MREMBO anayepamba video mbalimbali, Agness ‘Masogange’ Gerald amefariki dunia leo katika hospitali ya Mama Ngoma, Dar es Salaam.
Masogange amefikwa na mauti ikiwa zimepita siku 17 tangu amalize kesi yake ya kutumia dawa za kulevya.
Mwishoni mwa mwaka jana, Masogange na baadhi ya wasanii wengine walituhumiwa kwa matumizi ya dawa za kulevya ambapo Aprili 3 mwaka huu, Mahakama ya Kisutu ilimtia hatiani mrembo huyo ambapo alihukumiwa jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni 1.5. Alilipa faini na kuwa huru.
Habari za kifo chake Masogange zilianza kusambaa saa 11 jioni kupitia kwa wasanii mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii.
Wakili wa msanii huyo, Ruben Semwanza maarufu 'Kinara' aliithibitishia HabariLeo juu ya kifo cha msanii huyo ambaye alitamba kwenye video mbalimbali za wasanii wa bongo fleva.
"Ni kweli Masogange hatunaye, amefariki nusu saa iliyopita (saa 11:00) jioni, nimepigiwa simu hapa na ndugu zake, nipo njiani naelekea kwa Mama Ngoma," alisema Semwanza.
Taarifa zisizo rasmi zinasema kuwa msanii huyo alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na juzi alipelekwa hospitali ya Mama Ngoma baada ya kupanda, kabla ya kufikwa na umauti.
Wasanii mbalimbali walionesha kushtushwa na msiba huo na wengi wao wakionekana kutoamini kama kweli ‘Video Queen’ huyo ameaga dunia.Mwenyekiti wa bongo movie, Steven Mengele 'Nyerere'  akizungumzia kifo cha Masogange, alisema "Umeondoka bado mdogo sana, naamini ndo kwanza ulikuwa kwenye vita ya mafanikio yako, hakika duniani tunapita."
Naye Aunt Ezekiel alisema, "Aggy, umeamua kumuacha mtoto wako? Siamini, Mungu mkali sana aiseee, hakika kila nafsi itaonja umauti, naumia, Mungu ametuweza, kifo fumbo kubwa mno."
Kwa upande wa Jokate Mwegelo alisema, "Nimeamini kifo kipo, Mungu ni mkali aiseee, duniani tuishi vizuri tu, hapa si makao yetu, tangulia Aggy nasi tunakuja."
Msanii Belle 9 aliposti picha ya mshumaa kuonesha ishara ya kuomboleza kifo cha video queen huyo ambaye ndiye aliyemtambulisha kwenye ulimwengu wa muziki baada ya kumshirikisha kwenye wimbo wake wa Masogange na ndipo jina la Agness Masogange liliposhika chati.
Masogange ambaye alitambuliwa kwa umbo lake  tata hasa sehemu za makalio...Umaarufu wake ulianza baada ya kutokea kwenye wimbo huo wa Bel 9.
Source: Na Vicky Kimaro, HabariLeo

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO