji wa wataalam
mahiri katika nyanja mbalimbali hususan Sayansi na Teknolojia.
Maji
62. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kusogeza huduma za maji karibu zaidi na
wananchi ili wasitumie muda mwingi kutafuta maji badala yake wajikite katika
shughuli za uzalishaji mali. Ili kutimiza azma hiyo, Serikali inatekeleza
miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini ikiwemo miradi ya vijiji 10 chini
ya Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kati ya mwezi Julai na Desemba 2016, miradi 90 ya maji vijijini ilikamilika na
kufanya idadi ya miradi iliyokamilika kufikia 1,301 kati ya miradi 1,810 iliyolengwa. Miradi 509 iliyobaki ipo katika hatua
mbalimbali za utekelezaji na yote inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni,
2017.
63.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini katika
Halmashauri zote nchini ukiwemo mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe
unaolenga kuhudumia wananchi zaidi ya
456,000 katika vijiji 38 kwenye
miji ya Same, Mwanga na Korogwe Vijijini. Ili utoaji wa huduma ya maji uwe
endelevu, wananchi waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya
maji, uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya maji. Nitumie fursa hii
kuwakumbusha watendaji katika Halmashauri zote kusimamia kikamilifu sheria
inayokataza shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji.
Afya
64.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa ikiwemo kuhimiza
lishe bora. Aidha, Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa
kujenga vituo vya kutolea huduma za afya na tiba pamoja na kuboresha
upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka
kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka
2015/2016 hadi Shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Vilevile, Serikali
imeanzisha utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa
wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama. Serikali pia imeanzisha maduka ya
dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu kwa wananchi katika hospitali za mikoa
ambapo hadi sasa maduka manane (8) yameanzishwa, na ujenzi wa maduka mengine
katika mikoa iliyobakia unaendelea.
65.
Mheshimiwa Spika,
Serikali pia inaimarisha huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto nchini kwa kutekeleza
Mpango Mkakati wa Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto wa
mwaka 2016-2020. Lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 50 ya
vituo vya Afya nchini vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kwa matatizo
ya uzazi ikiwemo upasuaji na huduma za watoto wachanga. Hadi sasa, vituo vya afya 159 vinatoa huduma
za upasuaji ambapo vituo 106 ni vya Serikali.
Vilevile,
Serikali imeimarisha utoaji wa huduma za kinga na hivyo kuchangia kutokomezwa
kwa ugonjwa wa Polio hapa nchini na hatimaye nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi
zilizopatiwa hati ya kutokomeza ugonjwa huo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali
itaendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa
Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi na kuimarisha huduma za kinga ili
kupunguza vifo vya watoto na akina mama pamoja na makundi mengine. Naomba nitoe wito kwa wote Watanzania
wajiunge kwa wingi na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili Serikali iweze
kuwachangia kupitia mfumo huo.
BUNGE
66.
Mheshimiwa
Spika, Ofisi ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Katika mwaka 2016/2017, Ofisi ya Bunge iliratibu na kusimamia shughuli za Mikutano mitatu ya Bunge ambapo maswali 1,054 ya kawaida, nyongeza na
ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa. Miswada kumi (10) ya Sheria ilijadiliwa na kupitishwa na Bunge.
Aidha, Bunge liliratibu na kusimamia shughuli za Mikutano ya Kamati za Kudumu
za Bunge, kutoa huduma za Hansard, utafiti, utawala na kutoa mafunzo kwa
Waheshimiwa Wabunge na Watumishi wa Ofisi ya Bunge. Ofisi ya Bunge pia ilisimamia
kazi ya ukarabati wa jengo la Bunge pamoja na kuratibu ujenzi wa Ofisi za
Waheshimiwa Wabunge. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuliwezesha
Bunge kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba kama kawaida.
MAHAKAMA
67. Mheshimiwa Spika, utendaji wa mhimili wa Mahakama nchini
umezidi kuimarika. Katika mwaka 2016/2017, Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 279,331 kati ya 335,962 katika ngazi zote za Mahakama
sawa na asilimia 83.1 ya mashauri
yote. Pamoja na kazi kubwa ya kusikiliza mashauri, Mahakama imesogeza huduma
zake karibu na wananchi kwa kukamilisha ukarabati na ujenzi wa majengo ya
Mahakama Kuu katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. Pia, kazi za ukarabati wa
Mahakama Kuu katika Mkoa wa Mbeya inaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na
Mahakama ya Mwanzo Kibaha Mkoa wa Pwani umekamilika na kuzinduliwa.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba, katika mwaka
2017/2018, Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili
kupunguza mlundikano wa mashauri yaliyopo mahakamani. Hata hivyo, ili Mahakama
ifanye kazi zake vizuri, shughuli za upelelezi wa kesi na uendeshaji wa
mashtaka zinatakiwa pia kuimarishwa zaidi. Serikali itafanya kila liwezekanalo
kuimarisha taasisi zote zinazohusika katika mlolongo wa utoaji haki ili
wananchi wapate haki zao kwa wakati.
MASUALA MTAMBUKA
Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali
68.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliahidi kuanzisha
Mfumo wa Wazi wa Kielektroniki wa kufuatilia uwajibikaji na utendaji Serikalini.
Mfumo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za Serikali kwa
kuwawezesha Viongozi kutoa maelekezo na kufuatilia utekelezaji wake. Aidha,
Mfumo huo utasaidia ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi,
Ahadi na Maagizo ya Mheshimiwa Rais na Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Napenda
kulialifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mfumo huo umekamilika, kuzinduliwa rasmi na
mafunzo kutolewa kwa wataalamu katika Wizara zote. Mfumo huo pamoja na mambo
mengine utaongeza kasi ya utoaji taarifa za utekelezaji wa kazi za Serikali kwa
wakati na pia kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma. Wizara na Taasisi
zote za Serikali zinatakiwa kuutumia Mfumo huo kikamilifu ili kurahisisha
ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Serikali na kusaidia viongozi kutatua
vikwazo pale vinapojitokeza.
Vita dhidi ya Rushwa
69.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa. Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu Serikali ya Awamu ya
Tano ilipoingia madarakani Novemba, 2015 zimetambulika hata na Mashirika ya Kimataifa
yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa Duniani. Taarifa ya
Shirika la Transparency International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka 2016 imeonesha kuwa
viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini.
70. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2016/2017, Serikali kupitia
TAKUKURU imefanya uchunguzi wa
majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini
kuendelea na mashtaka kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU
iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa
walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407
zinaendelea kusikilizwa mahakamani. Kutokana na operesheni zilizofanywa na
TAKUKURU, kiasi cha Shilingi bilioni
9.75 ziliokolewa. Katika Mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na mapambano
yake dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, kudhibiti
matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya fedha za ushirika na
kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Vita dhidi ya UKIMWI
71.
Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi ya UKIMWI yamekuwa yakitegemea kwa
kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo. Ninapenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ulioanzishwa na
Serikali miaka miwili iliyopita, ulizinduliwa tarehe 01 Desemba, 2016 ambapo
kupitia harambee iliyofanyika kwa ajili ya kuchangia Mfuko huo, shilingi
milioni 347 zilipatikana kama ahadi. Vilevile, Serikali imetenga kiasi cha shilingi
bilioni 5.6 kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI.
72.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
inaendelea kutoa huduma kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) ambapo
hadi Desemba, 2016 WAVIU 839,574 sawa na asilimia 63 ya WAVIU wote, walikuwa
wamepatiwa dawa. Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuwahamasisha WAVIU
kujitokeza na kuingia kwenye Mpango wa Tiba ya Kufubaza Athari za UKIMWI. Aidha,
Serikali imekamilisha uandaaji wa miongozo minne ya
Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ikijumuisha Mpango Kazi wa Kinga, Mkakati wa Kondomu,
Mkakati wa Uwekezaji na Mpango kazi wa jinsia.
73.
Mheshimiwa
Spika, Serikali katika mwaka
2017/2018, itaimarisha uratibu wa afua za UKIMWI kwa wadau wote wa sekta ya
umma na binafsi na kupitia mifumo ya uratibu iliyoanzishwa. Serikali kwa
kushirikiana na wadau pia itazijengea uwezo Kamati zilizo katika ngazi ya jamii
hususan vijiji na kata ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kupunguza
na kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia mfumo ulio katika jamii. Vilevile,
Serikali itakamilisha utafiti wa nne wa kubainisha viwango vya maambukizo ya
UKIMWI nchini na kuboresha ushiriki wa sekta binafsi ili kuleta ufanisi katika
kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya UKIMWI.
Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
74. Mheshimiwa
Spika,
katika 2016/2017, Serikali imeendelea kutoa huduma pamoja na kuongeza
upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika kutimiza azma hiyo,
Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye
Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji. Aidha,
Serikali imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi
ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera,
Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na kampeni hiyo itaendelea nchi
nzima.
75.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inahakikisha
kwamba watumiaji wa lugha ya alama wanapata haki ya kupata habari na vituo
vyote vya televisheni vimeelekezwa kutumia wakalimani wa lugha ya alama. Napenda
kuvikumbusha Vituo vya Televisheni kuweka wakalimani wa lugha katika vituo
vyao. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye
ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni
na vifaa vya kufundishia.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
76. Mheshimiwa
spika,
dawa za kulevya zinaathiri maisha ya vijana wetu wengi na hivyo kuzima ndoto za
maisha yao na kupunguza nguvu kazi ya Taifa. Ili kupambana na janga hilo,
katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho ya Sheria ya
Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Marekebisho hayo
yameipa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nguvu ya kukamata,
kupeleleza na kushitaki watuhumiwa wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya.
Aidha, hivi karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi
wa Watendaji Wakuu watakaosimamia Mamlaka hiyo.
77. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Januari, 2017
watuhumiwa 11,303 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya katika sehemu mbalimbali
nchini. Kati ya watuhumiwa hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo
9,174 wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa
kesi zao unaendelea. Pia alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu,
jumla ya watuhumiwa 79 wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea. Ni imani yangu kuwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa
za Kulevya itaendeleza kwa kasi zaidi juhudi za kupambana na uingizaji, uzalishaji,
usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini. Watanzania wana imani
kubwa na Mamlaka hii na ninaomba wote tuipe ushirikiano wakati wote kwani vita
hii ni kubwa na ni ya Kitaifa! Aidha, nawasihi wazazi wenzangu, tuwe karibu na
vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili wasiingie kwenye mtego huu wa dawa za
kulevya.
Uratibu wa Maafa
78.
Mheshimiwa Spika, Serikali wakati wote inahakikisha kuwa nchi ipo
katika hali ya utayari wa kukabiliana na maafa na pia kutoa misaada ya kibinadamu ikiwemo huduma za
matibabu, ushauri wa kisaikolojia, na vifaa pale maafa yanapotokea. Serikali
imejenga vituo vipya 20 vya upimaji wa hali ya hewa katika Halmashauri 11 za Tarime, Nyamagana, Muleba, Longido, Geita,
Maswa, Kigoma, Sikonge, Kongwa, Serengeti, na Kahama. Kuwepo kwa vituo hivyo kutaongeza
ufanisi
katika upatikanaji wa taarifa za tahadhari hasa kwa majanga ya mafuriko na
ukame.
79.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia tetemeko la
ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa mwezi Septemba 2016, Serikali
kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua za kushughulikia athari zilizotokana na
tetemeko hilo. Huduma za afya na tiba na za kibinadamu za chakula na malazi zilitolewa
kwa walioathirika. Vilevile, Serikali ilirejesha hali ya miundombinu
iliyobomoka, yakiwemo majengo ya Serikali na Taasisi za Umma 686, Kituo cha
wazee Kilima pamoja na kutoa maturubai 6,237, mahema 367, mabati 7,300 na mifuko
ya saruji 1,825 kwa walioathirika. Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule za
Ihungo, Nyakato na Omumwani pamoja na ukarabati wa Kituo cha afya Kabyaile
Ishozi. Ninapenda kuwashukuru sana wananchi wote na wadau waliotoa michango yao
kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.
HABARI NA MICHEZO
Habari
80.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Huduma
za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 ambayo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi na
uwajibikaji katika Sekta ya Habari nchini. Kanuni za Sheria hiyo zimeandaliwa
na tayari zimeanza kutumika. Natoa wito kwa wadau wa sekta ya habari kuzingatia
sheria na kanuni hizo ili kuimarisha weledi katika tasnia ya habari. Aidha,
nashauri wadau wa habari kujikita zaidi katika kuandika na kutangaza habari za
masuala ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi kutekeleza azma ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za
kijamii.
Maendeleo ya Michezo
81.
Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona dalili nzuri za kuimarika kwa
shughuli za michezo hapa nchini. Mathalan, timu ya Mpira wa Miguu ya Serengeti Boys imefuzu kushiriki Mashindano
ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka
17 yatakayofanyika Gabon, Mei 2017. Napenda nimshukuru sana Makamu wa Rais,
Mama Samia Suluhu Hassan ambaye amewaaga na kuwakabidhi bendera ya Taifa tayari
kwenda kushiriki vita hiyo. Nawaomba Watanzania wote tuungane pamoja kuiombea
na kuiunga mkono timu yetu kwa michango ya hali na mali ili kuiwezesha
kushiriki kikamilifu. Kwa upande wa riadha, Mtanzania
mwenzetu Alphonce Simbu alipata medali katika mbio za marathon huko Mumbai
nchini India. Aidha, mwezi Septemba 2016, Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya
Wanawake Tanzania (Twiga Stars) iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutwaa
taji la CECAFA. Ninatoa pongezi kwa wale wote walioliletea Taifa sifa kupitia
michezo. Naziombea dua ili ziweze kushiriki michuano ya kimataifa.
82.
Mheshimiwa
Spika, michezo ni sekta muhimu
katika kuongeza ajira, kuimarisha afya, kukuza uchumi, kuimarisha umoja wa
Kitaifa na kuitangaza nchi Kimataifa. Nchi nyingi zilizofanikiwa kimichezo
ziliwekeza zaidi kujenga vipaji vya vijana katika michezo. Natoa wito kwa TFF ihakikishe
kuwa vijana wa Timu ya Serengeti Boys wanawekewa Mpango Endelevu wa Kukuza
Vipaji Vyao na kutunzwa vyema ili waweze kuiwakilisha nchi yetu katika
mashindano mengine ya kimataifa. Aidha, vyama vingine vya michezo vitoe msukumo
mkubwa kwenye kuwekeza zaidi kwa vijana wa shule za msingi na sekondari kwani
hao ndio watakuwa wawakilishi wetu katika miaka ijayo. Na mwaka huu, michezo ya
shule za msingi na sekondari itarejea na kufanyika mkoani Mwanza kama
ilivyotangazwa mwaka jana. Nazisihi wizara husika za TAMISEMI na Wizara ya
Elimu zianze maandalizi mapema na kuandaa mpango huo na kutoa taarifa timu hizo
ziweze kujiandaa na kushindana ili tupate wachezaji imara wa kushiriki michuano
hiyo.
ULINZI NA USALAMA
83. Mheshimiwa
Spika,
hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kutokana na kazi kubwa na nzuri
inayofanywa na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama katika kulinda mipaka ya nchi
yetu. Serikali imeendelea kuimarisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa
kulipatia zana na vifaa vya kivita na kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa
nyumba 6,064 za makazi ya askari ulioanza mwaka 2013/2014. Kwa upande mwingine,
Serikali kupitia Jeshi la Magereza inakamilisha ujenzi wa nyumba zilizojengwa
kwa njia ya ubunifu katika baadhi ya Magereza ikiwemo ujenzi unaoendelea katika
Gereza la Ukonga wa ghorofa 12 zenye uwezo wa kuishi askari na familia 320.
84. Mheshimiwa
Spika, Serikali itaendelea kuimarisha usalama wa raia na
mali zao kwa kufanya operesheni za
kuzuia uhalifu nchini, kufanya upelelezi wa kesi kwa kasi ili kupunguza
mlundikano wa kesi zilizopo mahakamani,
na kusimamia sheria za barabarani ili kupunguza ajali zinazoleta madhara
kwa wananchi. Aidha, Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa askari na maafisa wa
jeshi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kupambana na vitendo vya
rushwa na kupambana na biashara ya dawa za kulevya.
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
85.
Mheshimiwa Spika, kudumisha uhusiano mzuri na mataifa mengine
duniani pamoja na mashirika ya kimataifa ni moja kati ya Misingi ya Sera yetu
ya Mambo ya Nje. Tumeendelea kuimarisha ujirani mwema baina yetu na nchi
jirani, nchi marafiki pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa, jitihada
ambazo zimetuwezesha kuvutia mitaji mikubwa ya uwekezaji, utalii pamoja na
kupanua fursa za kibiashara. Katika mwaka 2016/2017, Serikali imefungua Balozi mpya sita (6) katika nchi za Algeria, Israel, Korea
Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Balozi hizo zina kazi kubwa ya kuendeleza
juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na
rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo
ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo. Serikali itaendelea kulinda na kutetea
maslahi ya Tanzania nje ya nchi na kuweka mikakati ya kunufaika na nafasi ya
nchi yetu kihistoria. Hivyo, ninatoa
wito kwa mabalozi wetu wote waendelee kuitangaza nchi yetu kama eneo mwafaka
lenye fursa nyingi za utalii, uwekezaji na biashara.
HITIMISHO
86. Mheshimiwa
Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda tunahitaji nidhamu
ya kazi, ubunifu, elimu na matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia. Vilevile,
tunahitaji kuimarisha sekta binafsi, miundombinu ya huduma za kiuchumi na jamii
na kuondoa urasimu usio wa lazima. Nafarijika kwamba misingi tunayoendelea kujenga
katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuzaa matunda kama nilivyoeleza awali. Ili
kufanya mafanikio hayo yawe endelevu, naomba nihitimishe hotuba yangu kwa
kusisitiza mambo makuu yafuatayo:-
(i)
Mosi,
ustawi wa nchi yetu na mafanikio ya mipango yetu ya maendeleo vinategemea amani
na utulivu. Hivyo, kila mmoja wetu aweke nadhiri ya kuendelea kuilinda na
kuienzi amani ya nchi yetu ili mipango yetu iweze kufanikiwa. Tunalo jukumu la
kuhimiza amani ili tufanye kazi zetu kwenye mazingira ya amani na utulivu.
(ii)
Pili,
jukumu la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu wa
kila mwananchi. Njia pekee ya kuijenga nchi yetu ni kufanya kazi kwa bidii,
kulipa kodi kwa hiari na kufichua wakwepa kodi wote na wala rushwa.
(iii)
Tatu,
ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji wananchi wenye afya njema na maarifa ya
kufanya kazi na ubunifu. Tujenge
utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa
yasiyo ya kuambukiza ambayo yanapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa;
(iv)
Nne,
rasilimali tulizonazo ipo siku zitaisha. Hivyo ni
wajibu wa kila mmoja wetu kuzitumia kwa uangalifu ili zitufae sisi na vizazi
vijavyo. Tuepuke matumizi mabaya ya
rasilimali zetu kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe kizazi hiki na
vizazi vijavyo;
(v)
Tano,
tuongeze nidhamu na uwajibikaji katika kila jambo la maendeleo tunalolifanya na
kuzingatia matumizi ya muda. Tamaduni na mila zinazohamasisha uvivu na uzembe
ni lazima tuzipige vita kwa nguvu zetu zote; na
(vi)
Mwisho,
dawa za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna kwa
kasi nguvukazi ya nchi yetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita hii
kwa kufichua mtandao wa wahusika wa dawa za kulevya. Ahadi
yetu ni kuwapa ushirikiano na kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2017/2018
87.
Mheshimiwa
Spika, kwa
mwaka 2017/2018, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba
Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Sabini na Moja; Milioni Mia Sita Sitini na Nne, na Hamsini na
Tano Elfu (Sh.171,664,055,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na
Nne, Milioni Mia Sita Arobaini na Tatu, na Mia Tatu Thelathini na Tisa Elfu
(Sh.74,643,339,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Tisini na Saba, Milioni
Ishirini, na Mia Saba na Kumi na Sita Elfu (Sh.97,020,716,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
Vilevile, ninaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Moja,
Milioni Mia sita Hamsini na Mbili na Mia Mbili Sitini na Mbili Elfu (Sh.121,652,262,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha
hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na
Nne, Milioni Mia Nne Hamsini na Mbili, na Mia Mbili Sitini na Mbili Elfu
(Sh.114,452,262,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Saba na Milioni Mia Mbili
(Sh.7,200,000,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
88.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
COMMENTS