JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

TAMKO LA MHE. UMMY  A. MWALIMU (MB) - WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MALARIA DUNIANI -
TAREHE 25 APRILI, 2017

Ndugu Wananchi,
Siku ya Malaria Duniani, huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 mwezi Aprili. Maadhimisho haya yaliridhiwa katika Mkutano wa 60 wa Afya Duniani (World Health Assembly) huko Geneva nchini Uswisi.  

Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuielimisha na kuikumbusha jamii ili kutambua athari za ugonjwa wa malaria, jinsi unavyoambukizwa, na namna ya kujikinga. Aidha maadhimisho haya pia hutumika kuihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua dalili za malaria mapema; kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya ili kupima na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya malaria kabla ya kuanza kutumia dawa, kutumia dawa sahihi ya kutibu malaria pale itakapothibitika kuwa na vimelea vya malaria na kukamilisha matibabu ya malaria kulingana na maelekezo ya mtoa huduma. Kauli Mbiu ya mwaka huu inasema Shiriki Kutokomeza Malaria Kabisa, kwa Manufaa ya Jamii”.

Ndugu Wananchi,
Takwimu kutoka katika vituo vya kutolea huduma za Afya zinaonesha kuwa, takribani wastani wa  watu million  12 huripotiwa kuwa na ugonjwa wa malaria katika vituo vya kutolea huduma za Afya  kwa mwaka.

Aidha Takwimu za viashiria vya malaria kutoka tafiti zilizofanyika katika kaya zimeonesha kuwa maambukizi ya malaria yalikuwa asilimia 18 mwaka 2008, aslimia 10 mwaka 2012 na asilimia 14.8 kwa mwaka 2015.
Utafiti wa mwaka 2015-2016 unaonesha mikoa mitatu ya; Kagera, Geita na Kigoma ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria, (Kagera 41%, Geita 38% na Kigoma 38%). Makundi yanayoathirika zaidi na malaria ni wajawazito na watoto umri chini ya miaka mitano.

Mikakati inayopendekezwa kimataifa ambayo inatekelezwa na Wizara yangu kwa kushirikiana na  wadau wetu ni pamoja na:

 1. Udhibiti wa mbu waenezao malaria; Udhibiti hufanyika kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu (LLINs); unyunyiziaji wa viuatilifu ukoko katika kuta ndani ya nyumba (IRS); kusafisha mazingira na kuua viluwiluwi vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia (LSM) hasa katika maeneo ya mjini.

 1. Uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa malaria; Kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ugonjwa wa malaria kwa kutumia kipimo mRDT au hadubini, na kutumia dawa mseto pale mgonjwa anapogundulika kuwa ana vimelea vya malaria; kuwapatia wajawazito vyandarua vyenye viuatilifu na dawa ya Sulphadoxine Pyrimethamine (SP) kwa vipindi maalumu wakati wa ujauzito ili kuwakinga na madhara yanayotokana na malaria.

Ndugu Wananchi,
Nchi yetu imepata mafanikio makubwa ambayo yametokana na utekelezaji wa mikakati na afua za kupambana na ugonjwa wa malaria na ushiriki wa wadau mbalimbali. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na:
 • Kukamilika kwa kampeni: Kampeni ya ugawaji wa Vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu (LLINs) katika kaya bila malipo katika mikoa 23 nchini, ambapo jumla ya vyandarua zaidi ya millioni 27 vimegawiwa kwa jamii bila malipo. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anatumia chandarua kujikinga na ugonjwa huu. Mikoa mitatu ya; Mtwara, Lindi na Ruvuma inapata vyandarua kupitia Mpango wa wanafunzi shuleni unaojulikana kama School Net Program (SNP) toka mwaka 2013.

Chandarua Kliniki: Ili kuhakikisha upatikanaji wa vyandarua unakuwa endelevu hususan kwa makundi yanayopata athari zaidi kwa ugonjwa wa malaria (Wajawazito na Watoto), utaratibu endelevu unaojulikana kama CHANDARUA KLINIKI umeanzishwa ambapo wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja hupewa chandarua wanapohudhuria kliniki kwa huduma mbalimbali. Hadi sasa utaratibu huo unatekelezwa katika Mikoa saba (9) ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Simiyu na Kigoma.

Ugawaji vyandarua kupitia Shuleni:
Mpango mwingine ni wa ugawaji wa vyandarua kupitia wanafunzi shuleni,  ambapo wanafunzi wanapata chandarua kila mwaka, kama njia ya kufikisha chandarua hicho kwa matumizi ya familia. Mpango huu wa vyandarua shuleni unatekelezwa katika mikoa saba (7) ya; Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mwanza, Geita, Kagera na Mara kupitia ufadhili wa PMI.

Upuliziaji viatilifu Ukoko (IRS):
Utekelezaji wa mkakati wa upuliziaji viuatilifu-ukoko katika kuta ndani ya nyumba, unatekelezwa katika Halmashauri za mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye maambukizi makubwa ya malaria. Ambapo kwa mwaka huu, zoezi la upuliziaji limefanyika katika mikoa 4 na Halmashauri 10 za Sengerema, Buchosa na Kwimba (Mwanza); Chato na Nyang’wale (Geita) Ngara, Misenyi na Bukoba (V) (Kagera); Musoma (V) na Butiama (Mara). Jumla ya nyumba 487,553 zimepuliziwa viuatilifu-ukoko na takriban wakazi 2,437,760 wamekingwa dhidi ya malaria katika maeneo hayo.

Tiba Sahihi ya Malaria:
Tiba sahihi kwa wagonjwa wa malaria imeendelea kutolewa katika vituo vya kutolea huduma za Afya, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vipimo vya kutambua uwepo wa vimelea vya malaria kwa kutumia hadubini au mRDTs  vinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya wakati wote. Aidha, inasisitizwa kuwa dawa zinatolewa kwa wale tu ambao watathibitika kuwa na vimelea vya malaria (confirmed cases).

Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa wataalamu wanajengewa uwezo kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ili kufanya kazi kwa ufanisi na weledi. Kwa kupitia juhudi hizi, kumekuwepo na ongezeko la upimaji kufikia asilimia 90 katika vituo hivyo; zaidi ya lengo ambalo Wizara ilijiwekea la asilimia 80.

Kwa upande wa dawa za malaria zimeendelea kupatikana katika vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za afya.  Dawa katika Sekta Binafsi:
Upatikanaji wa Dawa Mseto za malaria kwa bei punguzo kupitia sekta binafsi kupitia mpango  wa  Dawa Mseto kwa bei Punguzo (Co- payment mechanism for subsidized ACTs in the private sector) ambao unajumuisha vituo vya kutolea huduma za afya vya binafsi na maduka ya dawa. Mpango huu, unalenga kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi atakayekosa dawa za malaria pale anapougua na kuamua kwenda kutibiwa katika vituo vya serikali au binafsi.

Viuadudu vya Kibailojia (Larvicides):
Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya (LABIOFAM) kutoka nchini Cuba, imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha viuadudu (biolarvicides) ambavyo vitatumika kuua viluwiluwi vya mbu katika mazalia (madimbwi, mabwawa na sehemu nyingine zinazozalisha mbu). Tayari kiwanda kimeanza uzalishaji wa viuadudu, hivyo natoa wito kwa Halmashauri kutenga bajeti ya kununua viuadudu  hivyo kwa ajili ya utekelezaji wa afua ya kuangamiza viluwiluwi vya mbu kwenye mazalia.

Changamoto:
Pamoja na mafanikio kadhaa yaliyopatikana, bado tuna changamoto katika maeneo yafuatayo:
 • Wanajamii kutotumia vyandarua ipasavyo wakati wote katika kujikinga na ugonjwa wa malaria pamoja na mitazamo potofu juu vyandarua;
 • Hamasa ndogo ya Jamii kupima kabla ya kutumia dawa na kukubali matokeo ya vipimo. Hii huchangia katika matumizi yasiyo sahihi ya dawa za malaria na hivyo kuchangia katika usugu  wa vimelea dhidi ya dawa.
 • Jamii kutoshiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuharibu mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi, kusafisha mifereji, kuweka mazingira safi na kuharibu mazalia ya mbu kwa kuondoa maji yaliyotuama.
 • Changamoto kubwa ni upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kuendeleza mafanikio  tuliyoyapata. Kwa mfano misaada iliyokuwa ikitolewa katika nchi za Afrika imepungua kwa kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.6 kwa mwaka, Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo.
Ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto zilizopo, Wizara yangu inahakikisha inaendelea kutekeleza ipasavyo mikakati iliyopo ya kupamabana na ugonjwa wa malaria kwa kushirikiana na wadau.

Ujumbe Muhimu kwa jamii
Niwakumbushe kuwa Ugonjwa wa malaria bado ni hatari kwa uhai wetu, maendeleo na ustawi wa Taifa letu. Wakati tunaadhimisha siku ya malaria Duniani, napenda kusisitiza yafuatayo:
 • Wanajamii kushiriki kikamilifu katika kutekeleza na kutumia afua zote za kupambana na malaria.
 • Kila mwanafamilia alale kwenye chandarua chenye viuatilifu kila siku ili kujikinga na malaria. Ni kosa kutumia vyandarua kwa matumizi yasiyo sahihi mf. Kuvulia samaki, kufugia kuku na kuzungushia bustani.
 • Wanajamii kushiriki katika kuharibu mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi, kusafisha mifereji, kuweka mazingira safi na na kuondoa maji yaliyotuama.
 • Kila mwanafamilia  mwenye dalili za malaria ahakikishe anawahi kwenye kituo cha kutolea huduma na kupimwa kabla ya kutumia dawa, na endapo atagundulika kuwa na vimelea ahakikishe anatumia dawa kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.
 • Wajawazito kuhakikisha wanahudhuria Kliniki mapema ili kupata huduma zote muhumu ikiwemo kupata tiba ya tahadhari kwa vipindi kwa kutumia SP.
·         Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga bajeti ya kununua viuadudu  hivyo kwa ajili ya utekelezaji wa afua ya kuangamiza viluwiluwi vya mbu kwenye mazalia katika Halmashauri zao.

Msisitizo wa Wizara ya Afya, ni kwa wananchi na wadau wote kuendelea kuona umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria hususan kwa kutumia fursa zilizopo, kuwekeza katika mapambano dhidi ya malaria na kutekeleza ipasavyo mikakati niliyoitaja hapo juu.Shukrani:
Napenda nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali, kutoa shukrani zangu za dhati kwa wadau wetu wote waliochangia katika mafanikio tuliyofikia wakiwemo; Mfuko wa Dunia wa kushughulikia ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (The Global Fund), Mfuko wa Rais wa Marekani unaoshughulikia Malaria (PMI), Shirika la Misaada la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la UNITAID, Taasisi zisizo za Kiserikali, Sekta binafsi kupitia Mpango wa Malaria Safe Initiative, Taasisi za Utafiti (NIMR na Ifakara Health Institute) nikitaja kwa uchache; na bila kuwasahau ninyi wanahabari, wananchi na jamii kwa ujumla kwa kuwa tayari kutumia mikakati hiyo kwa kushirikiana na Serikali.

Nimalizie kwa kusisitiza kwamba iwapo tutaitekeleza ipasavyo mikakati niliyoitaja hapo juu, nina imani kabisa, tunaweza kujikinga na ugonjwa wa malaria  na hatimae kuufanya ugonjwa wa malaria kuwa si tatizo kubwa tena katika jamii yetu.

Mwisho kabisa niwakumbushe kuwa zama zimebadilika “Sio kila homa ni Malaria nenda ukapime”, na “lala kwenye chandarua chenye viuatilifu kila siku” ili kujikinga na malaria.   

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO