Waombolezaji, wakiwa wamebeba jeneza lililokuwa na mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, wakati wa kutoa heshima za mwisho katika viwanja vya Majengo, Moshi mkoani Kilimanjaro.

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amelishauri jeshi la polisi kutotumika katika masuala ya kisiasa kwani kwa kufanya hivyo ni kujenga chuki baina ya serikali na wananchi jambo ambalo huenda likaathiri umoja wa kitaifa uliopo.
Alisema hayop wakati wa shughuli ya kumuaga mbunge mstaafu wa jimbo la Moshi mjini, hayati Philemon Ndesamburo jana.
"hii inasikitisha wananchi wanataka kumuaga mpendwa wao katika uwanja wa Mashujaa....inafika usiku tunapokea barua kwamba haturuhusiwi kwa visingizio vya kuwepo kwa shule na mahakama, hili linaonesha dalili za ubaguzi wa wazi, tunajenga chuki...epukeni,tutaligawa taifa"alisema.
Alitaka viongozi wa serikali akiwamo Waziri mkuu , Kasim Majaliwa na Rais Dk John Pombe Magufuli kulijenga taifa kwa misingi ya umoja badala ya mfumo uliopo sasa, mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kuonekana kama wasaliti wa serikali.
Nao mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye  waliomba serikali kulinda uhuru wa kidemokrasia badala ya kuuminya kama ambavyo imejidhihirisha katika shughuli ya kuaga mwili wa mbunge mstaafu wa Moshi mjini Hayati Ndesamburo.
"Kuna watu wanajitahidi sana kuminya demokrasia , hii madhatra yake ni makubwa, wananchi ni wengi mno kuliko vyombo vya dola, wakiamua kutaka demokrasia hiyo hatutafika pazuri"alisema.
Viongozi hao walimtaja Ndesamburo kama nguzo imara ya mageuzi ya kisiasa nchini kwa kuendesha siasa za kistaarabu mkoani Kilimanjaro.
Mapema akizungumza kwa niaba ya katibu wa wabunge wa CCM, mbunge wa viti maalum, Ester Mmasy alitoa pole kwa familia ya hayati Ndesamburo pamoja na Chadema kwa kumpoteza  kiongozi mahiri na mpenda maendeleo.
Mwili wa Ndesamburo uliingia uwanjani saa 6:36 mchana na jeneza kubebwa na wabunge na baadaye madaktari wenzie waliotunukiwa pamoja stashahada ya udaktari Desemba 17, 2016 kutoka Chuo cha biblia cha Japan, waliweka joho kama ishara ya heshima
Baadhi  ya viongozi wa dini, wamemtaja mbunge mstaafu wa jimbo la Moshi mjini, hayati Philemon Ndesamburo kama mtu asiyekuwa na makuu na mrahisi kuwasiliana na kuonana naye ikilinganishwa na watu wengine wenye nyadhfa katika maeneo mbalimbali.
Akitoa salama za baraza kuu la waislamu nchini (BAKWATA), mjumbe wa halmashauri kuu ya baraza hilo, Shehe Mlewa Shaaban alisema kwa kipindi ambacho amemfahamu Ndesamburo alimuona kama mtu aliyejitoa katika kusaidia jamii zaidi.
"Mungu alimpa hayati Ndesamburo karama ya peke yake, kwa jinsi nilivyomfahamu hakuna na makuu wala majivuno kwa kile alichonacho.....wapo baadhi ya wafanyabiashara kwa jinsi walivyo ukitaka kumuona ni bora umtafute Mungu, unaweza kumuona,  kuliko yeye"alisema.
Aidha alisema Ndesamburo, aliwasaidia maimamu wa misikiti ya Moshi mjini kwa kuwapa pikipiki, alisaidia kuchimba visima kwenye misikiti, alijenga madrasa, amewasafirisha maimamu kwenda Dodoma kuangalia shughuli zinazoendelea pia amewapa waislamu kipindi cha maalamu cha kutoa mawaidha kwenye redio yake ya Moshi FM.
Awali akizumngumzia hayati Ndesamburo, mwasisi wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Edwin Mtei alisema alikuwa kiongozi msikivu na mwenye mtazamo wa kuleta mabadiliko ya wananchi kiuchumi na kijamii.
"Nimefanya kazi na Ndesamburo hata miaka ile ya 1991 tunafanya harakati za kuleta mageuzi ya kisiasa tulikuwa pamoja na alitumia fedha zake na muda ili kuona taifa linakuwa na mabadiliko ya kifikra ikizingatiwa tulikuwepo katika mfumo wa Chama kimoja cha siasa"alisema.
mwisho


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO