" Ingawa Jamal Khashoggi ni mmoja tu kati ya waandishi 70 waliouawa mwaka huu, Taarifa zinazogusa mamlaka, watu wenye fedha, mak...
" Ingawa Jamal
Khashoggi ni mmoja tu kati ya waandishi 70
waliouawa mwaka huu, Taarifa zinazogusa mamlaka, watu wenye fedha, makundi
yenye fedha, watawala wababe, magenge ya dawa za kulevya rushwa binafsi na za
kimakundi hazijawahi kumwacha mwandishi
wa habari salama."
Na Mwandishi wetu, Mashirika ya kimataifa
KILA kazi duniani hapa ina hatari zake, wakati hatari nyingi
ya kazi za kawaida ni ajali, kazi ya uandishi wa habari haina ajali, yenyewe
ina mauaji na jela nadra sana kupotea bila kuonekana.
Katika siku za karibuni, watu wamepata kujua madhara ya
kufanyakazi ya habari na kupishana na mamlaka kutokana na kupotea na kujulikana
baadaye kwamba mwandishi wa habari Jamal Khashoggi ameuawa.
Katika shauri la
Khashoggi, mamlaka za Saudi Arabia zimekiri kwamba mwandishi huyo aliuawa ndani ya ubalozi wake
mdogo uliopo Istanbul, Uturuki.
Khashoggi (59) ambaye huenda alikuwa akisakwa kwa muda mrefu
aliingia katika ubalozi wa Saudia kupata hati inayomuonesha kwamba ametaliki
ili aweze kuoa tena. Mwandishi huyo ambaye kalamu yake ilikuwa inaonekana
katika gazeti la Washington Post ilidaiwa na mamlaka za Saudia kwamba alikufa katika mapigano ya ngumi ndani
ya ubalozi huo, lakini hawakusema mwili wake upo wapi.
Mrithi wa ufalme wa Saudia , Mohammed bin Salman alisema hivi
karibuni kwamba kifo cha mwandishi huyo kinaleta simanzi kubwa na kwamba haki
itatendeka.
Staili iliyotumika kumpoteza Khashoggi, kwa wale wanaosoma
hadithi na pia ripoti mbalimbali katika maeneo ambayo waandishi wapo katika
hatari kubwa Amerika ya Kusini na Asia wataona kwamba ni ile ile ya kujaribu kupoteza ushahidi.
Hapa palikuwa na mtu anayefanana na Khashoggi ambaye aliondoka
kutoka katika ubalozi huo kuonesha kwamba Khashoggi aliondoka kwa matakwa yake
kumbe alikuwa ni ‘feki’ wakati Khashoggi mwenyewe ameshauawa.
Mamlaka zinadai kwamba alikufa wakati akinyamazishwa, alipoanza
kuleta fujo za kuomba msaada alipoambiwa anapelekwa katika nyumba salama.
Kuna maswali mengi katika kifo cha mwandishi huyu kama katika
vifo vya waandishi wengine. Mwaka huu pekee waandishi 70 wameshauawa katika
pande tofauti za dunia.
Taarifa ya International Press Institute (IPI) kuhusu vifo vya
waandishi wa habari na watu wanaohusiana na
vyombo vya habari (wafanyakazi) (IPI Death Watch) ambavyo vifo vyao
vimeunganishwa katika sababu za uandishi wa habari imefikia 70. Kwa kawaida
orodha hii huingia watu tu waliouawa kwa sababu ya kazi zao au kwa sababu wao
ni waandishi wa habari.
Katika orodha hiyo mwaka
huu ambao haujamalizika idadi ya
vifo ni 70kubwa kwani, mwaka jana walikuwa 82. Katika orodha hii kuanzia mwaka
2004 mwaka mbaya kabisa ulikuwa mwaka 2012 ambapo idadi ya waandishi waliouawa
ilikuwa 133.Orodha hiyo imechapisha kuwa mwaka: 2018 vifo 70 ; 2017 vifo 82 ; 2016 vifo 120; 2015 vifo 115;
2014 vifo 99; 2013 vifo 121 ;2012 vifo 133;2011 vifo 102; 2010 vifo 101; 2009 vifo
110 ; 2008 vifo 66 ; 2007 vifo 93;2006 vifo 100;2005 vifo 65 ; 2004 vifo 78;2003
vifo 64 ; 2002 vifo 54 ; 2001 vifo 55 ; 2000 vifo 56 ; 1999 vifo 86 ;1998 vifo 50
na 1997 vifo 28 .
Wakitoa ufafanuzi watu wa IPI wanasema idadi ya waandishi waliokufa
katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu ilifikia 49.Waandishi 22 wakiwemo
waandishi 11 wa Afghanistan na wawili Palestina wameuawa kwa kutoa hadharani
taarifa za uhalifu unaofanywa kimakundi na rushwa. Mauaji mengine 18 bado
yanachunguzwa sababu ingawa ushahidi wa kimazingira unabaki ni mauaji yenye
lengo la kuondoa ushahidi baada ya kufichuliwa kwa uhalifu wa kimakundi na
rushwa.
Waandishi wanne waliuawa wakati wakiandika habari katika maeneo
yenye migogoro na wengine watano
walikufa wakiwa kazini. Kati ya waandishi waliokufa 49, wanne walikuwa
wanawake.
Uchambuzi kuhusiana na
vifo hivyo zinaonesha kwamba yalikuwa mauaji ya kukusudiwa na upelelezi wake
umekuwa ukienda taratibu huku wengi wa wahusika bado kufikishwa mahakamani.
Mkuu wa Uragibishi wa IPI , Ravi R. Prasad anasema vifo hivyo vinahitaji
kuchunguzwa haraka ikiwa jamii inataka kulinda uhuru wa vyombo vya habari na
upashanaji habari.
Februari 22 mwaka huu polisi walipata mwili wa mwandishi Ján
Kuciak, anayeandikia mtandao wa Aktuality.sk, na mchumba wake nyumbani kwao
Slovakia. Kuciak alikuwa anaandika habari za uchunguzi kuhusu rushwa serikalini
ambapo taarifa zake zilihusisha watumishi wa serikali ya Slovak na makundi ya
kihalifu ya Mafia yaliyopo Italia.
Taarifa hizo za uchunguzi zilichapishwa baada ya kifo chake. Mauaji
hayo yalisababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Slovak , Robert Fico: Imeelezwa kuwa serikali ya Slovak imeendelea
kuchunguza kadhia hiyo.
Nchini India uchunguzi unaendelea wa vifo vya waandishi wa
habari wanne vilivyotokea katika pande tofauti za nchi hiyo. Kwa mujibu wa
vyombo vyao vya habari waandishi hao walikuwa wakichunguza rushwa. Watu waliomuua
Mhariri Mkuu wa Rising Kashmir, Syed
Shujaat Bukhari, ambaye aliuawa Juni 14
mwaka huu, nje ya ofisi yake wametambulika lakini bado kusimamishwa kizimbani.
Mauaji ya waandishi wa habari nchini India, Brazil, Guatemala,
Philippines, Afghanistan, El Salvador na Pakistan pia yanasubiri uchunguzi. Eneo
baya kabisa la mauaji kwa mwaka huu ni Afghanistan ambako waandishi wa habari
tisa wameuawa kwa bomu la kutegwa Aprili 30.Waliuawa wakati wakiandika habari
za bomu jingine la kutegwa lililolipuka.
Waandishi wengine wawili waliuawa kwa risasi wakielekea kazini.
Waandishi saba waliuawa nchini Mexico tangu kuanza mwaka huu. Mexico ni nchi ya
pili hatari kwa maisha ya waandishi wa habari duniani. Mathalani mwishoni mwa
Juni mwandishi mwingine wa Mexico aliyetambuliwa kwa jina la José Guadalupe Chan Dzib aliuawa.
India na Marekani zinakuwa nchi za tatu hatari kwa kazi ya
uandishi wa habari wakiwa na mauaji ya waandishi wanne kwa mwaka huu kila
mmoja. Nchini Marekani waandishi wanne na mfanyakazi mmoja wa Maryland’s
Capital Gazette waliuawa kwa kumiminiwa risasi hapo Juni 29 mwaka huu.
Mwaka jana kwa mujibu wa IPI, ndio ulikuwa mwaka nafuu ambapo
waandishi wa habari 82 waliuawa na kufanya kuwa mwaka pekee ambapo waandishi
waliouawa idadi yake ikiwa ni chini ya 100.
Mazingira ya kisiasa na kiuchumi duniani kwa sasa inafanya waandishi
wa habari kuwa katika hali ngumu zaidi hasa wale ambao wanapingana na mamlaka
au kuingilia maslahi binafsi ya kimakundi hasa katika masuala ya rushwa,
upindishaji wa ukweli na uhalifu binafsi
na wa kimakundi.
Kwa kuangalia mazingira haya watu wa Reporters Without Borders
(RSF) wamekuwa wakiutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kulinda usalama wa
waandishi wa habari kwa kuwa na mwakilishi maalumu wa kada hiyo Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa Reporters Without Borders (RSF) katika kipindi
cha miaka 10 iliyopita zaidi ya waandishi 700 wameuawa wakitekeleza kazi zao.
Miaka mitatu iliyopita, Mwaka 2015, World Press Freedom Index ilionesha
kwamba hali ya uhuru wa vyombo vya habari inazidi kuporomoka duniani huku
theluthi mbili za nchi 180 zilizofanyiwa utafiti zikiwa na hali mbaya zaidi kuliko
mwaka uliotangulia.
Mwaka huo uliotangulia ( 2014) mauaji ya kupangwa dhidi ya
waandishi yalifanyika na wengine walikatwa vichwa. Nchi ambazo zilikuwa na
mauaji mengi ni Syria, Palestina, Ukraine, Iraq na Libya. Mwaka huo huo
waaandishi wa habari 119 walitekwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 la mwaka
2013 hasa kwa waandishi wa habari wenyeji wa Ukraine, Libya, Syria, Iraq na
Mexico.
Wakati wakiandika ripoti ya mwaka 2015 RSF walisema kwamba tangu
kuanza kwa mwaka 2015, waandishi wa habari 48 waliuawa, wanane nchini Ufaransa,
sita Sudan kusini, watano Yemen, watano Iraq,
watano Syria, watatu Mexico na watatu Brazil. Ripoti hiyo haikugusa
miezi ya kumalizika mwaka 2015.
Taarifa zinazogusa mamlaka, watu wenye fedha, makundi yenye
fedha, watawala wababe, magenge ya dawa za kulevya rushwa binafsi na za
kimakundi hazijawahi kumwacha mwandishi
wa habari salama. Kwa waandishi wa habari, kazi hii ni sawa na kuwa askari
jeshi ambaye anatarajia muda wowote ule kufa au kupata madhara kutokana na
kalamu yake hasa jamii inapokuwa na uhalifu wa kimakundi, rushwa na misimamo
mikali ya kimamlaka na wakati mwingine kiutamaduni.
COMMENTS