LICHA ya kukabiliwa na matatizo mbalimbali katika sekta ya afya ikiwemo uhaba wa dawa na wafanyakazi, Halmashauri ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani imefanikiwa kudhibiti vifo vya wajawazito vinavyotokana na matatizo ya uzazi.
Wilaya ya Mafia ambayo ni kisiwa, kilichopo umbali wa kilometa 131 au maili 81Kusini mwa Dar es Salaam, imefanikiwa kudhibiti vifo hivyo kutokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na idara ya afya.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Dk. Joseph Mziba anaitaja mikakati hiyo ni pamoja na kuhakikisha wajawazito wote ambao ni mara yao ya kwanza kubeba mimba wanajifungulia hospitalini badala ya zahanati.
Anasema wengine ni wajawazito ambao wameshazaa zaidi ya mara nne wakipata mimba nao hutakiwa kujifungulia katika hospitali ya wilaya.
“Tulikuwa na tatizo la vifo vya wajawazito vilivyokuwa vinasababishwa na matatizo ya uzazi mwaka 2015 wajawazito nane wamekufa na kabla ya hapo wajawazito 12 wamekufa mwaka 2014, hivyo tukaweka mkakati,” anasema Dk. Mziba.
Anasema mkakati huo unahusisha ufuatiliaji wa wajawazito wanaofika kliniki ambapo anayeonekana na matatizo hushauriwa kwenda hospitali ya wilaya badala ya zahanati, aliyezidiwa ambulance huitwa kumchukua na kumpeleka hospitali ya wilaya.
Kauli yake inaungwa mkono na Mganga wa hospitali ya wilaya Dk. Abdallah Bhai ambaye anasema ili kufanikisha mkakati huo wameimarisha mfumo wa mawasiliano baina ya zahanati na hospitali ya wilaya.
Dk. Bhai anasema endapo zahanati itampokea mjamzito anayejifungua kwa mara ya kwanza ana aliyezaa zaiidi ya mara nne wanawasiliana na hospitali ya wilaya ambayo hutuma gari ya wagonjwa kwenda kumchukua na kumpeleka hospitali ya wilaya.
“Tuna ambulance moja, inazunguka wilaya nzima iwe mchana au usiku, haturuhusu mjamzito mwenye matatizo kubaki zahanati, wote wanaletwa hospitali ya wilaya,” anasema.
Mganga Mfawidhi huyo anasema mkakati huo umesaidia kupunguza vifo vya wajawazito ambapo tangu 2016 hadi mwezi Machi mwaka huu (2017) hakuna mjamzito hata mmoja aliyekufa kutokana na matatizo ya uzazi,” anasema.
Dk.Bahi anafafanua kuwa, “Pamoja na tatizo la watumishi wakiwemo wauguzi, lakini nusu ya watumishi tulionao wote tumewaelekeza katika wodi ya wazazi.
Mkazi wa Bondeni kisiwani humo Sharifa Abdu anasema mpango huo umeleta nafuu kwa wajawazito ingawa wananchi wengine hasa wale wanaoishi mbali wanaulalamikia, huku akiitaka halmashauri hiyo kulipatia ufumbuzi tatizo la dawa.
“Wajawazito wenye matatizo kwa kweli hawakai zahanati wanaletwa hospitali ya wilaya, ingawa wananchi wanaotoka mbali wanaona utaratibu huo unawatesa kwa kuwa wanatumia gharama kufika mjini kumuona mgonjwa wao, lakini serikali pia imalize tatizo la dawa na wafanyakazi,” anasema Sharifa.
Kisiwa cha Mafia ni moja ya wilaya za mkoa wa Pwani ina kata nane, tarafa mbili, vijiji 23, vitongoji 139, watu 46,438 kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inakabiliwa na tatizo kubwa la dawa na watumishi.
Katibu wa afya wa halmashauri hiyo Dk. Omari Kambangwa anakiri kuwepo kwa tatizo la dawa na kwamba linasababishwa na bajeti finyu kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Anasema wilaya hiyo inahitaji zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka kwa ajili ya dawa na vifaa tiba lakini inayopatikana ni milioni 196 au chini ya hapo.
Kwa upande wa wafanyakazi Dk. Kambangwa anasema wilaya hiyo inahitaji watumishi wa kada mbalimbali za afya 489, waliopo sasa ni 186 tu.
Source: Said Mmanga


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO