MAELEZO YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI K...
MAELEZO YA
MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA
MAPINDUZI KUHUSU UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CHAMA CHA MAPINDUZI YA MWAKA 2020 KWA KIPINDI CHA
NOVEMBA 2020 HADI OKTOBA 2022
Ndugu Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Ndugu Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi;
Ndugu Abdulrahman Omari Kinana, Makamu Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi Bara;
Ndugu Daniel Godfrey Chongolo, Katibu Mkuu wa
Chama cha Mapinduzi;
Ndugu Dkt. Philip Isdor Mpango, Mjumbe wa Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Ndugu Hemed
Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;
Ndugu Christina
Solomon Mndeme, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Bara;
Ndugu Dkt.
Abdallah Juma Saadala, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar;
Ndugu Wajumbe
wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa;
Ndugu Viongozi Wastaafu
wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Ndugu zetu
Wenza wa Viongozi mliopo hapa;
Ndugu Wajumbe
kutoka Vyama vya Siasa Rafiki; na
Waheshimiwa
Mabalozi kutoka nchi mbalimbali mliopo hapa;
Mabibi na
Mabwana.
KIDUMU CHAMA
CHA MAPINDUZI
UTANGULIZI
1. Ndugu
Mwenyekiti, ninaomba kuanza maelezo yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa
kutufikisha siku hii ya leo tukiwa salama na wenye afya njema.
2. Ndugu
Mwenyekiti, leo tunaandika historia nyingine ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kupitia Mkutano Mkuu huu wa 10 kwa kuwa kikao hiki ni cha kwanza kupokea
Taarifa za Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya
Mwaka 2020.
3. Ndugu
Mwenyekiti, Ilani
tunayoitekeleza ni ya mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo
ya mwaka 2025 ambayo CCM imeielekeza Serikali kutekeleza maeneo makuu sita ya
kipaumbele yafuatayo: -
Mosi: Kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa,
haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu;
Pili: Kukuza uchumi wa kisasa,
fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma
za kiuchumi na miundombinu wezeshi;
Tatu: Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na
uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na
kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi;
Nne: Kuimarisha upatikanaji wa huduma bora
za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini;
Tano: Kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi,
teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi;
na
Sita: Kutengeneza ajira zisizopungua
8,000,000 katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.
UTEKELEZAJI WA ILANI (NOVEMBA 2020 HADI OKTOBA
2022)
4. Ndugu
Mwenyekiti, taarifa hii itabainisha hatua iliyofikiwa na Serikali katika utekelezaji
wa Ilani kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Oktoba 2022. Wasilisho hili ni
muhtasari wa taarifa ya kina iliyopo katika vitabu viwili vikubwa ambavyo kila
mmoja wetu amepatiwa. Taarifa hizo zimegusa maeneo mbalimbali ikiwemo: Afya,
Elimu, Maji, Utalii, Kilimo na Umwagiliaji, Miundombinu ya Barabara, Reli,
Madaraja, Bandari, Viwanja vya Ndege na Ukusanyaji wa Mapato.
5. Ndugu Wajumbe, ninaungana na
wenzangu kukupongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa kupata Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa kutokana na mafanikio
yako katika mageuzi ya kiuchumi, uimarishaji wa misingi ya demokrasia, utawala
bora na maendeleo ya jamii.
6. Ndugu
Mwenyekiti, mchango wako katika kuliongoza Taifa hili kwa weledi, ukomavu na kujenga
matumaini mapya kwa Watanzania umeleta chachu mpya ya kulijenga Taifa letu na
kusaidia tupate mafanikio ya haraka.
7. Ndugu Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wa
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, mafanikio makubwa na ya haraka yamepatikana
katika nyanja na sekta zote. Ninaomba
kutumia nafasi hii kuwaeleza kwa kifupi baadhi ya mafanikio.
a)
Ukusanyaji wa
Mapato
Ndugu Mwenyekiti, Serikali ilianza utekelezaji wa Mpango wa
Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026) ukiwa na
dhima ya Kujenga Uchumi Shindani wa Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Chini
ya uongozi wako mahiri na kuhimiza ulipaji kodi kwa hiari, ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeendelea kuongezeka hadi kufikia
wastani wa shilingi
trilioni 1.74 kwa mwezi ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.46 kwa mwezi mwaka 2020/2021. Aidha, hadi Agosti, 2022 mfumuko wa bei
umeendelea kudhibitiwa na kubaki kwenye
tarakimu moja.
b)
Elimu
Ndugu
Mwenyekiti, katika kutekeleza Ilani ya CCM, Serikali yako imeendelea kutekeleza mpango
wa kutoa elimu ya msingi na sekondari bila ada ikiwemo ada za mitihani na hivyo
kuimarisha uandikishaji na uhitimu wa wanafunzi shuleni.
Ndugu Mwenyekiti, ni
jitihada zako zilizowezesha kupatikana fedha za kujenga vyumba vya madarasa 12,000
katika shule za sekondari, vyumba vya madarasa 3,000 katika vituo
shikizi na kufanya uandike historia mpya katika nchi hii ambapo kwa mara ya
kwanza, wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa saba mwaka 2021 walipata
nafasi ya kuanza kidato cha kwanza Januari, 2022 bila kuwa na chaguo la pili.
Ndugu
Mwenyekiti, ujenzi wa shule za wasichana katika mikoa yote 26 zenye uwezo
wa kuchukua wanafunzi kati ya 1,000 na 1,200 ambao watakuwa wanasoma masomo ya
sayansi ni mpango mkakati wa kuongeza fursa kwa watoto wa kike nchini. Nitumie
nafasi hii kukushukuru kwa kuridhia kutenga shilingi bilioni nne kwa kila shule kwa mikoa 10 ya kwanza nchini katika bajeti ya mwaka huu na
ujenzi unaendelea.
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kugharamia elimu ya juu ambapo katika kipindi cha
Novemba 2020 hadi Oktoba 2022, imetoa mikopo ya shilingi trilioni 1.03
kwa wanafunzi 327,175 wa vyuo vya elimu ya juu.
c)
Kilimo na
Huduma za Ugani
Ndugu Mwenyekiti, ili kuimarisha
sekta ya kilimo, umefanya maamuzi ya kimapinduzi kwa kuridhia ongezeko la
bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi shilingi
bilioni 954 kwa mwaka 2022/2023. Tarehe 4 Aprili, 2022 hapa hapa mkoani
Dodoma, ulikabidhi vitendea kazi kwa maafisa ugani wote nchini zikiwemo
pikipiki 2,000, vifaa vya kupima afya ya udongo 143, simujanja 384 na visanduku
vya ufundi 3,400 vya maafisa ugani. Aidha, ili kuhakikisha upatikanaji wa
mbolea na kuongeza tija katika uzalishaji kwa wakulima, uliridhia ruzuku ya shilingi bilioni 150
ili isaidie kushusha bei ya mbolea na kwa sasa usambazaji unaendelea kwa wakulima
katika maeneo mbalimbali nchini.
d)
Kukuza
Demokrasia
Ndugu
Mwenyekiti, demokrasia popote pale
duniani huwa ina misingi na taratibu ambazo Taifa husika limejiwekea. Dhamira
yako ya dhati ya kuweka mazingira mazuri ya demokrasia na siasa hapa nchini,
imejidhihirisha kupitia sera
ya upatanishi, kuvumiliana, kuishi pamoja na kujenga nchi uliyoipa jina la R4
yaani Reconciliation, Resiliency,
Reforms and Rebuilding of the nation. Hii imejenga
mazingira ya demokrasia nzuri na inayoendana na hali halisi ya Kitanzania.
Ndugu Mwenyekiti, tarehe 21 Oktoba 2022 ulipokea taarifa ya Kikosi Kazi ambayo imebainisha
masuala mbalimbali yakiwemo yanayohusisha kutungwa kwa sheria mpya, marekebisho
ya sheria mbalimbali na kanuni. Serikali inafanyia kazi masuala hayo kwa
kuzingatia mpango kazi na hatua za mapitio ya ngazi za maamuzi
ndani ya Serikali.
e) Uhusiano wa
Kimataifa
Ndugu
Mwenyekiti, tangu uingie madarakani, umeimarisha uhusiano na mataifa mengine
zikiwemo nchi jirani hususan za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Kutokana na juhudi zako, baadhi ya Marais
na Wakuu wa Nchi waliotembelea Tanzania ni Waheshimiwa Yoweri Museveni
(Uganda), Felix Tshisekedi (Jamhuri Kidemokrasia ya Congo), Filippe Nyusi
(Msumbiji), Evariste Ndayishimye (Burundi), Hakainde Hichilema (Zambia) na
William Ruto (Kenya). Aidha, wewe binafsi umefanya ziara katika nchi za
Marekani, Ubelgiji, Ufaransa, Qatar, Uganda, Ghana, Uingereza, Msumbiji, China,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu,
Scotland, Malawi, Rwanda na Burundi.
8. Ndugu Mwenyekiti, maelezo ya kina kwa maeneo yote
haya yamewasilishwa kwenye makala fupi ambayo ninaomba wote sasa tuitazame:-
A.
UCHUMI
Ukusanyaji wa Mapato
Ndugu Mwenyekiti, ukusanyaji wa mapato umeongezeka ambapo kwa
kipindi cha mwaka 2021/2022 wastani wa mwezi ulikuwa ni shilingi trilioni
1.74 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.46 kwa mwaka 2020/2021.
Ndugu Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili
kuvutia uwekezaji katika viwanda vitakavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini
ili kukuza pato la mwananchi, kupunguza umasikini na kuongeza ajira. Baadhi ya
viwanda vilivyozinduliwa hivi karibuni ni kiwanda cha kuzalisha sukari cha
Bagamoyo, kiwanda cha kusafishia madini ya dhahabu cha Geita, na kiwanda cha
kuchambua pamba cha NGS, Ifukutwa, kilichopo wilaya ya Tanganyika, mkoani
Katavi.
Uzalishaji wa Ajira
Ndugu Mwenyekiti, moja
ya ahadi ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020 ni kuzalisha ajira zipatazo milioni
nane katika kipindi cha miaka mitano. Katika kutekeleza Programu ya Kukuza
Ajira kwa Vijana ambayo ni jumuishi katika sekta zote, kuboresha mazingira ya
uwekezaji, kutekeleza miradi ya kimkakati, kutoa mafunzo ya ujuzi na kutoa
mikopo yenye masharti nafuu, ajira 1,381,618 zimezalishwa kwa Watanzania
kupitia sekta ya umma na binafsi.
Ndugu
Mwenyekiti, vilevile, Serikali imehakikisha miradi ya kimkakati inayotekelezwa
nchini inatoa ajira, kuwanufaisha wazawa na kuwajengea uwezo ili kukidhi vigezo
vya ajira hizo. Jitihada hizo zimewezesha miradi ya kimkakati kutoa ajira za
moja kwa moja kwa vijana 97,832 na zisizo za moja kwa moja 377,000
kwa vijana wenye ujuzi mahiri, ujuzi wa kati na wasio na ujuzi.
B.
MIUNDOMBINU
Barabara na
Madaraja Makubwa
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha barabara na ujenzi wa madaraja makubwa
ili kurahisisha usafiri na usafirishaji. Kipindi cha Novemba, 2020 hadi Oktoba,
2022 Serikali imejenga mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita
950.29. Aidha, Serikali iliendelea na ujenzi na matengenezo ya barabara mijini
na vijijini zenye urefu wa kilomita 50,373.23 ambapo barabara za
kiwango cha changarawe ni kilomita 9,989.36 na matengenezo ya kawaida na
sehemu korofi ni kilomita 22,045.68.
Ndugu
Mwenyekiti, vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa madaraja makubwa ya
Kitengule (Kagera), Daraja Jipya la Wami (Pwani), Daraja la Msingi (Singida) na
Daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza). Ujenzi wa Daraja la Tanzanite (Dar es
Salaam) na Daraja la Kiyegeya (Morogoro) umekamilika.
Ndugu Mwenyekiti, mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha
Kimataifa (SGR) unaendelea na hadi kufikia Novemba, 2022 kipande cha Dar es
Salaam – Morogoro (Km 300) kimefikia asilimia 97.49 na Morogoro –
Makutopora (km. 422) asilimia 90.07, Mwanza – Isaka (km. 341) asilimia
14.2 na Makutupora – Tabora (km. 368) asilimia 1.92 ilhali ujenzi
wa kipande cha Tabora - Isaka chenye urefu wa km. 165 umeanza. Utengenezaji
wa mabehewa unaendelea vizuri. Kati ya mabehewa 81, mabehewa 36 yamekamilika na
14 kati ya hayo yaliwasili bandari ya Dar es Salaam tarehe 22 Novemba, 2022.
Mabehewa 45 yaliyobakia, yanategemewa kukamilika Machi, 2023.
Bandari
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali inaendelea na hatua
mbalimbali za upanuzi wa bandari za Dar es Salaam na Tanga na katika Ziwa
Tanganyika kwenye bandari za Kibirizi (Kigoma), Karema (Katavi) na Kabwe Mkoani
Rukwa ili kuongeza ufanisi katika huduma. Hadi Oktoba 2022, ujenzi wa gati 1-7
katika Bandari ya Dar es Salaam unaohusisha kuongeza kina, kujenga Gati Maalumu
(RoRo berth) ya kuhudumia meli za magari na kujenga yadi ya kuhudumia makasha (container
yard) umekamilika. Vilevile, Serikali imeboresha bandari ya Tanga kwa
kuongeza kina cha lango la kuingilia na kugeuzia meli.
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali imeendelea na upanuzi
wa bandari ya Kibirizi (Kigoma) ili kuchochea biashara na nchi jirani za Congo
(DRC), Zambia na Burundi. Pia ujenzi wa bandari ya Kabwe Mkoani Rukwa
umekamilika, na utakuwa kivutio kikubwa cha biashara baina ya Wilaya ya Nkasi
na eneo la Moba nchini Congo.
Ndugu
Mwenyekiti, pia ujenzi wa bandari ya Karema iliyopo mkoani
Katavi umekamilika na imeanza kutumika. Ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 47.9, ukihusisha ujenzi wa kivunja mawimbi, mlango
bandari na gati ya meta 150 zenye uwezo wa kulaza meli zenye urefu wa mita 75
na upana wa mita 15, uchimbaji na uwekaji wa kina wa mlango wa bandari, jengo
la ofisi, jengo la abiria na shehena ya jumla.
Usafiri wa Anga
Ndugu
Mwenyekiti, katika sekta ya anga, Serikali imeendelea na uboreshaji wa viwanja vya
ndege vya Songea mkoani Ruvuma na Nduli mkoani Iringa. Kwa uwanja wa ndege wa
Songea, ujenzi na ukarabati wa jengo la kuongozea ndege upo katika hatua za
mwisho na wanakamilisha uwekaji wa taa ili kuwezesha ndege kutua usiku. Katika
kiwanja cha ndege wa Nduli, upanuzi wa kiwanja hicho unahusisha ujenzi wa
barabara za kutua na kurukia ndege.
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili
liweze kutoa huduma bora ya usafiri wa anga ndani na nje ya nchi. Hivi sasa
limefanikiwa kuanza safari za Arusha, Geita, na kurejesha safari za Mtwara na
Songea. Pia, limerudisha safari za kikanda katika vituo vya Bujumbura, Entebbe,
Harare, Lusaka na Hahaya pamoja na kuanzisha vituo vipya vitatu katika miji ya
Lubumbashi, Nairobi na Ndola. Vilevile, Shirika limerejesha safari ya kimataifa
kwenda Mumbai - India pamoja na kuanzisha safari za mizigo na abiria kuelekea
Guangzhou – China.
Ndugu
Mwenyekiti, ili kuboresha usafiri wa majini, Serikali inaendelea na ujenzi wa Meli
ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ambao
umefikia asilimia 73. Pia ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria 600 na tani 400
za mizigo katika Ziwa Tanganyika na meli mpya ya kubeba mabehewa (wagon
ferry) katika Ziwa Victoria unaendelea.
C.
NISHATI
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua madhubuti kuimarisha sekta ya nishati ili
kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali. Hatua hizo
zilijumuisha kuendelea na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere
(Julius Nyerere Hydro Power Project - JNHPP) ambao umefikia asilimia 77.15 na
unatarajia kuzalisha MW 2,115.
D.
KUKUZA UTALII
Uzinduzi wa filamu ya ROYAL TOUR
Ndugu
Mwenyekiti, utalii ni sekta muhimu ya uchumi yenye mchango mkubwa katika Pato la
Taifa. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kulinda na kuhifadhi
rasilimali na kuendeleza utalii nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu
ya utalii, kuongeza na kutangaza vivutio vya utalii.
Ndugu
Mwenyekiti, takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa sekta ya utalii inazidi kuimarika
zaidi hususan baada ya uzinduzi rasmi wa programu maalumu ya The Royal
Tour uliofanyika tarehe 19 Aprili, 2022 nchini
Marekani. Na hadi kufikia
Septemba 2022, takwimu zinaonesha kuwa watalii wanaokuja nchini Tanzania
wameongezeka kutoka 922,692
mwaka 2021 na kufikia 1,034,180.
Pia, mapato yatokanayo na utalii
yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka dola za Marekani milioni
714.59 (sawa na shilingi trilioni 1.6) kwa mwaka 2020 na
kufikia dola za Marekani bilioni 1.3 (sawa
na shilingi trilioni 3) katika mwaka 2021.
Ndugu
Mwenyekiti, Novemba 2022, Tanzania ilipokea meli kubwa ya kitalii ya Zaandam kutoka
Florida, Marekani ikiwa na watalii 1,060
kutoka mataifa ya Marekani na Ulaya na wafanyakazi 520
kutoka mataifa 35 duniani. Vivutio
vya utalii tulivyonavyo vimeifanya sekta hii kuwa mhimili muhimu wa uchumi na
sasa Tanzania imeanza kuwa kitovu cha utalii wa mikutano (conference
tourism) ambapo hivi
karibuni tumeweza kuwa wenyeji wa Mkutano
wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani - Kamisheni ya Afrika.
Pia tulikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF). Mikutano hii ilifanyika jijini Arusha.
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali
itaendelea kuongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa na kuibua
masoko mapya ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini
hadi kufikia watalii milioni tano
na mapato ya dola za Marekani bilioni sita
ifikapo mwaka 2025.
Kulinda Hifadhi ya Ngorongoro
Ndugu
Mwenyekiti, ili kulinda ikolojia na uoto wa asili katika Eneo la Hifadhi ya
Ngorongoro (NCA), Serikali imefanikiwa kuwaratibu wakazi wanaohama kwa hiari katika eneo la
hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga. Zoezi la kuandikisha wakazi wanaoomba kuhama kwa hiari linaendelea
vizuri. Aidha, hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2022 jumla ya kaya 1,524
zenye watu 8,715 na mifugo 32,842 zilikuwa zimekwishajiandikisha.
Aidha, kati ya tarehe 16 Juni, 2022 na tarehe 15 Novemba, 2022 makundi 16
yenye kaya 489 zenye watu 2,629 na mifugo 14,132 zilikuwa
zimeshahamia katika kijiji cha Msomera, wilayani Handeni. Katika maeneo ambayo wakazi
hao wamehama kwa hiari, uoto umeanza kurejea katika hali ya awali huku wanyama
wakiongezeka na watalii wanaotembelea eneo hilo pia wameongezeka.
E. MAJI
Miradi Mikubwa Mitano
Ndugu
Mwenyekiti, katika kuimarisha sekta ya maji nchini, Serikali imetekeleza miradi
mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama. Hadi kufikia Oktoba
2022, ujenzi wa miradi mikubwa mitano ya Tabora-Igunga-Nzega; Orkesumet;
Kagongwa-Isaka; Longido na Misungwi ilikuwa imekamilika. Aidha, vijiji 171
vilivyopo kandokando ya miradi hiyo, vilikuwa vimeunganishwa na huduma ya maji.
Miradi ya Maji katika Miji 28
Ndugu
Mwenyekiti, tarehe 6 Juni 2022, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
alishuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maji ya miji 28. Miji
itakayonufaika na miradi hiyo ni Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani,
Kilwa-Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Chunya, Rujewa, Wangingo’mbe, Makambako,
Njombe, Kiomboi, Singida, Manyoni na Chemba. Miji mingine ni Chamwino, Mugumu,
Kasulu, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Geita, Chato, Mafinga pamoja
na ukanda wa Makonde. Utekelezaji wa miradi hiyo
ni mojawapo ya mikakati ya Serikali ya kusambaza maji safi na salama maeneo ya
mijini na vijijini. Aidha, kiwango cha upatikanaji wa majisafi na salama
mijini kimeongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2020 hadi asilimia 86 mwaka 2022
na vijijini kutoka asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 74.5 mwaka 2022.
Ndugu
Mwenyekiti, mwaka huu,
umeandika historia mpya kwa kuridhia zitolewe shilingi bilioni 100 kati
ya shilingi bilioni 329 ili kuanza utekelezaji wa mradi huu muhimu unaotarajiwa
kuchukua miezi 36 hadi kukamilika. Pamoja na mradi huu, Serikali inaendelea na
taratibu za awali za ujenzi wa Bwawa la Farkwa kwa gharama ya shilingi
bilioni 292 ili kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma na miji ya Bahi, Chemba na Chamwino.
F. KUHAMIA DODOMA
Awamu
ya Pili ya Ujenzi wa Mji wa Serikali
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali ilifanya uamuzi wa kuhamishia
Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma. Ili kutimiza azma hiyo, shilingi bilioni
300 zilitolewa kwa ajili ya awamu ya pili
ya ujenzi wa Mji wa Serikali unaohusisha majengo ya ofisi yenye
urefu wa ghorofa kuanzia sita hadi 11 ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha Serikali inahamishia shughuli zake Makao
Makuu ya nchi jijini Dodoma.
Ndugu
Mwenyekiti, ujenzi huo ambao umefikia asilimia kati ya 50 na 70, unatarajiwa
kukamilika Oktoba, 2023 na utaenda sambamba na uwekaji wa miundombinu ya maji,
umeme, mawasiliano, usalama, gesi, TEHAMA, zimamoto na uokoaji na programu za
upandaji miti. Lengo ni kuwa na mji wa Serikali wa kisasa utakaozingatia dhana
ya mji wa kijani na mji rafiki ili kudhibiti gharama za uendeshaji. Ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita
51.2 katika eneo hilo umekamilika kwa asilimia 99.
Ndugu Mwenyekiti, sambamba na hatua hizo, Serikali inaendelea na ujenzi
wa barabara ya mzunguko wa nje ya Jiji yenye urefu wa kilomita 112.3
ambapo sehemu ya Nala -Veyula – Mtumba - Ihumwa Dry Port ni kilomita 52.3 na
sehemu ya Ihumwa Dry Port -Matumbulu - Nala ni kilomita 60. Ujenzi huu
utakapokamilika, utakuwa umegharimu shilingi bilioni 230.4.
Ndugu
Mwenyekiti, ili kuboresha Jiji la
Dodoma kwa mawasiliano ya anga, Serikali imeanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Msalato ambapo barabara ya kuruka na kutua ndege imeanza
kujengwa.
Ndugu
Mwenyekiti, katika kuhakikisha shughuli
zote za Serikali zinafanyika makao makuu ya nchi, kwa dhamira ya dhati kabisa,
Serikali iliamua kujenga Ikulu mpya ya Chamwino, Dodoma. Na ujenzi wake
umekamilika kwa asilimia 100.
Ndugu
Mwenyekiti, ili kuhakikisha utekelezaji
wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi unaenda sambamba na maono yake, Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akifanya
ziara za kukagua miradi ya ndani na kuzungumza na wananchi ili kutatua kero zao
papo kwa papo. Kutokana na ziara hizo, miradi mingi ya maendeleo imezinduliwa
na kuwasaidia wananchi kupata huduma za msingi zikiwemo maji, umeme, barabara
na afya.
H.
Sensa
Ndugu Mwenyekiti, Serikali imekamilisha kwa mafanikio
makubwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022. Sensa hiyo ni ya kihistoria
katika nchi yetu kwa kuwa ni ya kidigitali na ilijumuisha Sensa ya Watu,
Majengo na Anwani za Makazi. Taarifa ya awali ya matokeo ya Sensa iliyozinduliwa
tarehe 31 Oktoba, 2022 inaonesha kuwa idadi ya watu ni 61,741,120. Kati
ya hao, watu 59,851,347 wapo Tanzania Bara na 1,889,773 wapo Zanzibar.
Kwa upande wa majengo, taarifa inaonesha yapo majengo 14,348,372. Kati
ya hayo, 13,907,951 yapo Tanzania Bara na 440,421 yapo Zanzibar.
I. MPANGO WA
MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19
Ndugu Mwenyekiti, mnamo tarehe 10 Oktoba, 2021 Serikali ilizindua Mpango wa Maendeleo
kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19. Mpango huo uliotokana na mkopo nafuu wa shilingi
trilioni 1.3 kutoka Shirika
la Fedha Duniani (IMF) na ulilenga kuiwezesha Tanzania kukabiliana na athari za
UVIKO-19 katika uchumi na maisha ya Watanzania. Ndugu Wajumbe, tofauti na nchi
nyingi, maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais yameiwezesha nchi yetu kutumia
fedha hizo kuinua na kuendeleza sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya,
elimu na maji.
i. Afya
Ndugu
Mwenyekiti, katika sekta ya afya, Serikali ilitoa shilingi
bilioni 466.9 kuimarisha huduma za afya na hadi sasa ujenzi wa vituo
vya afya 394 na zahanati 763 umekamilika na huduma zinatolewa.
Aidha, shilingi bilioni 136.51 zilitolewa kununua vifaa na vifaa tiba ambavyo vinaendelea kusambazwa
maeneo mbalimbali nchini. Wakati Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani,
ni hospitali mbili tu za mikoa zilikuwa na mashine za CT Scan, sasa hivi hospitali 34 zina mashine hizo zikiwemo hospitali
zote za mikoa. Kila mashine inanunuliwa kwa shilingi bilioni 2.4. Pia
magari ya wagonjwa 720 yatanunuliwa ili kuimarisha huduma za wagonjwa
nchini.
Ndugu
Mwenyekiti, leo hii, hospitali zote za rufaa
nchini zina mashine za MRI, tofauti na hapo zamani wakati nchi nzima ilikuwa na
MRI moja tu. Hii imesaidia kusogezwa karibu na wananchi huduma za
kibingwa badala ya kwenda Muhimbili, Nairobi au India kama ilivyokuwa awali.
ii.
Madarasa na Mabweni
Ndugu
Mwenyekiti, katika kufikia azma ya kuboresha sekta ya elimu, Serikali ilitoa shilingi bilioni 304 kwa ujenzi wa
miundombinu ya elimumsingi katika Halmashauri zote 184. Fedha hizi zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 12,000
katika shule za sekondari, vyumba vya madarasa 3,000 katika vituo
shikizi na mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Utekelezaji wa mpango huo umepunguza uhaba wa miundombinu ya shule katika shule
za msingi na sekondari. Pia umewezesha wanafunzi wote 907,803 waliofaulu mtihani wa darasa saba mwaka 2021 kupata
nafasi ya kuanza kidato cha kwanza Januari, 2022 bila kuwa na chaguo la pili.
iii. Uchimbaji
Visima na Mabwawa
Ndugu
Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji nchini,
Serikali ilitenga shilingi bilioni 139.4 ili kutatua matatizo ya maji. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 104.2
zimepangwa kutekeleza miradi 218; shilingi bilioni 17.5 kununua seti
25 za mitambo ya kuchimba visima; shilingi bilioni 17.6 kununua seti
5 za mitambo ya ujenzi wa mabwawa pamoja na seti 4 vifaa vya utafiti
wa maji. Mwezi Novemba, mwaka huu,
Wizara ya Maji ilikabidhiwa mitambo ya kuchimbia maji yenye thamani ya shilingi bilioni 35 ili ikafanye kazi ya kuchimba mabwawa siyo
tu kwa ajili ya wanadamu lakini pia kwa ajili ya mifugo.
Ndugu
Mwenyekiti, ili kuimarisha
ushirikiano wa kikanda na kimataifa, Serikali imeboresha mahusiano na kukuza
diplomasia ya siasa na uchumi kwa kufungua balozi mbili ambazo ni
Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Vienna - Austria na
Ubalozi wa Tanzania Jakarta, Indonesia. Pia imefungua Konseli Kuu mbili ikiwemo
jiji la Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na jiji la Guangzhou,
China na kuratibu mikutano 25 ya ubia wa maendeleo baina ya Tanzania na nchi za
Afrika, Ulaya, Amerika, Asia, Australasia na Mashariki ya Kati. Vilevile, lugha
ya Kiswahili imetambulika na kuidhinishwa kama lugha rasmi katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika na Umoja wa Afrika na
tarehe 7 Julai ya kila mwaka imetangazwa kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. Aidha,
katika kuimarisha diplomasia, Serikali iliratibu ziara 36 za viongozi wa
kitaifa nje ya nchi na ziara 11 za viongozi wa nje ya nchi waliotembelea
nchini.
K. MUUNGANO
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kulinda na kuthamini Muungano ili kudumisha umoja,
mshikamano, amani na utulivu kwa wananchi wa pande zote mbili. Katika kipindi
cha Novemba 2020 hadi Desemba 2022, Serikali iliratibu vikao vitatu vya Kamati
ya Pamoja ya SMT na SMZ na vikao 30 vya ushirikiano baina ya sekta zisizo za
Muungano za SMT na SMZ. Aidha, hoja 18
zilijadiliwa na kati ya hizo, hoja 14 zilipatiwa ufumbuzi ikiwemo
wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili na gharama za umeme kutoka
TANESCO kwenda ZECO.
L.
MICHEZO
Ndugu
Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha timu za Taifa ili ziweze kushiriki
katika mashindano ya Kimataifa na zimepata mafanikio makubwa. Timu hizo ni Tembo
Warriors iliyofika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia la
mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu na Serengeti Girls iliyofika robo
fainali ya Kombe la Dunia katika michuano ya wanawake iliyofanyika nchini
India.
Aidha, katika ngazi ya klabu, mafanikio hayo
yanajumuisha timu za Simba Queens ambayo imefanikiwa kufika hatua ya
nusu fainali ya Mashindano ya Klabu Bingwa ya Wanawake kwa upande wa Mpira wa
Miguu barani Afrika, Simba Sports Club imefika hatua ya makundi ya
michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika na Dar Young Africans iliyofika
hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
KIDUMU CHAMA
CHA MAPINDUZI
Ndugu
Mwenyekiti, baada ya kuangalia clip hiyo ninaomba sasa nihitimishe maelezo yangu:
MATARAJIO
9. Ndugu
Mwenyekiti, katika miaka mitatu iliyobaki ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka
2020, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar zitaendelea na utekelezaji wa programu na miradi mikubwa ya kimkakati
pamoja na maeneo yote yalioainishwa katika Ilani ikiwa ni pamoja na kuimarisha
utoaji wa huduma za kijamii.
10. Ndugu
Mwenyekiti, tunaendelea kuzingatia maelekezo yako ya kuboresha mazingira ya
uwekezaji nchini kwa kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji
wa masuala ya uwekezaji. Aidha, maeneo yenye changamoto yataainishwa na
kufanyiwa kazi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuendelea kupitia tozo, ada na
taratibu zote za uwekezaji. Lengo ni kuifanya nchi yetu kuwa na mazingira
shindani ya uwekezaji na biashara.
HITIMISHO
11. Ndugu
Mwenyekiti, mafanikio yote
tuliyoyapata katika kipindi hiki cha miaka miwili ya utekelezaji wa Ilani
yamechagizwa na juhudi zako binafsi pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuiongoza nchi
yetu na kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma bora. Vilevile, ni kutokana
na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Chama na Serikali.
12. Ndugu
Mwenyekiti, nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mwenyekiti na
viongozi wote wa Chama katika ngazi zote kwa kazi kubwa mliofanya na
mnayoendelea kufanya.
13. Ndugu Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
KIDUMU CHAMA
CHA MAPINDUZI
COMMENTS