Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga maeneo ya uwekezaji mjini Dodoma kwa ajili ya kujenga viwanda, mahoteli makubwa, nyumba za makazi na huduma muhimu za kijamii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) Mhandisi Paskas Muragili amesema kuwa maeneo hayo ni Njedengwa, hekta 580 ambapo miundombinu muhimu imewekwa  ikiwemo maji, umeme na barabara ya lami ili kurahisisha uwekezaji, eneo la  Iyumbu hekta 78 na Western Industrial Area hekta 334.6 (WIA).
Mhandisi  Muragili  ameongeza CDA  imetenga hekta 14,700 eneo la  Kikombo, Chigongwe hekta 6, 278,   Nyankali  hekta 2,495 na  Mtumba hekta 8,000, kwa ajili ya kujenga mji wa  Serikali ambapo kutajengwa Wizara  mbalimbali, Idara za Serikali, Taasisi, na mashirika yatakayowekeza Dodoma.
Vilevile, eneo hilo litajengwa makazi ya watumishi wa Umma na huduma mbalimbali za kijamii kama masoko, zahanati, hoteli, maduka na nyumba za kuabudia kulingana na imani zao.
Akikaribisha wawekezaji kuwekeza Dodoma, Muragili  amewahasisha Watanzania na wasio watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kujenga  hoteli za kitalii za nyota tano na zile za kawaida, kwa kuwa mji unategemea kupata wageni wengi siku za usoni.
“Nawakaribisha wawekezaji wa ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, bila wasiwasi niwahakikishie ardhi  iliyopo Dodoma  inatosha  kwa uzalishaji  mkubwa  wa malighafi mbalimbali zitakazohitajika viwandani”.
“Aidha, Mkoa huu upo katikati ya Tanzania hivyo malighafi  yoyote itakayohitajika ni rahisi kufika Dodoma ambayo imeunganishwa kila kona na barabara za lami,” alisema Muragili.
Pia mikoa inayoizunguka Dodoma ikiwemo Manyara, Singida, Iringa na Morogoro inaweza kunufaika kwa wepesi zaidi na fursa hizo.
Akiwatoa hofu wakazi  wa Dodoma  Muragili  amesema; “Ardhi  itauzwa kwa bei ya kawaida ili wananchi  waweze kumiliki  viwanja”. 
Ameyasema hayo akijibu hoja za waandishi wa habari kuhusu kauli za wananchi kudai bei ya viwanja itapanda, kutokana na ujio wa Makao Makuu ya Serikali, ambapo wananchi wa kipato cha chini hawataweza kumiliki viwanja hivyo.
Muragili alisisitiza kuwa viwanja havitapandishwa bei  kwani  kwa sasa CDA inauza mita moja ya mraba ya kiwanja cha makazi Shilingi  5,500 hadi 10,000 za fedha ya Tanzania, katika maeneo ambayo kitaalamu tunayaita “medium density”. 
Aidha, alisema kuwa viwanja kwa ajili ya uwekezaji mkubwa mita moja ya mraba ni Shilingi 13,300  fedha ya Tanzania, maeneo hayo kitaalamu yanaitwa “low density”.
Mhandisi Paskasi Muragili ametoa angalizo kwa wanaohitaji kununua viwanja mjini Dodoma ya kwamba anayetaka kiwanja lazima afike na kufuata taratibu za  ofisi za CDA kwa kuwa ndiko viwanja vinakopatikana. “
“Tusinunue viwanja kienyeji, mwisho wa yote utakuwa umedanganywa na madalali ambao kisheria ardhi ya mji wa Dodoma iko chini ya CDA na haihitaji dalali ila ufuate taratibu zilizowekwa”, alisema Muragiri.
Alimalizia kwa kusema “Kwa wale wanaohitaji ardhi nje ya Dodoma kama Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Kondoa, Chemba  na Chamwino wahakikishe wanawasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili wapate taratibu rasmi za ununuzi wa ardhi.
Mapaka sasa eneo la WIA lina viwanda kama Machinjio ya kisasa Dodoma na viwanda vya magodoro QFL na Dodoma Halisi.
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ni miongoni mwa Mamlaka zilizopata ufadhili wa kutekeleza mradi wa Uboreshaji Miji Kimkakati unaofadhiliwa na Mkopo wa Benki ya Dunia na msaada kutoka Serikali ya Denmark.
Aidha, tamko la serikali la mwaka 1973 lenye tangazo namba 230 la tarehe 12 Oktoba 1973 ndio liilianzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma  kama mji mkuu wa Serikali ulipewa  majukumu makuu 8. 
Kutokana na wimbi la mataifa ya Afrika kubadili miji mikuu, liliingia pia hapa nchini, na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Tanzania, ambaye ni miongoni mwa wana watiifu wa Afrika alionyesha dhamira hiyo “kuhamia’ Dodoma kama njia ya kuunga mkono.
Historia ya kuhamisha miji mikuu ilitokea miaka ya 1970 nchi nyingi za kiafrika zilibadili miji mikuu ya serikali. Mathalani Malawi ambayo ilibadilisha mji mkuu kutoka Blantyre  kwenda jiji la Lilongwe,na Nigeria ilihama kutoka Lagos kwenda Abuja.
Hoja kubwa iliyopelekea Mwalimu Nyerere kuchagua  mkoa huo ni kwamba Dodoma ni katikati mwa Tanzania, hivyo itarahisisha kuleta maendeleo katika mikoa yote kwa urahisi hususan utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi.
Hiyo ndio hoja ya msingi iliyomsukuma Mwalimu Nyerere kutoa maamuzi hayo ambapo alikuwa na uhakika iko siku dhana yake itatimia, Hongera Rais Dkt. John Pombe Mangufuli kwa jitihada zako za kutimiza ndoto za Muasisi wa taifa hili, sote tunaziona juhudi zako na Watanzania wanakuunga mkono, Hapa Kazi Tu”.
Source: Judith Mhina - MAELEZO
Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO