SERIKALI imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa, Mhandisi Ngusa Izengo kilichotokea jana kwa ajali ya gari.
Taarifa hiyo ya masikitiko imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo wakati akizungumzia  kifo hicho jana.
Taarifa ya ajali hiyo zinasema kwamba gari la Mkurugenzi huyo lililaliwa na lori la mafuta katika eneo la Chalinze Nyama nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Taarifa zaidi zinasema kwamba gari dogo alilopanda Mkurugenzi huyo, lenye namba za usajili T619 DMA aina ya Toyota Crown Athlete, liliangukiwa na lori lililobeba mafuta eneo la Mbande Makaravati.
Ajali hiyo imethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Giles Muroto na kuahidi kutoa taarifa kamili baadae. 
"Nitatoa taarifa kamili zoezi hili uokaji litakapomalizika maana mpaka muda huu tumetoka eneo la tukio tumeshindwa kujua kuna watu wangapi ndani ya gari hilo lililoangukiwa. Tunaenda TAMESA kutafuta 'grinder machine' ili tuweze kujua idadi kamili ya miili iliyopo ndani ya gari",alisema Kamanda Muroto. 
Hata hivyo baadae wasaidizi wa kamanda huyo walisema kwamba shughuli ya kutafuta chanzo cha ajali kilikuwa kinaendelea na kwamba wapo hospitali kwa ajili ya majeruhi.
Inaaminika dereva wa lori amejeruhiwa na amekimbizwa hospitalini.
Taarifa hiyo ya kifo imewasikitisha wakurugenzi wenzake waliomo mkoa wa Dodoma ambao walisifu uchapaji kazi wake na kusema mkoa umeondokewa na mmoja wa watu wanaowajibhika katika nafasi zao.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya chemba Dk Semistatus Mashimba alisema Izengo alikuwa  Mchapakazi, mwenye busara,  upendo kwa watu na mcheshi sana na hakuwa na makuu na jamii itamkosa sana.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa  halmashauri ya Bahi, Rachel Chuwa alisema Ngusa alikuwa kijana mchapa kazi, mpenda watu, mtu mpole, muelewa wa mambo mengi, mcheshi, asiye na majivuno na kusema watamkosa katika utendaji.
“Juzi tu Ijumaa tulikuwa naye katika Kikao cha Kamati ya Sherehe Taifa kilichofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kupanga mikakati ya kufanikisha Sherehe za Muungano wa Tanzania na Zanzibar inayotarajiwa kufanyika 26/04/2018 Dodoma. Alikuwa mzima wa Afya, mwenye kujiamini katika mipango yake ya kuiendeleza Kongwa. “ alisema Chuwa.
Alisema alikuwa amezoeana sana Mkurugenzi wamekuwa wakipigiana sana simu ili kushaurina anamna bora ya kutekeleza maagizo mbalimbali ya serikali na wananchi.
“ Kifo chake kimenisikitisha sana. Alikuwa bado anahitajika na Familia yake, wana Kongwa, Wana Dodoma na Taifa kwa ujumla. Mwenyezi Mungu amrehemu, amsamehe dhambi zake zote na kuilaza mahali pema peponi Roho yake. Tulishirikiana naye, sisi tulimpenda, Mwenyezi Mungu amempenda zaidi. Kalale pema peponi Ngusa, tutakukumbuka kwa mema mengi. Wana Kongwa na Dodoma kwa ujumla tumepotelewa na mtu mwema sana.” Alisema Chuwa.
Ngusa alichaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kongwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli Julai,7, 2016 wakati wa uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji 5, Manispaa 21, Miji 22 na Wilaya (DC) 137 za Tanzania Bara.Aidha aliapishwa Ikulu Dar es Salaam,Jumanne tarehe 12 Julai, 2016 saa tatu asubuhi kwa ajili ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.
Kabla ya uteuzi wake alikuwa msaidizi wa waziri  na pia alishawahi kuwa msaidizi wa Prof Mwandosya
Source:Sifa LubasiHabarileo

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO