ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dk Joel Nkaya Bendera  amefariki leo jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikofikishwa kwa ajili ya kupata matibabu.
Bendera ambaye ndiye kocha pekee aliyeitoa kimasomaso katika miaka ya 1980 kw akutupeleka Nigeria wakati akifundisha soka, kazi yake ya mwisho ilikuwa mkuu wa mkoa wa Manyara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha, Bendera ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo alifariki saa 10:20 jioni wakati akipatiwa matibabu kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura.
Aligaesha alisema Bendera alifikishwa hospitalini hapo saa 6:00 mchana akitokea kwenye Hospitali ya Bagamoyo.
Kutokana na kifo hicho, Rais John Magufuli ametuma salamu za pole kwa familia, ndugu na jamaa.
“Jioni hii nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mkuu wa Mkoa Mstaafu Dkt. Joel Nkaya Bendera, natoa pole kwa familia yake na wote walioguswa na msiba huu na pia naungana nao katika kipindi hiki cha majonzi” ilisema taarifa ya Ikulu ikimkariri Rais Magufuli.
Katika taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Magufuli alisema Dk Bendera atakumbukwa kwa mchango wake alioutoa kwa Taifa akiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali, zikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Naibu Waziri , Mbunge na pia kwa mchango wake katika maendeleo ya michezo nchini kama kocha.
“Dk Joel Nkaya Bendera alikuwa kiongozi shupavu, mahiri na mchapakazi, alipenda kufanya kazi kwa ushirikiano na daima alitamani kupata mafanikio makubwa katika majukumu aliyokuwa nayo, hakika tutamkumbuka,” alisisitiza Rais Magufuli.
Pamoja na kutoa pole kwa familia ya marehemu, Rais Magufuli pia amewapa pole wananchi wa Mkoa wa Manyara ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa hadi Oktoba 26, 2017, wananchi wa Mkoa wa Tanga ambako alikuwa Mbunge, wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wanamichezo na wote walioguswa na msiba huu.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO