Nianze kwa kujitambulisha kidogo. Mimi mbali ya kuwa na fani nyingine nyingi pia ni mkereketwa wa mambo ya mazingira. Actually nimesomea uandishi wa habari na mawasiliano ya umma kwa masuala ya mazingira kwa ngazi postgraduate pale Makerere University.
Pia nimesomea masuala ya sheria za kimataifa za mazingira kupitia chuo cha cha mafunzo na utafiti cha Umoja wa Mataifa (UNITAR) cha Geneva, Uswizi.
Pia nimekuwa mwandishi wa habari za mazingira ndani na nje ya nchi (Uganda) kwa zaidi ya miaka 10. Nimekuwa nikiandika habari za kitafiti, makala na hata safu mbali mbali zihusuzo mazingira kwenye magazeti ya ndani na nje. Pia nilikuwa mmoja wa waanzilishi wa kwanza kabisa wa blogs hapa Tanzania na ya kwangu ilikuwa inahusu habari na taarifa za mazingira.
Turudi kwenye mada yetu. Mwaka 1998 baada ya mafuriko ya el nino nilikuwa mmoja wa jopo la waandishi ambao tulizunguka na kamati ya kutathmini athari za mafuriko hayo kwa jiji la Dar es Salaam iliyoundwa na Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya mwenyekiti wake, Prof. Masuha.
Tulizunguka maeneo yote yaliyoathirika ikiwemo Tabata Kisiwani, Jangwani, Kijiji cha Miti Mirefu (Jangwani), Makurumla, Kigogo, Msasani mpaka Msasani Bonde la Mpunga etc. Tuliona jinsi gani shughuli za binadamu zilivyochangia kuleta maafa yale. Kule Jangwani vijumba vidogo vidogo vilivyoanza kuchipuka kimoja kimoja kama kichunguu cha mchwa, viligeuka vijiji vikubwa kabisa! Kule Tabata maghala na viwanda pamoja na nyumba za makazi vilijengwa kwenye mabonde ya mito!
Kama anavyosema Mama Tibaijuka, hali hii iliachwa kuendelea kwa miaka mingi! Watoto walizaliwa na kukulia katika hivi vijiji!Mwaka 2005 Mama Tibaijuka akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Makazi la UN, aliteuliwa na Katibu Mkuu wa UN kuwa mwenyekiti wa kamati ya kwenda kufanya tathmini ya athari kufuatia ubomoaji mkubwa wa nyumba za watu kwenye maeneo ya watu wenye kipato duni(slums) kule Harare, Zimbabwe.
Mara baada ya kukamilisha kazi hiyo, akiwa njiani kurudi Nairobi yalipo makao makuu ya UN Habitat, Mama Tibaijuka kwa kuipenda nchi yake akafanya mkutano na wadau wa mipango miji pale Starlight Hotel Mnazi mmoja ambapo aliitahadharisha Tanzania juu ya hatari ya kushamiri kwa makazi holela nchini akitolea mfano eneo la Bonde la Jangwani hapa Dar es Salaam akitolea mfano yale aliyoyakuta Harare. Kwenye mkutano ule wadau wote muhimu walialikwa wakiwemo maofisa wa serikali wanaohusika na sera na utekelezaji wa mipango miji. Nilipata bahati ya kushiriki kwenye mkutano ule. Alishauri kuwa ni vyema wananchi walioshavamia maeneo haya waondolewe na wale wanaoanza uvamizi wazuie mara moja kabla hawajajihiimarisha humo mabodeni.
Pamoja na hadhari ile, maisha yaliendelea kama kawaida! Hata wale waliopewa viwanja maeneo ya miinuko ili watoke mabondeni wengi wao waliviuza na kurudi kuendelea kuishi mabondeni!
Majengo, viwanda, maghala na hata ofisi za vyama zinaendelea kujengwa na kuzinduliwa huko huko! Unakuta ofisi na tawi la chama limefunguliwa na diwani na hata mbunge!
Sasa hivi karibuni tumeshuhudia hata ofisi za miradi ya serikali nazo zikijengwa humo! Nadhani kila mtu ni shuhuda wa hilo!
Mwanzoni bomoa bomoa ilipoanza niliunga mkono ingawa ilikuwa maumivu kwa wale walioathirika, lengo kuu lingekuwa jema kwa kizazi cha sasa na baadae.
Nilikuwa mmoja wa watu waliohoji sana kuhusu ujenzi ule! Sasa matokeo yake tunayaona!
Emmanuel Kihaule FIRST PUBLISHED KATIKA FB


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO