*Zimo hospitali za wilaya 74, Ofisi za Halmashauri 123, polisi wilaya 131 na Posta 68 *Asema Serikali haina mzaha na rushwa; *Awat...
*Zimo hospitali za wilaya 74,
Ofisi za Halmashauri 123, polisi wilaya 131 na Posta 68
*Asema Serikali haina mzaha na
rushwa; *Awataka mabalozi watangaze fursa za utalii, biashara na
uwekezaji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa
kushirikiana na kampuni ya Viettel ya Vietnam inatekeleza mradi wa ujenzi wa
miundombinu ya mawasiliano vijijini ambao umefanikisha kuweka miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye
shule 417 hapa nchini.
Amesema mradi huo ambao unatekelezwa kwa kipindi
cha miaka mitatu kuanzia 2015-2017, umewezesha pia ofisi za Halmashauri
za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi
za Posta 68 kufikiwa na mtandao huo.
Waziri Mkuu ametoa kauli
hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji
wa kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa
mwaka 2017/2018 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya
Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake ukiwemo Mfuko wa Bunge kwa mwaka
2017/2018
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2016/2017, baadhi
ya kazi zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na ujenzi wa Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano; Mradi wa Anuani za Makazi na Postikodi; na kuanzisha
huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji wa huduma
muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na huduma za
kibenki.
“Sekta ya mawasiliano inatekeleza Programu ya
Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school),
Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na
ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika mikoa 26 na taasisi za Serikali,” amesema.
Amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha
kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centre) ambacho
lengo lake ni kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na
uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake
ya kila siku.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu
amesema Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga
viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kujenga uchumi wa viwanda, na kwamba
inatoa kipaumbele kwenye viwanda vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana
hapa nchini, vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye
soko hapa nchini na nje ya nchi.
“Katika kuhakikisha Watanzania
wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha zaidi
sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na mashirika ya umma kujenga viwanda.
Jitihada hizo zimewezesha mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF,
PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27
katika maeneo mbalimbali nchini,” amesisitiza.
Ameyataka mashirika ya umma
yahakikishe kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa viwanda.
Akizungumzia kuhusu juhudi za
Serikali kupambana na rushwa, Waziri Mkuu amesema Serikali inapambana
na rushwa kwa nguvu
zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya
rushwa.
“Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu
Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba, 2015 zimetambuliwa na
mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa
duniani. Taarifa ya Shirika la Transparency
International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka
2016, imeonesha kuwa viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini,”
amesema.
Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu amesema katika
mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali iliweza kuokoa kiasi
cha shilingi bilioni 9.75 kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU,
“TAKUKURU imefanya uchunguzi
wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka
Nchini kuendelea na mashtaka kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU
iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa
walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407
zinaendelea kusikilizwa mahakamani,” amesema.
Amesema katika mwaka
ujao wa fedha, Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya rushwa hususan katika
eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya fedha za umma,
malipo hewa, matumizi mabaya ya fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na
ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Wakati huohuo,
Waziri Mkuu amesema Serikali imefungua balozi mpya sita katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini,
Sudan, Qatar na Uturuki. Amesema Balozi hizo zina kazi ya kuendeleza juhudi
za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na rasilimali
zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo ikizingatiwa utulivu
na amani iliyopo nchini.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA,
ALHAMISI, APRILI 4, 2017.
COMMENTS