Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi na kuzindua kazi za mradi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam utakaoiwezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa na kuongeza kiasi cha mizigo ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.
Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi imefanyika katika eneo la bandari hiyo Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird.
Ujenzi, ukarabati na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umepangwa kufanyika kwa miezi 30 kuanzia sasa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 926.2 ambapo kati yake Shilingi Bilioni 132 zinatolewa na Serikali ya Tanzania, Shilingi Bilioni 770 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Shilingi Bilioni 24 ni Msaada kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID).
Kazi za ujenzi, upanuzi na ukarabati huo zitafanyika katika gati namba 1 hadi gati namba 7 ambazo zinaendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na zitahusisha kujenga gati hizo, kuongeza kina cha bahari kwa kuongeza urefu kutoka wastani wa mita 12 hadi kufikia mita 15.5 na kukarabati miundombinu wezeshi ya bandari.
Mradi huu mkubwa utaiwezesha bandari ya Dar es Salaam kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa kutoka meli zenye urefu wa meta 243 na uwezo wa kubeba makontena kati ya 2,500 na 4000 hadi kufikia meli zenye urefu wa meta 320 na uwezo wa kubeba makontena kati ya 6,000 na 8,000 na pia kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena za mizigo kutoka tani Milioni 18 za sasa hadi kufikia tani Milioni 28 ifikapo mwaka 2022.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wadau wa maendeleo walioshiriki kufanikisha mradi huo ambao ni Benki ya Dunia na DFID na amesema mradi huu ukikamilika utaiwezesha bandari kuwa ya mfano, na ametaka wakandarasi wanaojenga mradi huo waukamilishe haraka ikiwezekana kabla ya miezi 30 kuisha ili Tanzania na nchi za Rwanda, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, Malawi na Zimbabwe zianze kunufaika mapema.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha bandari zote nchini lakini ameitaka TPA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza udhibiti wa mizigo inayoingia na kutoka kupitia bandari kwa kuhakikisha mizigo hiyo inakuwa halali na inalipiwa kodi ipasavyo.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupigania maslahi ya nchi na ameonya dhidi ya baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakibeza juhudi hizo pamoja na juhudi za kukabiliana na wahalifu ambao wanawaua raia wasio na hatia pamoja na askari polisi.
“Wajifunze kufunga midomo yao wakati Serikali inafanya kazi yake, na kwa ujumbe huu nataka Watanzania waelewe kuwa tuna mambo makubwa katika nchi hii tunayoshughulika nayo, na ndio maana wakati mwingine unakuta ni mzahamzaha tu, unakuta wakati mwingine mnashughulikia rasilimali za Watanzania zinazoibiwa, mtu mwingine anapinga hadharani” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakizungumza kabla ya hotuba ya Rais, Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird wamempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali kwa juhudi kubwa zilifanyika kuongeza uwazi na ufanisi wa bandari, kudhibiti wizi, mizigo haramu na rushwa, na wameahidi kuendeleza uhusiano mzuri kati ya Serikali na vyombo wanavyoviwakilisha.
Nao Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa Ghasia wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya kuimarisha miundombinu na wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Julai, 2017


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO