TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Aprili, 2018 amezindua Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete na kuahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili kufanikisha malengo iliyojiwekea.
Katika hotuba yake wakati wa halfa ya uzinduzi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo kwa uamuzi wake wa kuanzisha taasisi itakayosaidiana na Serikali ya Tanzania na nchi zingine za Afrika katika kupambana na umasikini na kuboresha maisha ya watu.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo zikiwemo nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa kutoa ushirikiano na kuchangia juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa anaamini kuwa michango hiyo itatumika kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itashirikiana na taasisi zote za kiraia zinazofanya kazi kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi, na ameonya kuwa Serikali haitashirikiana wala kuzifumbia macho taasisi za kiraia zenye malengo ya kuvuruga amani na kuharibu maadili ya Watanzania.
Mhe. Rais Magufuli amemsifu Mhe. Dkt. Kikwete kwa kazi aliyoifanya akiwa Rais, ya kusimamia vizuri mageuzi ya kiuchumi, ujenzi wa miundombinu, uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii hususani afya, elimu na maji, ukuzaji wa demokrasia na kuitangaza vyema Tanzania kimataifa, na ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza juhudi hizo.
“Watanzania tutaendelea kukukumbuka kwa kusimamia ujenzi wa shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma, Hospitali ya Mloganzila, ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, bomba la gesi nakadhalika, kwa hakika umetufanyia mengi sana, tunakushukuru sana na nina hakika mchango wako utaendelea kukumbukwa vizazi na vizazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Dkt. Kikwete amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuzindua taasisi hiyo na amemhakikishia kuwa kama ilivyo katika malengo yake itahakikisha inajikita kusaidia juhudi za Serikali katika sekta ya afya hususani afya ya mama na mtoto, kuwaendeleza na kuwalea vijana kuwa raia wema na wazalendo kwa Taifa, kuboresha kilimo chenye tija, kuendeleza utawala bora na kudumisha amani.
Mhe. Dkt. Kikwete amesema taasisi hiyo itafanya kazi kwa ukaribu na Serikali na kwa kushirikiana na wadau wengine na kamwe haitajihusisha na shughuli za kupingana na Serikali wala kushindana na taasisi nyingine zinazofanya shughuli zao hapa nchini.
Hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Aprili, 2018

 

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO