LEO Watanzania wanasherehekea miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanya kuwapo kwa Tanzania.
Sherehe hizo zinafanyika huku muungano huo ukizidi kuimarika kutokana na vikwazo vilivyouteteresha katika siku za karibuni kupunguzwa.
Juhudi zilizofanywa na uvumilivu kwa muda umefanya Muungano huu kuwa wa aina yake duniani, hasa ikizingatiwa kwamba umewezesha wananchi wa pande zote mbili kuwa na fursa za kijamii na kiuchumi.
Hayo yamewezekana kutokana na kujengeka kwa tabia za kuangalia kinachotuuma na kukifanyia kazi.
Sisi kwa upande wetu tunapongeza juhudi zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kero za Muungano.
Kutokana na juhudi hizo, kero hizo sasa zimebakia tatu kati ya 15, zilizokuwa zikisumbua mawazo ya Watanzania.
Kufanikiwa kuondolewa kwa kero hizo kumeleta mwanga mkubwa kwa wananchi wanaopenda kuendelea kuwapo kwa uhusiano na pigo kwa wapinzani wa Muungano ambao kila kukicha wanapanga ajenda za kuwatenganisha wananchi wa Bara na Visiwani.
Vikwazo vilivyovukwa na Kamati ya pamoja ya kushughulikia kero na masuala ya muungano yenye wajumbe kutoka Serikali zote mbili  chini ya Makamu wa Rais , Samia Suluhu Hassan imewakata kiburi wapinzani ambao walikuwa kama fisi anayefuata mkono  akidhani kwamba utaanguka ili aule.
Huku kamati ya kupambana na vikwazo vya Muungano ikiwa katika hatua za mwisho za kutatua kero zilizobaki kwa lengo la kuimarisha Muungano; ufumbuzi wa kero 12  kati ya 15 ni kielelezo tosha cha kuonesha dunia kwamba hakuna kisichowezekana katika utekelezaji wa mambo yanayogusa maisha ya wananchi.
Ni dhahiri kwamba zipo kasoro ndogo ndogo ndani ya muundo wa Muungano, lakini ukiangalia vyema utabaini kwamba kasoro hizo haziwezi kutusababisha kuachana.
Tunasema hivyo, kwa kuwa kero ambazo hadi leo bado zinazungumzwa za vyombo vya usafiri wa moto kutoa huduma ya usafiri au kutumika pande zote mbili ni ndogo sana, kwani hiyo inahitaji mabadiliko ya kisheria inayogusa usafiri barabarani. Na hili haliwezi kutushinda.
Na kero nyingine ya suala la Hisa za Zanzibar za iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, ambayo Zanzibar alikuwa ni mjumbe wake  mpaka ilipokufa na hisa zake kuhamishiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tunaamini wakati wowote linapatiwa ufumbuzi kwa kuwa nyaraka zipo.

Hakika Watanzania wana haki ya kujivunia uwezo wa kuzungumza na kukubaliana katika mambo ya msingi na hivyo kuendelea kuuneemesha Muungano huu ambao wengine hawaupendi, kwa sababu binafsi na uroho unaoambatana na uchoyo wa nafsi.
Tunachotaka kusema ni kwamba wakati wananchi wanaendelea kufurahia undugu wetu, viongozi wetu wanapaswa kuendelea na mazungumzo ili mambo yaliyobaki yakitatiza yaweze kuondolewa.
Ni dhahiri Watanzania kwa sasa wanajivunia maamuzi yenye hekima yaliyofanywa na waasisi wa Muungano wa  serikali mbili,  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume ambayo yaliwezesha kufungwa kwa mkataba wa Muungano  Aprili 22, 1964 na kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi  Aprili 26,1964.
Majivuno hayo ya kiungwana yanatokana na faida kubwa zilizopatikana kwa kipindi cha miaka 53 ya Muungano ambayo ni kuimarika kwa sekta za ulinzi, elimu, fursa za kiuchumi na kibiashara, miundombinu ya majini, nchi kavu na anga pamoja na ustawi wa kijamii.
Source:Habarileo

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO