WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara Bw. Stephen Mafipa
kumtafuta popote alipo na kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji
wa Masasi Bw. Fortunatus Kagoro kwa tuhuma za matumizi mabaya
ya fedha.
Mbali na Bw. Kagoro pia Kaimu Mweka
Hazina Bw. Heri Hamad Afisa Mipango Bi Teresia Nsumba nao ameagiza
wakamatwe na baada ya uchunguzi watakaobainika kwamba hawajahusika na
ubadhilifu huo watarudishwa kazini. "Lazima fedha za Serikali zitumike kama
ilivyokusudiwa."
Watendaji hao wanadaiwa kutumia sh.
bilioni 1.8 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la
Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa kuchora mchoro na kujenga msingi katika maeneo
mawili tofauti.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumatatu, Februari 26, 2018) wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa
Halmashauri ya Mji wa Masasi na Halmashauri ya wilaya ya Masasi akiwa kwenye
ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.
Amesema mwaka 2014 Serikali
ilipeleka sh milioni 575 wilaya Masasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la
Halmashauri hiyo na fedha hizo ziliishia kutumika katika hatua za
maandalizi ya awali ikiwa ni pamoja na kutengeneza michoro ya jengo.
Waziri Mkuu amesema 2016/2017
Serikali ilipeleka tena sh. bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo
Halmashauri hiyo ilienda kutafuta eneo lingine na kufanya tena shughuli
zilizokuwa zimefanyika na kuanza ujenzi ambao umeishia katika msingi na fedha
zimeisha.
Pia amewataka watendaji hao kutotumia
fedha za makusanyo ya ndani kwa ajili ya kuziba pengo la fedha za mradi huo
ambazo baadhi yake hazijulikani zilipo na amewaagiza Madiwani kutoruhusu jambo
hilo.
"Madiwani msikubali kutumia
fedha za makusanyo ya ndani kupeleka kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo
ambayo tayari Serikali ilishatoa fedha ya ujenzi wake.
Amesema Serikali inahitaji kuona
fedha za maendeleo zinazopelekwa katika Halmashauri mbalimbali nchini
zinatumika kama ilivyoelekeza na si vinginevyo na Serikai haitakuwa na mzaha
kwa mtumishi atakayezitumia vibaya.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 26, 2018.
Post a Comment
Post a Comment