CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetoa tamko la kulaani kile inachodai ni upotoshaji unaofanywa na Maalim Seif Sharif Hamad  na kutaka aieleze  ukweli jamii ipate kuelewa kinachoendelea ndani ya Chama hicho.

Pia kimesema kina imani na Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai kuwa atafuata sheria na kanuni za uchaguzi kwa kutambua CUF ni moja na haina vipande vipande katika suala la wagombea wa Chama hicho wa Bunge la Afrika Mashariki.

Kaimu Katibu Mkuu (CUF) Magdalena Sakaya alisema hayo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa ambapo alikuwa ameongozana na wabunge wa chama hicho.

Alisema ni vyema Maalim Seif aeleze jamii ukweli kinachoendelea ndani ya CUF  juu ya mambo muhimu kama  kukaimiwa kwa nafasi ya Katibu Mkuu, Bodi ya Wadhamini na Kesi  nne  ambazo wamezifungua na genge lake.

“Anachofanya Maalim Seif na genge lake ni kuwatoa Wanacuf kwenye hoja za Kikatiba katika kushughulikia Mgogoro wa Uongozi ndani ya CUF” alisema.

Kuhusu suala la kukaimiwa kwa nafasi ya Katibu Mkuu, Sakaya alisema hilo  ni suala la kikatiba na sio utashi wake au wafuasi wake.

“Ibara ya 93 kifungu cha 2 kinampa madaraka Naibu Katibu Mkuu anayetokea upande wa pili wa Muungano tofauti na upande anao tokea Katibu Mkuu kukaimu nafasi na kufanya kutekeleza majukumu ya Katibu Mkuu mpaka pale Katibu Mkuu atakapokua tayari kutekeleza majukumu
yake” alisema.

Alisema anachopaswa kufanya Maalim Seif ni kusema kwamba kifungu hicho hakipo au hakisemi hivyo ili Jamii ipate kuelewa na sio kubadilisha Maneno.

“Kweli CUF tumeandika barua kumjulisha Msajili kuhusu suala hilo na Msajili amejibu  na kukiri kupokea barua na ameridhia kwa mujibu wa Katiba yetu” alisema,

Sakaya alisema Profesa  Lipumba na Maalim Seif hakuna Hata Mmoja Miongoni Mwao mwenye uwezo wa kumsimamisha mwenzie au kuteua mtu wa kukaimu nafasi ya mwenzie.

Alisema hata suala la Maalim Seif kuomba kusajili Bodi mpya, na Nakala ya Maombi hayo kuyawasilisha Ofisi ya Msajili, hicho nacho ni kichekesho kama sio kujichanganya.

Alisema Maalim Seif na genge lake wamefungua kesi Mahakama Kuu ya kutotambua Msimamo na ushauri wa Msajili kuhusu uliokua Mgogoro wa Uongozi ndani ya CUF na inaitaka Mahakama Kuu itamke kuwa Msajili hana haki ya kuingilia mambo ya ndani ya CUF.

“Swali kwa Maalim Seif na genge lake, je wanapopeleka nakala ya maombi ya kusajiliwa Bodi yao Ofisi ya Msajili huko sio kuingilia mambo ya ndani ya Vikao vya Chama ? Au ndio kusema kwamba sasa Seif na genge lake wameamua kumtambua Msajili kwa nyuma ya pazia?" alihoji.

Sakaya alisema lingekua jambo jema kama Maalim Seif angekiri wazi wazi kuwa ni kweli CUF haina Bodi halali kama ambavyo amesema Msajili kuwa Bodi ya Wadhamini ya CUF ni mfu na haipo Kisheria,  na ndio maana sasa ana hangaika kusajili Bodi mpya.

“Hivi Maalim Seif anaweza kuieleza Jamii na Wanacuf kwa ujumla kuwa zile kesi nne zilizopo mahakamani zimefunguliwa na bodi ipi ikiwa hivi sasa yeye ndio anaomba kusajili bodi mpya ? Au ndio kusema ameamua kufuta Kesi zote zilizopo Mahakamani Kimya Kimya ? “ alihoji Sakaya.

Alisema ingekuwa vyema ikiwa maombi yake ya kufungua bodi mpya yatakubalika  na bodi ipi sasa itasimia kesi zilizopo mahakamani Kati ya Bodi hizo mbili.

Alisema Maalim Seif hajui atendalo kwa sasa vyema amuache na Kamati mpya ya Utendaji wasimamie shughuli za Chama ikiwemo ya kuwafanyia kampeni na kuwaombea Kura wagombea wa bunge la Afrika Mashariki.

Aliwataja wagombea Ubunge wa bunge la Afrika Mashariki ni Habib Mnyaa,Thomas Malima na Sonia Magogo

Alisema wanaamini Spika atatenda haki katika suala la wagpmbea ubunge wa bunge  Afrika Mashariki kwa kuamini CUF ni moja na haiku vipande vipande.
source:
Sifa Lubasi, Dodoma

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO