T AKWIMU za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) za Februari, 2017, zao la Korosho limeingiza jumla ya dola za Marekani milioni 346.6, kulinganish...
TAKWIMU za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) za Februari,
2017, zao la Korosho limeingiza jumla ya dola za Marekani milioni 346.6,
kulinganisha na mwaka 2016 ambazo zilikuwa milioni 184.9. Kiasi hicho cha maingizo kinafanya Korosho kuwa zao
namba moja kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni nchini.
Takwimu hizo zilitolewa katika mkutano wa kujadili
mustakbali wa zao hilo, Dodoma hivi karibuni.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu
wa Wadau wa Tasnia ya Korosho nchini, uliofanyika Chuo cha Mipango, Dodoma, Mei
13 na Mei 14, mwaka huu, alisema kutokana na mchango wa zao hilo kwa umma na
pia kwa taifa Serikali
ya awamu ya tano italilinda zao la Korosho kwa kufa na kupona.
“Mwelekeo wa Serikali kwenye Sekta ya Kilimo ni
kuhakikisha kuwa kilimo kinakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha uchumi wetu,
kuongeza kipato cha mkulima, na kuchochea ukuaji wa viwanda ili kuongeza
ajira.” Alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, korosho
huendesha maisha ya kaya zaidi ya 500,000 kama zao kuu la kibiashara katika
wilaya zaidi ya 30 katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga.
Na sasa idadi ya Watanzania watakaokuwa wakiguswa
moja kwa moja na korosho inatarajiwa kuongezeka zaidi, na pengine hata kufikia
nusu ya Watanzania wote kutokana na mipango iliyo mbioni kutekelezwa, ya
kupanua kilimo cha Korosho.
Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba; Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho (CBT) Hassan Jarufu na Kituo cha Utafiti wa
zao la Korosho, Naliendele, Mtwara wamezungumzia uwezekano wa Korosho, ama
maarufu kama “Dhahabu ya Kijani”, kulimwa katika sehemu nyingine za Tanzania.
Kwamba
mbali na wakulima wa asili wa Korosho, Mikoa ya Pwani, Lindi, Tanga, Mtwara na
Ruvuma, sasa utafiti umeonyesha Korosho inastawi pia katika Mikoa ya Dodoma,
Mbeya, Njombe, Iringa, Morogoro, Tabora na Singida.
Hiyo ni
takriban mikoa 12 kati ya mikoa yote nchini. Kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2012,
mikoa hiyo ina wakazi wapatao milioni 25. Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya
watu milioni 50.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu Jarufu anasema upanuzi huo wa eneo la kilimo cha Korosho
unakwenda sambamba na uamuzi wa CBT kugawa bure kwa wakulima miche milioni 10
kila mwaka, kwa miaka mitatu, kuanzia na mwaka huu.
Lakini
pia, kwa nia ya kuhakikisha ya kuwa mkulima wa Korosho anafaidika, Waziri, Dk.
Tizeba amewatangazia wadau wa Tasnia ya Korosho kwamba Serikali msimu huu
itagawa bure dawa ya sulphur ambayo ni muhimu sana katika kilimo cha Korosho na
kwamba magunia yanayotumika kama vifungashio muhimu, nayo yatatolewa bure.
Ukiweka kando mipango hiyo mizuri ya kupanua kilimo
cha Korosho, Tasnia ya Korosho kwa ujumla, inakabilia na changamoto nyingi.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, changamoto hizo
ni pamoja na umri mkubwa wa mikorosho
unaosababisha mavuno haba; ununuzi holela wa korosho kupitia “Kangomba”;
ubadhirifu kwenye vyama vya ushirika, vyama vikuu na vya msingi; tozo nyingi
zinazopunguza faida ya mkulima; utegemezi kwa soko la nje; uuzaji wa korosho
ghafi badala ya kuziongeza thamani; Vyama Vikuu na Vyama
vya Msingi kutokuwa na takwimu sahihi za idadi ya wakulima na mikorosho.
Mheshimiwa Majaliwa anasema kutokana na umuhimu wa
zao la Korosho, Rais Dk. John Magufuli ameridhia kuchukua hatua kuliimarisha.
Hatua hizo ni pamoja na kufuta tozo tano kati ya
tisa zilizokuwa zinalalamikiwa na wakulima wa Korosho. Tozo hizo ni ya kusafirisha korosho Sh. 50 kwa kilo; gharama
ya Mtunza Ghala Sh. 10 kwa kilo kulipwa na mkulima; ushuru wa Chama Kikuu cha
Sh. 20 kwa kilo; Kikosi Kazi cha ufuatiliaji zao Sh. 1 kwa kilo; na Makato ya
unyaufu.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema pia kwamba
Serikali imefuta kilichokuwa kinajulikana kama Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho (CIDTF) na sasa
shughuli zake zitafanywa na Bodi ya Korosho.
“Tumechukua
pia hatua dhidi ya viongozi wa vyama vya ushirika wasio waaminifu. Na
tutaendelea kuchukua hatua. Aidha, tunaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya
viongozi wa Serikali na Ushirika wanaojihusisha na ubadhirifu wa fedha za
ushirika na wakulima,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa akiongeza:
“Tunaposema Hapa Kazi Tu, tunamaanisha kila mmoja
atimize wajibu wake ipasavyo. Mkulima alime kwa kuzingatia stadi za kilimo;
mnunuzi azingatie taratibu tulizojiwekea; kiongozi wa Ushirika aendeshe
Ushirika kwa uadilifu mkubwa na msimamizi wa zao (Bodi), awe nahodha wetu
kwenye kuimarisha zao husika kwa kuishauri vizuri Serikali kuhusu namna ya
kwenda mbele zaidi.”
Akiwasilisha mada: Athari za Rushwa katika Tasnia
ya Korosho nchini, katika Mkutano huo wa Wadau wa Tasnia ya Korosho, Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Valentino Mlowola
alisema taasisi yake itakuchukua hatua ikipata taarifa za rushwa.
“Wito wangu kwa wadau wa Korosho ni kuichukia
rushwa na kuidhibiti; Ushirika imara na endelevu utajengwa na wadau wote iwapo
mtaamua kufuata sheria, kanuni na taratibu mlizojiwekea na kuweka pembeni
maslahi yenu binafsi.
TAKUKURU itaendelea kushirikana nanyi wakati wote
na hatutosita kuchukua hatua pale mtakapotuletea taarifa za vitendo vya rushwa.
Kuna malalamiko mengi kutoka kwa wakulima ambayo mengine yanasababishwa na ukosefu wa uadilifu na kuwapo
kwa rushwa,” alisema.
Alisema Tasnia ya Korosho ina changamoto ambazo
zinahusishwa moja kwa moja na wadau ambao ni Wazalishaji Korosho; Wanunuzi
(Wafanyabiashara) na Watendaji wa Serikali/Wanasiasa na zimekuwa zikizua
migogoro mingi.
“Makundi haya yanasababisha migogoro mingi kwenye
vyama vya Msingi na Vikuu inayodidimiza dhana nzima ya Ushirika; Kutolipwa/
Kupunjwa fedha za mauzo ya Korosho baada ya Korosho zote kuuzwa minadani.
Kuna mlolongo wa kodi nyingi zinazotozwa kwenye
mauzo ya Korosho, mfano; makato ya usambazaji wa fedha na kinachoitwa Task
Force. Ugumu wa upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Huduma za Ugani kutosambaa
kwa wakulima wengi. Changamoto zinazohusu maofisa wa umma na wanasiasa kutosimamia
vyema Sheria na Taratibu zinazotawala sekta; kuwachanganya wafanyabiashara kwa
kutoa maagizo ambayo wakati mwingine yanapingana na sera na sharia na kubuni
Sera na Taratibu ambazo zinawaathiri wakulima na wafanyabiashara na kushirikiana
na wafanyabiashara na kujipatia maslahi binafsi.”
Alisema alikuwa akiyasema hayo kutokana na ukweli
kwamba na yeye amekuzwa na uchumi wa Korosho: “ nayasema haya kwa sababu
nayajua kutokana na kuwa nimekuzwa na uchumi wa Korosho. Si kwa kuyasoma tu
vitabuni”.
Maazimio kadhaa yalifikiwa katika Mkutano huo wa
Wadau wa Tasnia ya Korosho nchini ambayo ni pamoja na Vyama vya Ushirika
viajiri wafanyakazi wenye weledi akaunti za benki ili kurahisisha malipo,
kuwezesha usalama wa fedha zao na kwa jumla kupunguza wizi na mitandao ya simu
itumike kurahisisha malipo.
COMMENTS