Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipata maelezo toka kwa Waziri wa Nishati Dkt. Menard kalemani  kabla ya kuzindua mradi wa kuzalisha umeme MW 240 wa Kinyerezi ll eneo la Kinyerezi jijini Dar es salaam leo Aprili 3, 2018 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Aprili, 2018 amezindua mradi wa kuzalisha megawati 240 za umeme kwa kutumia gesi asilia (Kinyerezi II) uliopo Kinyerezi Jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kuzindua mradi huo Mhe. Rais Magufuli amekagua mitambo 6 ya kisasa inayotumia teknolojia mpya na ya kwanza kufungwa Afrika Mashariki iitwayo “Combined Cycle” ambayo inatumia hatua mbili za kuzalisha umeme kwa kutumia gesi na mvuke.
Teknolojia hii itaiwezesha mitambo ya Kinyerezi II kuzalisha megawati 167.82 kwa kutumia gesi asilia na megawati 80.4 kwa kutumia mvuke na mpaka sasa tayari megawati 160 zimeshaanza kuzalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa, megawati 40.2 zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwezi Mei na megawati 48 zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka amesema mradi huu umegharimu Shilingi Bilioni 798, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania ambapo kati ya fedha hizo asilimia 15 zimetolewa fedha taslimu na asilimia 85 zimekopwa kutoka benki za Japan.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Matogolo Kalemani amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuimarisha upatikanaji wa umeme hapa nchini ikiwemo kuhakikisha mradi wa uzalishaji wa umeme wa Kinyerezi II unakamilika, upanuzi wa Kinyerezi I kwa kuongeza uzalishaji umeme kutoka megawati 150 hadi kufikia megawati 335 na kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme megawati 2,100 katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers Gorge) ambayo ikikamilika itaiwezesha nchi kuwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 5,000 za umeme.
Dkt. Kalemani amebainisha kuwa pamoja na kutekeleza miradi hiyo Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza miradi ya usafirishaji na usambazaji wa umeme mkubwa ya Iringa – Dodoma – Singida – Shinyanga (kilovoti 400, kilometa 679), Singida – Arusha – Namanga (kilovoti 400, kilometa 414), Makambako – Songea (kilovoti 220, kilometa 300) na mradi wa umeme vijijini (REA) umevifikia vijiji vipya 4,916 na wateja wapya 874,984.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TANESCO kwa kazi nzuri inayoifanya na amempongeza mkandarasi kampuni ya Sumitomo Corporation kwa kukamilisha mradi wa Kinyerezi II siku 45 kabla ya muda uliopangwa na kuwaajiri Watanzania kwa asilimia 80 ya wafanyakazi wote 2,000 waliopata ajira katika mradi huo.
Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati kuongeza juhudi za kusambaza umeme kwa wananchi ili kuepuka madhara yakiwemo uharibifu wa misitu unaosababisha hekta 400,000 kufyekwa kila mwaka kwa ajili ya kuni na mkaa.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa wizara, idara na taasisi za Serikali kuwasiliana pale kunapokuwa na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo vifaa kukwama bandarini kutokana na kudaiwa kodi ili kuepusha ucheleweshaji na ongezeko kubwa la gharama za miradi hiyo.
Mhe. Rais Magufuli amewaondoa shaka wananchi wa Dar es Salaam kuwa japo Serikali inahamia Dodoma Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuboreshwa na ameitaja baadhi ya miradi kuwa ni ujenzi wa barabara za juu (Flyover), ujenzi wa uwanja wa ndege (Terminal 3), reli ya kisasa (Standard Gauge), bandari, barabara na mradi wa kujenga vizuri eneo la bonde la Msimbazi.
“Hatutalitelekeza Jiji la Dar es Salaam, ninachowaomba endeleeni kuungana na Serikali katika juhudi hizi  za maendeleo na msikubali watu wawashawishi kuvuruga amani kwa kuwa nchi hii ni yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Aprili, 2018

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO