Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi , Mohammed Abdullah Aden (12) wa Somalia hundi ya shilingi milioni 15, 750,000/= mshindi wa ...
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Waziri Mkuu amuagiza Meya wa
Temeke kesho atoe maamuzi ya kiwanja
MTOTO wa miaka 12 kutoka
Somalia, Mohammed Abdullahi Aden ameibuka kidedea na kitita cha dola za
Marekani 7,000 (sawa na sh. milioni 15.75) katika mashindano ya 18 ya Afrika ya
kuhifadhi Quran kwenye kundi la washiriki wa juzuu 30.
Mohammed ambaye ni miongoni
mwa washiriki wadogo zaidi wawili kuliko wote (mwenzake anatoka Burundi),
amejishindia pia IPAD, cheti, kompyuta iliyotolewa na Balozi wa Kuwait, ahadi
ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na ahadi ya kwenda
nchi yoyote aitakayo kutoka kwa kampuni ya Sky Bus Travel Agency ya jijini Dar
es Salaam.
Akizungumza na maelfu ya waumini
na Watanzania waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo
mchana (Jumapili, Juni 11, 2017), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa waandaaji wa mashindano
hayo ambayo ni Taasisi ya Al-Hikma waangalie uwezekano wa kuboresha
zawadi kwa kutoa scholarships (udhamini) kwa washindi au washiriki,
hususan kwa washiriki wa Tanzania.
“Ongeeni na nchi marafiki
kama Saudi Arabia, waone uwezekano wa kutoa zawadi za ufadhili kwenye masomo ya
sekta za kimkakati kama vile mafuta na gesi, ili kuongeza hamasa na chachu ya
vijana walioko kwenye sekondari zetu nao waone fursa hii na kuichangamkia,
badala ya mashindano kujikita kwenye madrasa peke yake,” amesema.
Waziri Mkuu amewataka
wazazi wafuatilie nyendo za vijana wao ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa
za kulevya na vitendo vingine viovu vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na
ustawi wa nchi yetu lakini akasisitiza pia waisaidie Serikali katika mapambano yake
dhidi ya rushwa na ufisadi.
“Endeleeni kushirikiana na
Serikali katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi na kuwafichua wakwepa
kodi. Kila mmoja wetu ahakikishe analipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria. Hii
itasaidia Serikali kuboresha huduma kwa wananchi ili waweze kufanya ibada zao
vizuri zaidi,” amesema.
Washindi wengine kwenye kundi
hilo na umri wao kwenye mabano ni Abdulkarim Ahmed Farhina (22) wa Sudan ambaye
ameshinda dola za Marekani 5,000, cheti, IPAD, kompyuta iliyotolewa na Balozi
wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wa tatu ni Mahamoud Ali
Chamfi wa Comoro (18) na Seif Ramadhani Zombe (18) kutoka Taasisi za Tanzania
ambao wote wamepata dola za marekani 3,000, cheti, IPAD, kompyuta iliyotolewa
na Balozi wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam.
Wa nne ni Khalil Mussa
Hussein (17) kutoka Tanzania Bara ambaye amepata dola za marekani 1,500, cheti,
IPAD, na ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Wa
tano ni Ismail Issa Qasim (17) kutoka Tanzania Visiwani ambaye dola za marekani
1,000, cheti, IPAD, na ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam,
Washiriki wengine kwenye
kundi la juzuu 30 walitoka nchi za Nigeria, Kenya, Uganda, Djibouti, Afrika
Kusini, Rwanda, Ghana, Ethiopia, Congo DRC, Burundi na Msumbiji. Umro wao
ulikuwa ni kati ya miaka 12 na 26.
Washiriki wengine
waliopewa zawadi ni wale walioweza kuhifadhi Juzuu tatu (washindi watano),
Juzuu tano (washindi watatu); Juzuu 10 (washindi watatu) na Juzuu 20 (washindi
watatu).
Viongozi wengine
waliohudhuria kilele hicho ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan
Mwinyi, Makamu wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Mohammed Gharib Billal,
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Balozi wa Saudi Arabia nchini
Tanzania, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Malek. Wengine ni wawakilishi wanne wa
Imam Mkuu wa Mskiti Mtakatifu wa Makkah, Sheikh Abdul Rahman Ibn Abdul Aziz
as-Sudais; Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amemuagiza Meya wa Temeke, Bw. Abdallah Chaurembo kesho (Jumatatu, Juni
12, 2017) afuatane na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bw. Nassib Mmbaga hadi
kwenye kiwanja kilichopo eneo la Matumbi na kukagua kama kuna uwezekano wa
kuliongeza kwa taasisi ya Al-Hikma na wampe majibu Jumanne kwani limekaa wazi
kwa muda mrefu licha ya kuwa walishaliomba na hawakupata majibu.
“Mstahiki Meya wa Temeke na
Mkurugenzi wako, kesho Jumatatu nendeni mkaangalie eneo husika kama linafaa
kuongezwa na mfanye maamuzi. Eneo hilo limekaa wazi kwa muda mrefu, na hawa
wanataka wanataka kujenga zahanati. Jumanne asubuhi nipate taarifa ya maamuzi
yenu,” alisema Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya waumini waliokuwepo
kwenye hafla hiyo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JUNI 11, 2017.
COMMENTS