WAKAZI watatu wa kijiji cha Magila wilayani Korogwe akiwemo mama na watoto wawili wamekufa papo hapo na wengine tisa wamejeruhiwa vibaya mwilini baada ya makazi yao kusombwa na mawe na maji ya mvua yaliyotoka katika milima ya Usambara Magharibi.

Maji hayo ambayo si mafuriko inadaiwa yametokana na mvua ya masika inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoani Tanga yalizingira kwa kasi kijiji hicho mapema jana (juzi) na kuharibu kabisa mazao, samani na vitu mbalimbali yakiwemo makazi ya kaya 17 za kijiji hicho.

Waliokufa ni Hapiness Mvita (24), ambaye ni mama na mwanae aitwae Prisca Lugila (4) pamoja na mtu mwingine mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana haraka.

Akizungumza katika mahojiano kwa njia ya simu, Mkuu wa wilaya ya Korogwe Robert Gabriel alisema ni mapema sana kwa uongozi wa wilaya kutangaza thamani halisi ya athari ya Mali zilizoharibiwa.

"Kilichotokea hapo kijijini Magila kata ya Mkumbara niseme tu kwamba si mafuriko bali ni kutokana na asili ya eneo hilo kuzungukwa na milima ya usambara iliyoko katika baadhi ya maeneo ya wilaya za Korogwe na Lushoto ambapo mikondo ya asili inayopitisha maji ya mvua kutoka juu milimani ilizidiwa nguvu na kusababisha kuzuka mikondo mingine mipya ambayo iliongeza kiasi cha Maji kielekea bondeni kilipo kijiji hicho," alisema.

" Maji hayo ambayo yalikuwa yakitiririka kwa kasi kutoka juu milimani yalikusanya miti na mawe makubwa kuelekea huko Magila na kusababisha maafa hayo, lakini kwa maeneo ya vijiji vya juu mlimani havikuathiriwa na hali hiyo," alisema Dc huyo.

Akizungumzia majeruhi tisa ambao kati yao nane ni wanawake na mwanaume mmoja alisema hawakuvunjika bali wamepata michubuko na maumivu makali katika maeneo tofauti mwilini.

" Hawa majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya wilaya ya Korogwe, Magunga na tayari wamepatiwa huduma na afya zao zinaendelea kuimarika vizuri," alisema.

Mkuu huyo alisema tayari serikali ya wilayani humo imeanzisha kambi maalum ya kupokea waathitika wa maafa hayo katika kijiji cha Kwenangu Mkumbara ambapo tayari kaya tatu zenye wakazi saba zimepokelewa na kupatiwa huduma muhimu ikiwemo chakula, mavazi na malazi.

Hata hivyo, alisema tayari serikali imetoa taarifa kwa wananchi kuanza kuondoka kutoka katika maeneo yote chepechepe hususan katika kingo za mito na vijito kwakuwa si salama kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha milimani hivi sasa.

" Tumeagiza uongozi katika serikali ya kijiji kwa kila eneo kuanza kutathmini hali ya ongezeko la maji na usalama katika maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wanahama kabla ya kukutwa na maafa. Aidha, kwa upande wa wazazi na walimu wakuu wa shule za msingi nao nawataka wahakikishe watoto wanasindikizwa na watu wazima wakati wa kwenda na kurudi shuleni ili kuhakikisha usalama wao," alisema.


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO