Timu ya soka ya Mgomba ya wilayani Rufiji imetwaa ubingwa wa Siro Super Cup 2018 kwa kuifunga Mjawa ya wilaya ya Kibiti kwa penati 11-10 mchezo.

Mchezo huo uliopigwa uwanja wa Samora wilayani Kibiti ambapo mgeni rasmi alikuwa ni mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ulikuwa mzuri na ushindani mkubwa.  

Timu hizo hadi zinamaliza muda wa kawaida wa dakika 90 zilishindwa kufungana na kufanya matokeo kuwa 0-0 ndipo zikaingia hatua ya matuta ambapo Mgomba walipata penati zote na Mjawa ambapo walikuwa wenyeji wakikosa penati moja.

Kutokana na ushindi huo Mgomba walijinyakulia kiasi cha shilingi milioni moja,kombe,seti ya jezi na medali huku Mjawa wakijinyakulia kiasi cha shilingi 500,000 seti ya jezi na medali na mshindi wa tatu timu ya Mipeko kutoka wilaya ya Mkuranga wakijinyakulia 300,000.

Mfungaji bora Dickson Mhilu alijinyakulia mpira huku mwamuzi bora akijinyakulia jezi kwenye mashindano hayo yaliyokuwa na kauli mbiu ya Kibiti salama Jamii salama.

Ndikilo alisema kuwa mashindano hayo yameleta hamasa kwa vijana na jamii huku malengo makuu yakiwa ni kuhamasisha jamii kuishi kwa amani na kufichua uhalifu.

Alisema kuwa mashindano hayo yamedumisha upendo na kuondoa tofauti na kuzifanya wilaya tatu za Kibiti,Mkuranga na Rufiji kushirikiana na kuonyesha mshikamano wa hali ya juu.

Mashindano hayo ambayo yalianza mwezi Aprili yaliandaliwa na Inspekta wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Siro na kushirikisha kata 54 za wilaya hizo za kanda Maalumu ya Kipolisi.


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO