MAAZIMIO YA MKUTANO KATI YA SMZ NA SMT KUSHUGHULIKIA MELI ZINAZOPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KWA TUHUMA ZA KUSAFIRISHA SILAHA NA MADAWA ...
MAAZIMIO YA MKUTANO
KATI YA SMZ NA SMT KUSHUGHULIKIA MELI ZINAZOPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KWA
TUHUMA ZA KUSAFIRISHA SILAHA NA MADAWA YA KULEVYA, TAREHE 17 JANUARI 2018
Ndugu Waandishi wa
Habari, nimewaita hapa kuzungumza nanyi na kupitia kwenu kuzungumza na
wananchi wenzangu kuhusu taaarifa ya kukamatwa kwa meli zilizokuwa zimepakia
shehena za dawa za kulevya na silaha zikiwa zinapeperusha bendera ya nchi yetu.
Meli hizo ni:
i. Kaluba yenye usajili
namba IMO 6828753 iliyokamatwa tarehe 27 Desemba 2017 ikiwa na wastani wa kilo
1,600 za dawa za kulevya huko katika maeneo ya Jamhuri ya Dominican Republic;
na
ii. Andromeda yenye
namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa kwa kusafirisha
silaha kinyume na Sheria za kimataifa.
Meli zote mbili zimesajiliwa Tanzania kupitia taasisi yetu
ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ambayo ndiyo imepewa mamlaka
ya kusajili meli za nje.
Hapa kwetu
Tanzania tuna aina mbili za kusajili Meli; usajili wa Meli zenye asili ya
Tanzania na zile zenye asili ya Nje. kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi
mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake mbalimbali, siku zote tumekuwa
tunaheshimu na kutekeleza kikamilifu majukumu yetu ya kimataifa yaliyowekwa
kupitia mikataba na maazimio mbalimbali ya vyombo hivyo.
Ndugu Waandishi wa
Habari, kwa mujibu wa mkataba wa UNCLOS 1982 kila nchi imepewa haki
ya kufanya usajili wa meli kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa na sheria za
nchi husika.
Kwa upande wa
Tanzania, usajili wa meli za kimataifa
unasimamiwa na Sheria Na 5 ya mwaka 2006,
(Kwa upande wa
SUMATRA ina Merchant Shipping Act ya mwaka 2003. Sheria hi inaruhusu usajili wa
meli inayomilikiwa na Mtanzania, au meli inayomilikiwa kwa ubia kati ya
Mtanzania na raia wa nchi nyingine. Kwa sheria hii ili meli ipate usajili wa
SUMATRA na kuruhusiwa kupeperusha bendera ya Tanzania ni lazima umiliki wa meli
uhusishwe na raia wa Tanzania kwa umiliki wote au kwa ubia lakini ni lazima
Mtanzania awe na hisa nyingi. Vilevile kampuni hiyo ya umiliki lazima iwe ya
Kitanzania kwa maana ya kusajiliwa na kujiendesha kutokea Tanzania hata kama
kampuni hiyo inamilikiwa na watu wasio Watanzania. Na kwa upande wa Zanzibar
kupitia ZMA wana Maritime
Transport Act ya mwaka 2006).
Sheria hii inaruhusu usajili wa meli yoyote hata kama mmiliki wake sio Mtanzania wala kampuni kuwa ya Kitanzania hivyo basi kutoa fursa kwa meli ambayo haina umiliki wa aina yeyote wa Tanzania kwa maana umiliki na ukazi kupewa usajili wa kupeperusha bendera yetu nje ya Tanzania. Aidha, Sheria hizi huendeshwa sambamba pamoja na Sheria na Kanuni za Kimataifa.
Ni vyema
tukafahamu kuwa Sheria na Kanuni hizo humlazimu mwenye Meli, kujaza fomu
maalumu ya maombi pamoja na Fomu za “DECLARATION OF VESSELS NON INVOLVEMENT
WITH CRIMINAL ACTS OR OMISSIONS”; na ndipo hatua nyingine za kufanya
uchunguzi wa historia ya meli kupitia International Maritime websites na
vyanzo vingine, tangu Meli
ilipotengenezwa hadi muda inapoomba usajili.
Uhakiki
hufanywa pia kupitia mitandao mingine mikubwa mitatu inayotumika duniani kote
kupata historia ya meli, Mitandao hiyo ni:
i. Fleet Moon;
ii. Maritime Traffic; na
iii. Maritime-connector.
Baada ya ZMA
ambayo ndio kisheria imeruhusiwa kusajili meli nje ya Tanzania, kujiridhisha na
maelezo na taarifa zilizopatikana, maamuzi ya kusajili au kutosajili yanatolewa
kupitia Idara ya Usajili.
Ndugu Waandishi wa
Habari, kwa mujibu wa taratibu za Mkataba wa Kimataifa wa
Kupambana na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya, 1988 na Azimio la Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa 1970
(2011).
nchi zilizosajili
Meli zinazokamatwa hutakiwa kutoa kibali kwa Walinzi wa Mwambao wa Bahari wa
nchi husika, na kwa Meli hizi, tulitoa kibali kwa Jeshi la Mwambao wa Marekani
na Jeshi la Mwambao wa
Ugiriki kuzikamata na kuzipekua meli hizo.
Baada ya kupata
taarifa za upekuzi hatua za haraka zilizochukuliwa upande wetu ni kufuta
Usajili wa Meli hizo.
Ndugu Waandishi wa
Habari, Tanzania vilevile ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa
Kupiga Vita Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya (United Nations
Convention Against Illicit Traffic of Narcotic Drugs and
Psychotropic Substance, 1988) na pia ni Mwanachama wa Mkataba wa
Kimataifa wa Kupiga Vita
Usafirishaji Haramu
wa Silaha (United Nations Protocol Against Illicit Manufacturing of and
Trafficking in Arms, their Parts and Components and Ammunition, Supplementing
the United Nations Convention Against Transnational Organized Crime, 2001).
Kwa mnasaba huu, tunapenda
kutoa taarifa kuwa Tanzania imejidhatiti na imedhamiria kutekeleza majukumu
yake yaliyoelezwa katika mikataba hiyo ya
kimataifa, ikiwemo
kushirikiana na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa katika kupiga
vita usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha. Nyote ni mashahidi
kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Tano imetangaza
vita dhidi ya watu wote wanaojihusisha na dawa za kulevya na vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha
vinatokomeza kabisa uhalifu huo.
Hivyo basi, taarifa
ya kukamatwa kwa meli zenye bendera ya Tanzania zikisafirisha dawa za kulevya
na silaha ni kinyume na Sheria za nchi yetu na zile za kimataifa. Taarifa hizi
zimeleta mshtuko mkubwa ndani ya nchi yetu. hasa kwa kuwa Tanzania
imejipambanua kupambana na maovu hayo kwa kutumia nguvu zote.
Ndugu
Waandishi wa Habari, kufuatia taarifa hizo, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aliniagiza kuitisha kikao cha dharura baina ya viongozi wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuzungumzia kadhia hiyo.
Jana Jumatano,
tarehe 17 Januari 2018, Viongozi na Wataalamu wa pande zote mbili wakiongozwa
na mimi mwenyewe na Mhe. Balozi Seif Ali Idi, Makamo wa Pili wa Rais, Zanzibar
tulifanya kikao kilichojadili masuala haya kwa kina huko Zanzibar.
Ndugu
Waandishi wa Habari, baada ya majadiliano ya kina kuhusu masuala haya, kikao
kilibaini yafuatayo:
· Suala la Usajili wa
Meli za Nje linafanywa na Nchi nyingi duniani; Kwa
mfano katika Bara la Afrika
nchi zinazofanya usajili wa kimataifa ni pamoja na Liberia,
Komoro na Sierra Leone. Aidha, kwa Bara la Asia, kuna nchi za China na
Singapore na kwa Amerika ya Kusini ni pamoja na Panama.
· Ilibainika kwamba
Wenye Meli hupendelea kusajili meli zao nje ya nchi zao kwa kukimbia uzito wa
kodi na sheria zinazobana shughuli zao.
· Wakala aliyekuwa
akifanya kazi hii kwa niaba ya ZMA na ambaye ameshavunjiwa Mkataba bado
anaendelea kufanya usajili kwa kuiba Bendera ya Tanzania.
Kutokana na hayo kikao kiliazimia yafuatayo:
i. Kutoa taarifa na
ufafanuzi wa kina kuhusu kadhia ya meli hizo kukamatwa na dawa za kulevya na
silaha kwa umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla ili kuondoa upotoshaji wa
aina yoyote kwa kupitia vyanzo visivyo rasmi. Kwa sasa ndio natekeleza azimio
hili;
i. Kwa kuwa uendeshaji
wa biashara hii unaonekana kuleta utata na kutia dosari kubwa kwa Taifa letu na
kuharibu sifa njema za Nchi yetu, imeonekana haja ya kuunda kamati ya pamoja ya
wataalam wa SMZ na SMT itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili
ya kupitiwa upya usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za
meli zote zilizosajiliwa nchini mwetu, kuangalia mwenendo mzima wa usajili, na
hatimaye kutoa mapendekezo na ushauri kwa Serikali;
ii. Kuanzisha utaratibu
wa kuzifanyia uchunguzi wa kina (due diligence) meli zote mpya
zitakazoomba usajili pamoja na wamiliki wake kwa kushirikisha vyombo mbalimbali
vya Serikali vikiwemo vile vya ulinzi na usalama;
iii. Kufanya mapitio ya
sheria zetu, ili kuzipa nguvu zaidi taasisi zinazosimamia usajili wa meli.
Wakati wa mapitio ya sheria, timu ya wataalam itaangalia kwa makini
kodi zinazotozwa na mchango wake nchini ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi
viwango kuomba usajili Tanzania;
iv. Kuendelea kushirikiana
na nchi nyengine kwa kuzipa ruhusa kukamata na kuzipekua meli zinazopeperusha
bendera yetu wakati wote zinapohisiwa kuwa zinafanya uhalifu, au masuala ambayo
haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazokubalika kimataifa
na wakati wa usajili.
Asanteni kwa
kunisikiliza.
COMMENTS