MBUNGE wa Malindi, Ali Saleh (CUF) ameishauri Serikali ikubali ripoti
ya Haki za Binadamu ijadiliwe bungeni ili wabunge waweze kujua mambo
yanayotokea nchini ikiwemo vitendo vya utesaji.

Saleh aliyasema hayo alipokuwa anauliza swali la ngonyeza kwa Waziri
wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, akisema kumekuwa na
vitendo vya utesaji na vimekuwa vikitajwa sana, lakini sasa mfumo
uliopo hauruhusu ripoti ya Haki za Binadamu kujadiliwa bungeni.

“Kwa maana hiyo, hatuna uelewa wa pamoja na mkubwa wa kujua kiasi gani
madhara ya haki za binadamu na zinavyokiukwa, je kwa weledi wako huoni
ni wakati wa kuishauri Serikali ili wabunge wajue yanayotokea katika
nchi yao,” alihoji mbunge huyo ambaye pia kitaaluma ni mwanahabari.

Alisema Mahakama zitakuwa na nguvu zaidi kukabiliana na vitendo hivyo
kama Tanzania itaridhia mikataba ya Kimataifa.

“Kuna mkataba muhimu wa kukabiliana na vitendo vya utekaji mpaka leo
Serikali ni kama inasuasua kujiunga, ni lini serikali itaridhia
mkataba huo muhimu ili Mahakama zipate nguvu zaidi ya kushughulikia
masuala haya,”alihoji Saleh.

Akijibu maswali hayo, Profesa Kabudi, alisema Katiba ya Tanzania
inakataza vitendo vyovyote vya kumtesa, kumtweza au kumdhalilisha mtu.

“Katiba imeweka wazi na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Mbushu
Mnyaroje dhidi ya serikali ambapo Mahakama ya rufaa ilieleza kwamba
vitendo vyovyote vinavyomtesa mtu, kumtweza na kumdhalilisha
havikubaliki na Katiba,”alisema.

Alieleza kuwa Mahakama ya rufaa ilikwenda mbele zaidi na kutumia
mikataba ya Kimataifa, ile ambayo Tanzania imeridhia na ile ambayo
haikuridhiwa kama msaada kwao wa kutafsiri maana ya neno au maneno
utesaji, udhalilishaji na utwezaji.

Alisema mkataba dhidi ya utesaji ambao tayari misingi yake ipo ndani
ya Katiba ya Tanzania na tayari mahakama ya rufani ambayo ni ya mwisho
imeyakubali, yanafikiriwa ili kwa wakati mwafaka, jambo hilo
lifanyike.

Kuhusu ripoti ya haki za binadamu kuletwa bungeni, alisema amelipokea
suala hilo na atalifanyia kazi kulingana na taratibu zilizopo mara
baada ya kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri.

“Nimeyapokea na nitauliza kwa jinsi gani yanafikishwa maana yake hata
kikao kimoja cha Baraza la Mawaziri bado sijakaa ili kujua utaratibu
wa kuyafikisha kujadiliwa ili nikiongozwa njia basi nitajua jinsi ya
kwenda nalo,” alisema Waziri huyo aliyeteuliwa kuwa mbunge hivi
karibuni na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria,
akichukua nafasi ya Dk Harrison Mwakyembe aliyehamishiwa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Profesa Kabudi alisema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na ya Zanzibar
inakataza vitendo vya utesaji watu kwa kuwa vinakiuka matakwa ya
Katiba.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Bumbwini, Muhamed Amour Muhammed
(CUF) katika alitaka kujua kama Serikali haioni kuwa wananchi wanaweza
kukosa imani na serikali kutokana na vitendo vya uvunjifu wa haki nza
binadamu vinavyojitokeza mara kwa mara.

Naye Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) akiuliza swali la
nyongeza, alitaka kujua kama serikali ipo tayari Wizara zinazohusu
Sheria na Mambo ya Ndani kupiga marufuku na kuchukua hatua dhahiri na
za wazi kwa polisi wanaoidhalilisha serikali kwa kuwaumiza raia kwa
kipigo.

“Baadhi ya askari polisi wanashindwa kutumia sheria inayowaelekeza
namna ya kukamata watuhumiwa na mara nyingi sana polisi wamekuwa
wakiwahukumu watuhumiwa kwa kipigo kikali sana kabla hawajafikishwa
mahakamani,”alisema Selasini.

Akijibu swali hilo, Profesa Kabudi alisema kuna umuhimu wa Wizara hizo
kukaa chini na kupitia mambo hayo na kwamba Polisi wamepewa mafunzo
juu ya haki za binadamu na jinsi ya kutumia mamlaka waliyonayo ya
kukamata watu na kuzuia uhalifu kwa namna ya kuheshimu Katiba na
Sheria

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO