Wafungwa 8,157 wamefaidika na msamaha na Msamaha wa Rais katika kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara leo. Kati ya wafungwa...
Wafungwa 8,157 wamefaidika na msamaha na Msamaha wa Rais katika kuadhimisha
miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara leo.
Kati ya wafungwa hao 1,828
wataachiliwa huru tarehe 9 Disemba, 2017 na 6,329 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki
baada ya kupewa msamaha huu.
Aidha Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli kwa mujibu wa Ibara ya
45(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inampa Mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa
ajili ya kosa lolote au kufuta adhabu yote.
Kwa
kutumia Mamlaka aliyo nayo amewasamehe wafungwa wengine 63
kati yao wafungwa 61 ni wale waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa, waliokuwa
na umri mkubwa na waliokaa gerezani muda mrefu.
Na pia
amewasamehe wafungwa wengine wawili waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha
ambao ni Nguza Viking(BABU SEA) na
Johnson Nguza. Hivyo kwa ujumla amewasamehe wafungwa 8220.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka Mambo ya Ndani katika utoaji wa msamaha huo kwa
kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-
(i)
Wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita (1/6)
ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1)
cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika
Ibara ya 2(i – xxi).
(ii)
Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI,
Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga
chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa
Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
(iii)
Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au
zaidi. Umri huo uthibitishwe na Jopo la
Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu
wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
(iv)
Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani,
pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
(v)
Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability).
Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
2. Aidha, Msamaha wa Mheshimiwa Rais
hautawahusu wafungwa wafuatao:-
(i)
Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa
makosa ya kujaribu kuua (attempt to
murder).
(ii)
Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na
adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
(iii)
Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha
gerezani.
(iv)
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya
kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.
(v)
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya
kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.
(vi)
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya
unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and
attempted robbery).
(vii)
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya
kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).
(viii)
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya
shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, ukatili kwa watoto au kujaribu
kutenda makosa hayo.
(ix)
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa
kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za
Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane
(18) na kuendelea.
(x)
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi
wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa
hayo.
(xi)
Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya
Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No.
6/2002).
(xii)
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa
kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na kuhujumu uchumi.
(xiii)
Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha
wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo
kilichobaki.
(xiv)
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa
kosa la kuzuia watoto kupata masomo.
(xv)
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa
kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human
Trafficking).
(xvi)
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa
kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.
(xvii)
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya
kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).
(xviii)
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya
wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.
(xix)
Wafungwa
wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya
ulinzi halali.
(xx)
Wafungwa
walioingia gerezani baada ya tarehe 30/10/2017.
(xxi)
Wafungwa
waliowahi kufungwa gerezani.
COMMENTS