JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI Simu: +255-22- 2112035/40 Nukus...
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
|
|
|
Simu: +255-22-2112035/40
Nukushi:
+255-2122617/2120486
|
9 Barabaraya Ohio
S.L.P.
9223
11483 DAR ES SALAAM
|
MAADHIMISHO YA SIKU YA WAKIMBIZI DUNIANI TAREHE
20 JUNI, 2017
Kila mwaka, tarehe
20 Juni, Mataifa yote ulimwenguni huadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani (World
Refugee Day). Awali siku hiyo ilikuwa inaadhimishwa Barani Afrika peke yake
ikiitwa Siku ya Wakimbizi Barani Afrika na kuanzia mwaka 2001 Maadhimisho hayo
yalianza kufanyika Duniani kote baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
kuelekeza hivyo katika kuadhimisha miaka 50 ya Sheria ya Kimataifa ya
Wakimbizi.
Lengo la maadhimisho
haya ya kila mwaka ni kuhamasisha Ulimwengu kutambua uwepo wa mamilioni ya
wakimbizi na watu wengine wanaohama kutoka kwenye maeneo yao kwenda maeneo
mengine ndani ya nchi zao (internally displaced persons) kuogopa vita, migogoro
na mateso.
Maadhimisho haya
huwahusisha viongozi wa serikali, watumishi wa mashirika ya misaada, watu
mashuhuri na wakimbizi wenyewe. Maadhimisho haya huambatana na kauli mbiu
ambayo kutoa msisitizo wa jambo ambalo hupewa msukumo katika matamko ya mwaka
husika ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tuko
Pamoja na Wakimbizi’ ikiwa na lengo
la kukumbusha jukumu la kila mmoja la kuwasaidia wakimbizi na kutafuta ufumbuzi
wa matatizo ambayo yamesababisha wao kujikuta katika hali hiyo.
Kama
inavyofahamika Tanzania imekuwa na historia ndefu ya kuhifadhi wakimbizi toka
nchi mbalimbali za Afrika na kwingineko.
Kwa vipindi mbalimbali wamekuwepo wakimbizi tofauti tofauti kama vile wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi
za Kusini ya Afrika ambapo kulikuwa na wakimbizi toka Afrika Kusini, Namibia,
Msumbiji, Angola na Zimbabwe ambao walirudi katika nchi zao za asili baada ya
ukombozi kupatikana katika nchi hizo.
Aidha, nchi yetu
inaendelea kuhifadhi wakimbizi toka nchi za jirani zinazokumbwa na migogoro ya
kisiasa na kivita hususani zile za Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Pembe ya Afrika kama Somalia na wachache toka nchi mbalimbali.
Maazimio ya mwaka
huu, ya Siku ya Wakimbizi Duniani yanaikuta nchi yetu ikiwa inahifadhi
wakimbizi wapatao 345,000, wengi wao
wakiwa wanatoka katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na
ambao wanahifadhiwa katika kambi zilizoko Mkoa wa Kigoma za Nyarugusu, Nduta na
Mtendeli na wengine wachache waliosalia baada ya wenzao wengi kupata uraia
ambao wapo Katavi na Tabora.
Kwa kuzingatia
uwepo wa wakimbizi hao, maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika Dar es Salaam
ambapo yatahusisha Wakimbizi wenyewe, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Viongozi
wa Serikali, Asasi zisizo za Kiraia, watumishi wa Mashirika ya Misaada, na
Wasanii maarufu, vyombo vya habari, wananchi na kwenye maeneo yanayohifadhi
wakimbizi katika Mikoa iliyotajwa.
Serikali yetu
itapenda kutumia maadhimisho ya mwaka huu kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa, wakimbizi
wenyewe pamoja na wadau mbalimbali kuwa itaendelea kuchukua hatua muhimu za kuboresha
huduma kwao katika sekta za elimu, afya, makazi na kuihuisha Sera ya Wakimbizi
ili ieandane na changamoto za wakati huu.
Kwa upande wa
elimu, Serikali inatambua tatizo la upungufu wa madarasa katika kambi za
wakimbizi linalotokana na upungufu wa fedha zinazotolewa na Wahisani kufadhili
mradi mzima wa kuhifadhi maelfu ya wakimbizi toka nchi za jirani na kwingineko.
Pamoja na hayo, nchi yetu kwa kushirikiana na UNHCR na wadau wengine itafanya
jitihada za kujenga madarasa na miundo mingine muhimu kuhakikisha kuwa watoto wote
wa wakimbizi wanapata elimu bora kuwawezesha kupata taaluma na ujuzi utakaowanufaisha wao
wenyewe na jamii zao wakiwa kwenye kambi na wakati watakaporejea kwenye nchi
zao za asili .
Vile
vile Serikali, kupitia taasisi yake ya RITA, inakusudia kutoa vyeti vya kuzaliwa,
kwa watoto wa wakimbizi ambao wanazaliwa hapa nchini, katika kambi za wakimbizi,
ili kuwafanya watoto hao kuwa na hati
zinazotambulika kisheria na zenye kubainisha waziwazi uraia wao wa asili. Ni
vema ikafahamika kuwa hati hizo ni muhimu hata baada ya maisha ya ukimbizi.
Uamuzi wa kuwapatia hati unafuatia
makubaliano baina ya serikali na UNHCR
yanayowezesha Shirika hilo kusaidia
nyenzo
muhimu zinazohitajika katika zoezi hilo.
Ni nia ya Serikali
kuhakikisha kuwa wakimbizi wanapata hati zote muhimu zinazohitajika kama cheti
cha kuzaliwa, kitambulisho n.k kwa mujibu ya Mikataba ya Kimataifa mbayo
nchi imeiridhia. Ni matarajio ya
Serikali kuwa vyeti vya kuzaliwa vitaanza kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu
na utakuwa ni utaratibu wa kudumu.
Eneo jingine
ambalo litapewa kipaumbele kwa lengo la kuboresha huduma kwa wakimbizi ni mradi
wa kuhuishwa Sera ya Wakimbizi na Sheria pamoja na mambo mengine, Sera mpya na Sheria zitakazotungwa inakusudia kupanua
wigo wa wakimbizi wenye ujuzi na sifa za kupata ajira kama wataalamu katika
sekta mbalimbali na pia kupata fursa za kujiari wenyewe nje ya kambi.
Wakati dunia inaadhimisha
siku ya Wakimbizi Duniani, ni vema pia tukaikumbusha Jumuia ya Kimataifa kuhusu
wajibu wao kuongeza ufadhili kuzisaidia nchi changa, kama Tanzania, kutekeleza
jukumu la kuhifadhi wakimbizi. Misaada
wanayotoa inasaidia katika kupatikana
kwa bidhaa mbalimbali ambazo zitatumiwa na wakimbizi na huduma nyingine wanazohitaji. Ni vema ikaeleweka pia kuwa Jumuia ya
Kimataifa ina wajibu wa kuzisaidia jamii ambazo zinaathirika na uwepo wa
wakimbizi wengi kama Kagera, Kigoma,
Katavi na Kigoma.
Imetolewa na
Balozi Hassan Simba
Yahya
Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi,
19 Juni, 2017
COMMENTS